Hivi karibuni mwandishi wetu wa Habari alipata fursa ya kufanya mahojiano na Mkurugenzi wa bodi ya Utalii ya Tanzania Bw. Peter Mwenguo. Katika mahojiano hayo Bw. alianza kueleza kuhusu uhusiano wa Tanzania na China katika utalii baada ya China kuiweka Tanzania katika orodha ya nchi zinazoweza kuwapokea watalii kutoka China.
Bw. Mwenguo alisema baada ya Tanzania kuwekwa kwenye orodha ya nchi zinazoweza kuwapokea watalii kutoka China, wameweza kuchukua hatua mbalimbali ambazo zinajenga misingi ya kuwavutia watalii wachina kutalii nchini Tanzania. Moja ya hatua hizo ni kubaini mawakala wa utalii wa nchini Tanzania ambao wanaweza kushirikiana na mawakala wa utalii nchini China kwa madhumuni ya biashara ya kuwaleta na kuwapokea watalii. Hatua nyingine ni pamoja na kutafsiri majarida ya utalii ya Tanzania kwa lugha ya kichina ili wachina waweze kupata taarifa zozote kuhusu utalii nchini Tanzania kwa lugha ya kichina. Hatua nyingine ni kuwafundisha watanzania lugha ya kichina ambapo mwaka huu alikuja mfanyakazi mmoja nchini kujifunza lugha ya kichina kwa mwezi mmoja chini udhamini wa serikali ya China. Bw. Mwenguo aliendelea kusema kuwa, kutokana na kutokuwepo kwa usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka nchini China hadi Tanzania na pia kutoka Tanzania kuja China, Taasisi ya wakala wa usafiri wa anga Tanzania wasaini makubaliano na serikali ya China ili kuweza kupata usafiri wa ndege wa moja kwa moja.
Akieleza kuhusu idadi ya watalii wa China wanaokwenda nchini Tanzania, Bw. Mwenguo amesema, idadi ya watalii wa China wanaoingia nchini Tanzania inaongezeka ingawa ni kwa kiasi kidogo, kwa mfano mwaka 2006 ni watalii takriban 5600 wa China waliotembelea Tanzania. Aliendelea kusema kuwa idadi hii sio kubwa ukichukulia kwamba hivi sasa China inaongoza kwa kutoa watalii wengi, kwa mfano mwaka 2006 wachina milioni 40 walizitembelea nchi mbalimbali duniani.
Hatua nyingine ni pamoja na wajumbe wa China wapatao 350 ambao walitembelea Tanzania, ili kutafuta fursa mbalimbali ikiwemo utalii, na kwa upande wa bodi ya utalii wameingia mkataba wa ushirikiano na serikali ya jimbo la Guangdong nchini China, ambapo lengo la ushirikiano huo ni kukuza mawasiliano ya utalii kati ya pande mbili na kupata watalii kutoka jimboni humo watakaotembelea Tanzania.
Aliendelea kusema kuwa vilevile sasa kuna wakala wa utalii wa China anayeshirikiana na watanzania ambapo wamefungua ofisi nchini Tanzania na nyingine nchini China, jambo ambalo litawahamasisha wachina wengi zaidi kutembelea Tanzania. Kitu kingine ni ongezeko la migahawa ya kichina nchini Tanzania, kwa mfano Dar es salaam peke yake kuna migahawa isiyopungua saba. Bw Mwenguo pia alisema, mwezi Desemba mwaka huu kutakuwa na mkutano nchini Tanzania unaolenga katika masuala ya uwekezaji ambapo kutakuwa na washiriki mia sita kutoka nchini China peke yake licha ya kuwa kutakuwa na washiriki kutoka nchi nyingine.
Akieleza ni jinsi gani Bodi ya utalii ya Tanzania inavyoshirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini kuutangaza utalii Bw. Mwenguo alisema, wamekuwa wanashirikiana kwa karibu sana na ubalozi ambapo huwaletea majarida yanahusu utalii, na ubalozi umekuwa mstari wa mbele ambapo umeyatafsiri majarida mengi katika lugha ya kichina. Na kuanzia mwaka huu wa fedha bodi ya utalii ikishirikiana na wizara ya Utalii imeazimia kutoka kiasi fulani cha fedha kwa balozi zote za Tanzania na hasa zile balozi ambazo ziko mstari wa mbele katika kuutangaza utalii na ubalozi wa Tanzania nchini China ukiwa mmoja wapo. Nia na lengo la fedha hizo kwanza ni kuboresha ofisi ambayo watalii watakuwa wakikaa wakati wakichukua viza ili iwe na hadhi na wajisikie wameengia nchini Tanzania na pia waweze kutoa vielelezo vinavyotoa taarifa za utalii nchini Tanzania. Bwana Mwenguo pia alisema Vilevile watakuwa wanatoa kanda za filamu ambazo zitakuwa zinaoneshwa mara kwa mara katika balozi, na cha muhimu zaidi kanda hizo zitakuwa na lugha inayotumika katika nchi husika
|