Maendeleo ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing
Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha Sanduku la barua. Michezo ya 29 ya Olimpiki ya majira ya joto itafunguliwa mwezi Agosti mwaka 2008. Ili kuwawezesha wasikilizaji wetu waelewe vizuri zaidi na kushiriki kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 na kuenzi moyo wa Michezo ya Olimpiki, kuanzia tarehe 1 Novemba mwaka 2007 hadi tarehe 25 Aprili mwaka 2008, idhaa mbalimbali za Radio China Kimataifa zinatangaza makala 4 za Mashindano ya chemsha bongo yasemayo: "Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki", makala hizo zinahusu "Maendeleo ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing", "Mwito wa Kauli mbiu ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing na Fuwa wa alama ya Baraka ya michezo hiyo", Viwanja na majumba ya michezo vya Michezo ya Olimpiki ya Beijing" na "Miji mingine itakayoshirikiana na Beijing kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008".
Kama ilivyokuwa kwenye mashindano ya miaka iliyopita, kila baada ya kusoma makala moja, tutauliza maswali mawili. Baadaye kamati yetu ya uthibitishaji itachagua wasikilizaji washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu pamoja na nafasi maalum. Kila mshiriki wa mashindano hayo ya chemsha bongo atapata kadi moja ya kumbukumbu; washindi watakaopata nafasi za kwanza, pili na tatu watapewa kadi ya kumbukumbu na zawadi; na wasikilizaji washindi watakaopata nafasi maalum wataalikwa kuja China, ambapo watapewa tuzo ya kikombe na kadi, watatembelea mji wa Beijing kwa siku 10, watatembelea viwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki na kukutana na wachezaji maarufu wa China.
Kuanzia leo tarehe 11 Novemba, kwenye Kipindi cha Sanduku la Barua, Idhaa ya Kiswahili inaanza kutangaza makala nne za mashindano ya chemsha bongo yasemayo: "Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki. Na matangazo ya makala hizo nne yatarudiwa kuanzia tarehe 9 Desemba mwaka huu, msikose kutusikiliza".
Wasikilizaji wapendwa, sasa tunawaletea makala ya kwanza inayosema: "Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing yanaendelea vizuri".
Wasikilizaji wapendwa, tarehe 13 Julai mwaka 2001, kwenye Mkutano wa 112 wa wajumbe wote wa Kamati ya kimataifa ya Michezo ya Olimpiki uliofanyika huko Moscow, Russia, mji wa Beijing ulipewa nafasi ya kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya siku za joto ya mwaka 2008. Hii ni mara ya kwanza kwa Michezo ya Olimpiki kufanyika nchini China. Mwezi Desemba mwaka 2001, Kamati ya maandalizi ya Michezo ya 29 ya Olimpiki ya Beijing ilianzishwa, ambapo kazi ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ilianza rasmi. Michezo ya Olimpiki ya Beijing itafanyika kuanzia tarehe 8 hadi 24 Agosti mwaka 2008. Hivi sasa imebaki miezi 9 hivi kabla ya kufunguliwa kwa michezo hiyo. Naibu mwenyekiti mtendaji wa Kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki Bwana Wang Wei hivi karibuni alijulisha hali ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2008 mjini Beijing.
Beijing, maana ya kichina ni "mji mkuu wa sehemu ya kaskazini", mji huo umekuwa na historia ya zaidi ya miaka 3,000, ambao ulikuwa mji mkuu katika enzi tatu za China ya kale za Yuan, Ming, na Qing katika historia, na baada ya kuzaliwa kwa Jamhuri ya watu wa China mwaka 1949, Beijing imekuwa mji mkuu wa China mpya. Beijing ya hivi leo ni mji mkubwa wa kisasa wenye idadi ya watu milioni 13.
Historia ndefu imeacha mabaki mengi ya utamaduni wenye thamani kubwa mjini Beijing. Ukuta mkuu ambao ulisifiwa kuwa mwujiza duniani, sehemu yake yenye kilomita mia kadhaa inatambaa kwenye ukanda wa Beijing; Bustani ya Yiheyuan yaani Bustani ya majira ya joto (summer palace) ni bustani murua ya kifalme katika zama za kale za China; Kasri la kifalme ni kasri kubwa kabisa lenye majumba mengi ya kifalme duniani; Bustani ya Tiantan ni mahali pa kufanya matambiko kwa mungu wa mbingu kwa wafalme, bustani hiyo ni jengo lililojengwa kwa kufuata usanii murua wa ujenzi wa zama za kale za China. Na majengo hayo manne ya kale tuliyotaja yote yameorodheshwa na Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa urithi wa utamaduni duniani. Na vichochoro vingi vya Beijing ya kale pamoja na makazi ya Siheyuan, ni kama ushahidi wa historia ya maisha ya wakazi wa Beijing katika karne kadhaa zilizopita, ingawa kutokana na maendeleo ya mji, vichochoro vya kale na makazi ya Siheyuan mjini Beijing vimepungua siku hadi siku.
