Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-12 14:43:35    
Wachoraji ndugu wawili Zhou

cri

Ndugu wawili Zhou ni wachoraji mashuhuri duniani, mtindo wao wenye uvumbuzi wa kijasiri, uchoraji wao wa picha, ufinyanzi wa sanamu na uchongaji picha kwenye mbao unawavutia na kuwastaajabisha sana watazamaji.

Ndugu hao wawili mmoja ni kaka, anaitwa Zhou Shanzuo, mwingine ni mdogo wake anaitwa Zhou Dahuang. Ndugu hao walizaliwa miaka ya 50 ya karne iliyopita katika wilaya ijiendeshayo ya kabila la Wazhuang mkoani Guanxi. Kwao kwenye genge la mlima kuna picha kadhaa za watu wa kale na wanyama ambazo zilichorwa kwa mtindo wa ajabu na zimekuwa na miaka zaidi ya elfu mbili. Bw. Zhou Dahuang alisema,

"Nilipokuwa mtoto baba yangu alinitembeza kwa mashua kwenye Mto Ming, niliona picha zilizochorwa kwenye magenge, niliona ajabu sana na nakumbuka mpaka sasa. Baadaye niliamua kufuata maisha ya usanii, nilipojaribu kutafuta mtindo wangu, ule mtindo wa picha kwenye genge ulinipa mwangaza."

Bw. Zhou Dahuang alisema, baadaye alifahamu kwamba kwenye usanii wa mwanzoni mila ya usanii ya kwao ilikuwa na athari kwao pole pole bila wao kujua. Mwanzoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita picha zao zilianza kujulikana nchini China. Mwaka 1986 ndugu hao wawili walikwenda Marekani kwa lengo la kujifunza uchoraji wa Kimagharibi. Tokea wakati huo Bw. Zhou Shanzuo ambaye alikuwa na umri wa miaka 34 na ndugu yake Zhou Dahuang mwenye umri wa miaka 29 walianza kusafiri katika njia pana zaidi ya sanaa nchini Marekani.

Wasanii hawawezi kufanikiwa mpaka wawe na mitindo yao maalumu, lakini si rahisi hata kidogo kujipatia mitindo tofauti na wengine. Ndugu hao wawili hawakufuata mkondo wa nyanja ya uchoraji nchini Marekani wala mkondo ulioenea duniani, bali walifyonza viturubisho walivyohitaji kwa kuvichagua. Picha zao kwa wingi zaidi zinachorwa kwenye kitambaa kikubwa kama pazia la kuoneshea filamu, wanamwaga rangi kwenye kona ya kitamba hicho, kisha huku wakitumbuizwa kwa kutumbuizwa muziki wanatumia brashi kubwa kupakapaka rangi na kuchorachora, watazamaji hawafahamu watachora picha gani. Baada ya nusu saa au saa moja hivi, kwenye kitambaa sura zinazofanana na binadamu au alama za ajabu zinatokea na kuwavutia watazamaji. Tokea mwaka 1994 ndugu hao wawili walianza kuchora picha kwenye jukwaa mbele ya watazamaji ili kuonesha jinsi wanavyochora picha.

Mwezi Septemba mwaka huu walifanya maonesho ya picha walizochora katika muda wa miaka 30 iliyopita katika Jumba la Maonesho ya Sanaa la Beijing, na kuchora picha mbele ya watazamaji katika Jumba la Muziki la Zhongshan mjini Beijing. Mfadhili wa duka la picha za ndugu wawili Zhou Bw. Nicole Caros aliyetoka Marekani ni shabiki wao. Alisema,

"Nimekuja kutoka Chicago, naona picha wanazochora zina nguvu kubwa ya kunivutia! Watu wa Chicago wote wanawapenda sana."

