Mkutano wa Kimataifa kuhusu kuutangaza Utalii duniani ulifanyika hivi karibuni hapa Beijing, wajumbe kutoka nchi zote wanachama wa Shirika la Utalii duniani (WTO) walishiriki kwenye mkutano huo. Radio China Kimataifa ilipata fursa ya kufanya mahojiano na Katibu Mkuu wa wizara ya Utalii Tanzania Bibi Blandina Nyoni, aliyekuwepo hapa Beijing kuhudhuria mkutano huo. Bibi Nyoni alizungumzia mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na hali ya Utalii nchini Tanzania na uhusiano kati ya Tanzania na China kwenye mambo ya Utalii.
Bibi Nyoni alisema Mkutano huo umewafundisha mambo mengi washiriki waliotoka Tanzania, kwanza waliweza kukutana na watu kutoka nchi nyingine ambao wameendelea zaidi katika kuutangaza Utalii, na hivyo waliweza kujifunza baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kusaidia kuutanganza zaidi utalii wa Tanzania. Vilevile ilikuwa ni nafasi nyingine nzuri kwa watu wanaofanya kazi kwenye sekta ya Utalii Tanzania kujionea ukubwa wa soko la China, na kupata nafasi ya kutangaza vivutio na huduma zilizopo kwa makampuni ya Utalii ya China yanayotaka kutuma watalii Tanzania. Mbali na kupata fursa ya kutembelea sehemu za utalii na kujionea jinsi China inavyoendesha utalii wake, pia washiriki kutoka Tanzania waliweza kujionea jinsi China inavyohimiza soko la ndani la Utalii.
Tanzania ilipewa heshima ya kuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa wizara ya Utalii Tanzania Bibi Blandina Nyoni alisema, "sababu iliyoifanya Tanzania ipewe heshima ya kuwa mwenyekiti wa mkutano huo, kwanza hii ilikuwa ni zamu ya Afrika kuwa mwenyekiti wa Mkutano huo, na pili waliichagua Tanzania kutokana na juhudi ambazo Tanzania imekuwa inazifanya katika kuutanganza na kuuboresha utalii, na kuwa na utulivu. Watanzania wamefurahia na kuona wanathamini kwa kupewa dhamana ya kuwa mwenyekiti wa mkutano huo"
Katibu Mkuu wa wizara ya Utalii Tanzania Bibi Blandina Nyoni, pia alizungumzia ushirikiano kati ya China na Tanzania kwenye sekta ya utalii. Alisema zamani kulikuwa na uhusiano wa kisiasa zaidi, lakini katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano kati ya China na Tanzania umeendelea zaidi na kuingia kwenye mambo ya biashara na hata utalii. Zamani wengi waliifahamu China kutokana na miradi ya ujenzi kama TAZARA na miradi mingine, hivi sasa watalii wa China pia wanakuja Tanzania na inatarajiwa kuwa itaendelea kuongezeka.
Pamoja na hayo, tatizo kubwa ambalo linalofanya kuwa na idadi ndogo ya watalii kutoka China ni miundo mbinu ikiwa ni pamoja na hoteli na huduma zinazotolewa kwenye mbuga za utalii, na kutokuwa na usafiri wa moja kwa moja kati ya China na Tanzania. Bibi Nyoni alisema, "serikali ya Tanzania imeona hali hiyo, na sasa inafanya juhudi za kuboresha miundo mbinu ya kwenye mbuga za wanyama, na tayari mahoteli yanajengwa na barabara zinaendelea kujengwa, na pia juhudi za kuhakikisha kuwa kuna usafiri wa moja kwa moja kati ya China na Tanzania zinafanyika, na tayari mkataba kati ya Shirika la ndege la Tanzania na Shirika la ndege la China umesainiwa, na utekelezaji wake utaanza baada ya hali ya Shirika la ndege la Tanzania kutengemaa"
Na kuhusu usalama wa watalii, Bibi Nyoni alisema wizara ya Utalii ya Tanzania kwa kushirikiana na idara nyingine za serikali, wameanzsiha utaratibu wa kuwa na kikosi cha pamoja usalama kinachoshirikisha askari wa Jeshi la Polisi na askari wanaolinda wanyamapori, kikosi hiki kimekuwepo kwa muda sasa, na vitendo vya uhalifu dhidi ya watalii na ujangili kwenye mbuga za wanyama vimepungua, lakini juhudi zinaendelea ili kufanya usalama uwe mkubwa zaidi.
Alipozungumzia kuhusu Chuo Kikuu cha Utalii duniani ambacho kinatarajiwa kujengwa huko Dar es salaam nchini Tanzania Bibi Nyoni alisema Chuo Kikuu hicho kimeamuliwa kujengwa Tanzania lakini hakitakuwa ni Chuo kwa ajili ya watanzania peke yao, bali kitakuwa ni chuo kwa ajili ya watu kutoka sehemu mbalimbali duniani, na watanzania watatakiwa kwa kuwa na sifa kama ilivyo watu kutoka nchi nyingine.
|