Mwaka 2001, Beijing ilikubaliwa kuwa mwenyeji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008. Katika miaka 6 iliyopita, Beijing imefanya juhudi kubwa sana ili kuandaa Michezo ya Olimpiki. Naibu mwenyekiti mtendaji wa Kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing Bwana Wang Wei alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, baada ya kuanzishwa kwa Kamati ya Mandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, kamati hiyo inachapa kazi kwa juhudi kubwa, ikilenga kuandaa Michezo ya Olimpiki yenye umaalum na ya kiwango cha juu. Bw. Wang alisema: (??)
"kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 yenye umaalum na ya kiwango cha juu ni ahadi tuliyotoa kwa makini kwa dunia, pia ni matakwa na matarajio ya serikali ya China na wananchi wa China. Kwa ujumla hivi sasa kazi mbalimbali za maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing zinaendelea vizuri kama ilivyopangwa".
Bwana Wang alisema, ili kuandaa Michezo ya Olimpiki yenye umaalumu na ya kiwango cha juu, China inatakiwa kufanya kazi za pande nane. Kwanza ni lazima ijenge viwanja na majumba ya michezo ya kiwango cha juu na kufanya maandalizi ya michezo kwenye kiwango cha juu. Pili ni lazima ifanye maandalizi ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki ya kiwango cha juu pamoja na shughuli za utamaduni. Tatu ni lazima kutoa huduma bora kwa vyombo vya habari na kupata tathmini nzuri kutoka kwa maoni ya watu. Nne ni lazima kufanya kazi ya ulinzi wa usalama kwenye kiwango cha juu. Tano ni lazima kuwa na watu wanaojitolea ambao wataweza kutoa huduma za kiwango cha juu. Sita ni lazima kuandaa hali ya kiwango cha juu ya mawasiliano barabarani na kutoa huduma za maisha za kiwango cha juu. Saba ni kuwa na sura ya ustaarabu wa mji wa kiwango cha juu. Nane ni kuhakikisha wanamichezo wa nchi mbalimbali wanajipatia mafanikio makubwa.
Baada ya kufanya maandalizi yenye pilikapilika katika miaka karibu 6 iliyopita, lengo la kuandaa Michezo ya Olimpiki ya Beijing kuwa michezo yenye umaalum na kiwango cha juu linakaribia kutimizwa siku hadi siku. Bwana Wang Wei alisema ujenzi wa Uwanja wa michezo wa taifa, ambao ni kazi kubwa zaidi katika maandalizi ya michezo, mwendo wake unaifanya Kamati ya kimataifa ya Olimpiki isiwe na wasiwasi. Hivi sasa ujenzi wa viwanja na majumba 10 kati ya 37 ya michezo umekamilika. Mbali na Uwanja wa michezo wa taifa ambao ujenzi wake utakamilika mwanzoni mwa mwaka 2008 kutokana na mahitaji ya mradi wa kuandaa sherehe ya ufunguzi wa michezo, ujenzi wa majumba na viwanja vingine vya michezo vyote utakamilika mwishoni mwa mwaka 2007. Bwana Wang Wei alisema, kazi nyingine za maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing pia zinawafurahisha watu. Hivi sasa kazi ya kuandaa mashindano kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing inaendelea kwa kina, ratiba za mashindano yote zimepangwa; kazi ya utungaji wa sherehe ya ufunguzi na ufungaji wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing imekamilika kimsingi, na itaingia katika kipindi cha maandalizi ya mwisho hivi karibuni, na mwongozaji wa filamu maarufu Bwana Zhang Yimou ni mwongozaji mkuu wa sherehe ya ufunguzi wa Michezo ya Olimpiki. Aidha mpango wa njia ya kukimbiza mwenge wa Michezo ya Olimpiki pia umetangazwa. Katika njia ya kukimbiza mwenge huo, Beijing inajaribu kuufanya mwenge huo ufike kwenye Mlima Qomolangma ambao ni kilele cha juu kabisa duniani, ubunifu huo unawafanya walimwengu wawe na taswira nzuri kuhusu shughuli za kukimbiza mwenge zitakazoanza mwakani.
Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing yameungwa mkono na wakazi wa Beijing na wananchi wa China wenye uchangamfu. Hali hii imejionesha vilivyo katika kuwaandikisha watu wanaojitolea kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Michezo hiyo inahitaji watu wanaojitolea wapatao laki moja hivi, lakini ilipofika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, idadi ya watu waliotoa maombi imefikia zaidi ya laki 5. Kati yao asilimia 90 ya watu waliotoa ombi ni wa sehemu mbalimbali za China bara, uchangamfu mkubwa wa wananchi wa China kwa Michezo ya Olimpiki umeipa picha nzuri Kamati ya kimataifa ya Michezo ya Olimpiki. Bwana Wang Wei alisema: (??)
"Kazi ya kuwaandikisha watu wanaojitolea kwenye Michezo ya Olimpiki na Michezo ya Olimpiki ya walemavu ya mwaka 2008 imeanzishwa katika mikoa 31, miji na mikoa inayojiendesha katika China bara, pia imeanza kufanyika katika mikoa ya Hongkong na Makau, kisiwani Taiwan na sehemu za ng'ambo. Ilipofika mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu, idadi ya watu waliotoa ombi ilizidi laki 5.6. Tunaamini kuwa, idadi ya watu wanaojitolea kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing itakuwa ya kutosha tena watu hao watatoa huduma za kiwango cha juu".
Mji ukiwa mwenyeji wa kuandaa Michezo ya Olimpiki unapaswa kuwa na hali nzuri ya mawasiliano na mazingira mazuri. Maendeleo makubwa yamepatikana mjini Beijing katika hali ya mawasiliano na mazingira ya mji katika miaka ya hivi karibuni. Katika miaka 6 iliyopita, ili kupunguza shinikizo la mawasiliano kwenye Michezo ya Olimpiki, Beijing imeharakisha ujenzi wa mawasiliano kwenye njia ya subway. Njia ya No. 5 ya subway imezinduliwa mwezi Oktoba mwaka huu, na kazi zote za ujenzi wa njia za subway No.4 na No.10 pamoja na njia ya kurukia ndege kwenye uwanja wa ndege zitakamilika mwaka 2008, ambapo njia ya subway mjini Beijing itakuwa na urefu wa kilomita 200, hii ni rekodi mpya katika historia yake, ambayo itatoa uhakikisho wa kutegemewa kwa mawasiliano ya umma wakati wa Michezo ya Olimpiki.
Wakati huo huo, maendeleo yamepatikana katika kazi za kuboresha mazingira ya mji wa Beijing. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwishoni mwa mwaka 2006, Beijing imetenga dola za kimarekani bilioni 12.2, na kukamilisha miradi mikubwa 20 ya kushughulikia hali ya mazingira. Siku zenye hewa safi mjini Beijing ziliongezeka kuwa 241 mwaka 2006 kutoka siku 100 za mwaka 1998; eneo lenye miti na majani limefikia asilimia 42 mwaka 2006, na hakika eneo hilo litafikia zaidi ya asilimia 43 mwaka 2008; na maji taka yanayoshughulikiwa yamefikia asilimia 90. Bw. Wang Wei akijulisha alisema: (??)
"Hali ya mawasiliano barabarani na mazingira ya asili mjini Beijing yameboreshwa zaidi. Hivi sasa mjini Beijing inatekelezwa hatua ya kuuza tikiti za bei chini kwenye mawasiliano ya umma, hali ya mawasiliano ya umma imeboreshwa zaidi, tunajitahidi kutekeleza wazo la kuandaa Michezo ya Olimpiki katika mazingira yasiyo na uchafuzi, kujitahidi kuboresha hewa na maji mjini, kuboresha mazingira ya utamaduni mjini, na kuifanya jamii iwe na masikilizano zaidi".
Bwana Wang Wei alisema katika muda uliobaki kabla ya kufunguliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, Beijing ikifuata kanuni na desturi za michezo hiyo duniani, na maagizo mbalimbali ya serikali ya China kuhusu maandalizi ya Michezo ya Olimpiki, itaharakisha kazi za pande mbalimbali. Alisema:
"Tuna matumaini ya dhati kuwa, marafiki zetu wa nchi mbalimbali wataweza kufuatilia zaidi na kushiriki kwenye kazi mbalimbali za maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, tutafanya juhudi kwa pamoja ili kuifanya Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itakayofanyika mjini Beijing iwe michezo ya Olimpiki yenye umaalum na kiwango cha juu, kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo makubwa ya Michezo ya Olimpiki, na kujenga dunia nzuri zaidi yenye masikilizano".
Wasikilizaji wapendwa, sasa tunatoa maswali mawili:
1. Lengo la kazi ya Kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ni lipi?
2. Michezo ya Olimpiki ya Beijing itafunguliwa tarehe ngapi na itafungwa tarehe ngapi?
Idhaa ya kiswahili 2007-11-13
|