Ingawa wao ni ndugu wa tumbo moja lakini tabia zao ni tofauti kabisa. Msaidizi wa msimamizi wa duka la picha Bw. Dara Ola alisema, wakati walipochora picha, mmoja huharibu picha ya mwenzake ambayo inakaribia kukamilika na mara nyingi uharibifu huo unasababisha picha nyingine za ajabu. Alisema,

"Mara nyingi Zhou Dahuang alipokuwa anamaliza kuchora sehemu fulani kwenye kitambaa, kaka yake Zhou Shanzuo alikuja na kufuta sehemu yote na kuanza kuchora upya. Nadhani hii inasaidia sana kuinua kiwango cha usanii wao."

Ndugu hao wawili wameshirikiana kwa miaka 30, baadhi ya picha zilikamilishwa na watu wawili. Ni vigumu kuelewa kwamba watu wawili wenye tabia tofauti wanawezaje kuchora picha moja inayovutia sana. Bw. John Clark ni rafiki yao wa zaidi ya miaka kumi alisema,

"Hata mimi siamini kama nimeweza kushirikiana vizuri na ndugu yangu kwa muda mrefu kama huo. Ni vigumu kwa wasanii kupokea maoni ya watu wengine. Naona urafiki kati ya ndugu hao si wa kawaida."

Ndugu hao wawili walisema, mwanzoni walikuwa wana matumaini ya kuelewana sana katika uchoraji, baadaye walielewa kwamba ni kawaida kuwa na tofauti katika mtazamo wa sanaa, na tofauti hiyo kwa kiasi fulani inaleta matokeo mazuri na ya kustaajabisha. Kitu kinachowapatanisha ni moyo wa kutoridhika na kiwango cha usanii walicho nacho.

Picha zinazochorwa na ndugu wawili Zhou zinaivutia jamii ya wahifadhi wa picha, picha moja inaweza kuuzwa kwa dola za Kimarekani milioni tano. Vyombo vya habari vinasema wachoraji hao wamekuwa kwenye kiwango cha juu kabisa duniani. Watu wasiowafahamu pengine wanaona wana tamaa ya kujipatia sifa tu na wanafahamu sheria ya soko la sanaa. Lakini Bw. Zhou Shanzuo anaona kuwa mafanikio yao hawakuyatarajia. Alisema,

"Kwa kweli hatukufikiria sana kuhusu biashara ya picha tunazochora, sisi wawili si watu hodari wa biashara. Cha muhimu ni picha zetu zimewavutia wahifadhi wa picha duniani, matokeo hayo hatukuwahi kuyategemea."

Hivi sasa licha ya wakuu wa makampuni makubwa kuhifadhi picha zao, hata wanasiasa na wasanii pia wanashabikia picha zao. Mwigizaji nyota wa filamu Marlon Brando aliwahi kuonesha picha zilizochorwa na ndugu hao katika karamu ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Mwaka 1994, ndugu wawili walianzisha mfuko ili kuwasaidia wachoraji na washairi wa China walioanza kwenda Marekani kuanzisha ofisi zao na maingiliano ya sanaa. Hivi sasa licha ya kuwa wameanzisha kituo cha sanaa pia wamekuwa na bustani yenye sanamu walizofinyanga. Bw. Zhou Shanzuo alieleza,

"Miaka kadhaa iliyopita tulianzisha kituo cha sanaa, jumba la kituo hicho lina eneo la mita za mraba elfu tisa likiwa ni pamoja na sehemu ya maonesho na sehemu za shughuli mbalimbali za sanaa. Miaka kadhaa iliyopita tulijenga bustani yenye sanamu tulizofinyanga, kwenye bustani hiyo tuliwahi kupokea washairi, waongozaji na waigizaji wa filamu kutoka nchi mbalimbali kwenye sherehe za aina mbalimbali za sanaa."

Ndugu hao wawili wanapojitokeza hadharani huwa na jina la "Ndugu Wawili Zhou", na jina lao huwa ni "Zhou B".

Idhaa ya kiswahili 2007-11-12