"Xugong Xugong, itakusaidia kuelekea kwenye mafanikio". Hili ni tangazo linalofahamika kote nchini China. "Kundi la Xugong" ni ufupi wa jina la Kichina la kundi la viwanda vya kutengeneza mashine la Xuzhou, hivi sasa kundi hilo limekuwa linaongoza katika sekta ya uzalishaji wa mashine nchini China. Lakini kundi la Xugong halikuridhika na mafanikio liliyopata katika miaka 18 iliyopita, na sasa linatupia macho kwenye soko la kimataifa lililo kubwa zaidi.
Kundi la Xugong lilianzishwa mwaka 1989. Mwanzoni mapato ya kundi hilo kwa mwaka yalikuwa Yuan za RMB milioni 300 tu, lakini mwaka huu mapato ya kundi hilo yanatazamiwa kufikia zaidi ya Yuan za RMB bilioni 30, na mapato ya fedha za kigeni kutokana na uuzaji bidhaa nje ya nchi yanafikia dola za kimarekani milioni 500, na kulifanya Kundi hilo kuwa kampuni kubwa kabisa ya kuendeleza, kutengeneza na kuuza mashine nchi za nje nchini China. Lengo la kundi la Xugong ni "kuongoza kati ya viwanda vya kutengeneza mashine nchini China, kuwa mshindani mwenye nguvu katika soko la mashine, na kutimiza kuwa kundi la kisasa lenye nguvu kubwa."
Mkuu wa kundi la Xugong Bw. Wang Min alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, mafanikio ya hivi sasa ya kundi hilo hayawezi kutengana na mkakati wa kufanya juhudi kuvumbua chapa maarufu. Alisema,
"Chapa maarufu zinaonesha nguvu ya kampuni, sifa ya bidhaa, huduma na utamaduni wa kampuni hiyo, na ni lazima kampuni itegemee nguvu ya chapa yake katika kuinua nguvu ya ushindani ya bidhaa zake na kushinda kwenye soko."
Bw. Wang Min alisema, msingi wa chapa cha "Xugong" ni sifa nzuri ya bidhaa, ambayo ni pamoja na teknolojia ya kisasa, sifa bora ya wafanyakazi, utaratibu mzuri wa uhakikisho wa sifa ya bidhaa, na huduma bora baada ya mauzo, pia ni pamoja na kutenga fedha nyingi, kujitangazia vizuri kwenye nchi za nje na kuwa mkakati wenye mafanikio wa mauzo.
Kwa kweli, mwaka 2004 uzalishaji na uuzaji wa mashine kubwa zilizotengenezwa na kampuni ya Xugong "ulikuwa wa kwanza duniani", lakini mashine nyingi kabisa ziliuzwa nchini China, na soko la kimataifa bado lilikuwa linadhibitiwa na makampuni ya Ujerumani, Marekani na Japan. Bw. Wang Min aliona kuwa, kama kampuni ya Xugong haitaweza kung'ara katika soko la kimataifa, basi hata likiongoza katika soko la China, bado "halitakuwa la kwanza duniani". Pia aliona kuwa, bado kuna njia ndefu ya kuifanya chapa maarufu ya China "Xugong" kuwa chapa maarufu duniani. Alisema,
"Kwanza bidhaa hizo ni lazima zielekee kwenye soko la nje. Bidhaa hizo zinapaswa kulingana na mahitaji ya soko la kimataifa na wateja duniani, na kuelekezwa na soko. Wakati bidhaa zake zinaelekea kwenye soko la nje, mtandao wa huduma za vipuri unapaswa kufuata, ili ufanisi wa wateja wa nchi za nje uinuke kutokana na kutumia mashine maarufu ya 'Xugong' ya China. Pili ni lazima watu waende nje, na kuanzisha kituo cha utafiti katika nchi za ng'ambo, kuweka jukwaa la teknolojia, ili 'Xugong' siku zote iweze kufuata teknolojia ya kisasa kabisa ya mashine. Tatu ni lazima kampuni iende nje, kutokana na hatua hizo mbili, kampuni inaweza kuelekea kwenye soko la kimataifa katika wakati unaofaa. Hatua hizo zinaweza kuzifanya bidhaa za 'Xugong' kuwa chapa maarufu duniani siku hadi siku."
Hivyo kundi la Xugong lilitunga mkakati wa maendeleo wa dunia nzima, ambao kwanza ni kuingia katika soko la nchi zinazoendela na nchi jirani, halafu kuingia kwenye soko la nchi zilizoendelea. Kutokana na mwongozo wa mkakati huo, kundi la Xugong linafanya ushirikiano na wakala wa nchi za nje, hivyo linapanua njia na eneo la uuzaji bidhaa nje.
Kuonesha bidhaa za kampuni na sura ya kampuni kwenye jukwaa la kimataifa ni sehemu muhimu ya mkakati wa kundi la Xugong. Katika miaka ya hivi karibuni, "Xugong" imeonesha bidhaa zake kwenye maonesho mengi ya kimataifa ya mashine za uhandisi nchini Marekani, Ujerumani na Afrika ya Kusini.
Na msimamo huo wa kufungua mlango wa "Xugong" pia unavutia makampuni mengine duniani. Wajumbe wa makampuni ya kimataifa ya Marekani, Ujerumani na Korea ya Kusini walikuja kufanya ushirikiano zaidi na "Xugong", ili kujiendeleza pamoja kwenye soko la kimataifa. Hivi sasa kundi la "Xugong" limeanzisha makampuni kumi kadhaa za ubia na Viwanda vya Caterpillar, Liebherr na Thyssenkrupp, na bidhaa za "Xugong" zinauzwa katika nchi na sehemu zaidi ya 80.
Wakati huohuo, "Xugong" inatambua kuwa, bado kuna tofauti kati yake na baadhi ya makampuni maarufu za kimataifa kuhusu uzoefu wa usimamizi, utafiti wa bidhaa na uendelezaji wa biadhaa. Bw. Wang Min alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, baada ya kuchambua na kujiangalia, wamegundua kuwa udhaifu mkubwa wa "Xugong" ni kukosa nguvu kubwa za ushindani na vipuri muhimu vya kimsingi. Sasa nchini China kuna makampuni karibu 2,000 ya kutengeneza mashine, lakini makampuni hayo yote hayana teknolojia zake za kiini na baadhi ya vipuri muhimu. Wateja wa nchi za nje hawakubali vipuri vinavyotengenezwa na China, wanasisitiza kutumia vifaa vyenye chapa maarufu za kimataifa. Bw. Wang Min alisema, hatua ijayo ya "Xugong" ni kuendeleza utengenezaji wa vipuri muhimu vyenye thamani ya nyongeza na vyenye teknolojia ya hali ya juu. Alisema katika siku zijazo, "Xugong" itahimiza kuinua sifa na ufanisi kwa kuinua teknolojia. Alisema,
"Kwa kuinua uwezo wa ushindani wa kiini, sio kwa kuendeleza ufanisi kwa maeneo bali kuendeleza ufanisi kutokana na sifa nzuri, kufanya hivyo "Xugong" inaweza kupata nafasi kubwa zaidi kwenye soko la kimataifa, na chapa ya 'Xugong' kuweza kutambuliwa na kuwa na sifa nzuri kwa wateja duniani."
Ili kutimiza lengo la kuelekea kwenye soko la kimataifa na kushiriki kwenye ushindani wa kimataifa Bw. Wang Min alisema, ni lazima kundi la Xugong lifanye maandalizi ya kutosha. Alisema,
"Ni lazima tuendelee kufuata sera ya mageuzi na ufunguaji mlango, kutumia vizuri teknolojia za makampuni ya kimataifa. Lakini katika mchakato huo, ni lazima tudumishe mwelekeo wetu wenyewe, yaani uwezo wa usimamizi wa kujitegemea na kuwa na chapa yetu yenyewe, haviwezi kubadilika."
Idhaa ya kiswahili 2007-11-13
|