Mjumbe wa kabila la Watibet kwenye mikutano mikuu ya Chama cha Kikomunisti cha China Bw. Gesangdunzhu
cri
Miongoni mwa wajumbe zaidi ya 2200 waliohudhuria mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China uliofanyika hivi karibuni, wajumbe zaidi ya 200 wanatoka kwenye makabila madogo madogo. Mkurugenzi wa kamati ya mambo ya makabila madogo madogo ya mkoa wa Yunnan Bw. GeSangdunzhu, ambaye alichaguliwa kuwa mjumbe wa kabila la Watibet kwenye mikutano mitatu mikuu mfululizo ya Chama cha Kikomunisti cha China. Wilaya inayojiendesha ya kabila la Watibet ya Diqing iko kaskazini magharibi mwa mkoa wa Yunnan, watu wa makabila 26 yakiwemo makabila ya Watibet, Walisu, Wanaxi na Wahan wanaishi kwenye wilaya hiyo. Wilaya ya Diqing inajulikana duniani kutokana na mji mkuu wake Shangri-la, ina mandhari nzuri ya misitu, maziwa kwenye mbuga na milima yenye vilele vyenye theluji. Kila mwaka Diqing inawavutia watalii karibu milioni moja kutoka nchini na nchi za nje. Lakini kwa miaka zaidi ya kumi iliyopita, miundo mbinu ya Diqing ilibaki nyumma sana kimaendeleo, na hali duni ya mawasiliano ya barabara ilizuia maendeleo ya Diqing. Bw. Gesangdunzhu alisema, "Mimi pamoja na watu wote wa familia yangu tulikaa kando ya uwanja wa ndege kwa saa moja na zaidi, tuliangalia ndege zikiruka na kutua. Binti yangu aliniuliza kwa nini tunafanya hivyo, nilimjibu uwanja wa ndege utajengwa kwenye maskani yetu." Mwaka 1991, Bw. Gesangdunzhu ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa wilaya ya Diqing kwa kutumia fursa ya kwenda masomoni huko Kunming, mji mkuu wa Yunnan, alitembelea uwanja wa ndege wa Kunming, kwa kuwa kuboresha hali ya mawasiliano ya barabara ni matumani yake ya siku zote. Bw. Gesangdunzhu aliona kuwa, Diqing iko katikati ya mikoa mitatu ya Yunan, Sichuan na Tibet, ina mandhari nzuri na maliasili nyingi za utalii, endapo uwanja wa ndege unajengwa, muda wa wakati ya kusafiri kati ya Kunming na Diqing ungepungua kuwa dakika hamsini kutoka siku mbili au tatu, mawasiliano ya barabara yangeboreshwa, basi Diqing ingekuwa na maendeleo makubwa. Mpango wa Bw. Gesangdunzhu kuhusu kujenga uwanja wa ndege kwenye wilaya ya Diqing haukuelewa kwa watu wengi. Wengine walisema Diqing haina barabara nzuri, sembuse uwanja wa ndege, na wengine walisema hakuna haja ya kujenga uwanja wa ndege, kwa kuwa wilaya ya Diqing ina idadi ya watu laki tatu tu. Lakini Bw. Gesangdunzhu hakurudi nyuma, alitumia fursa yoyote aliyepata kufafanua umuhimu wa kujenga uwanja wa ndege, baada ya jitihada kubwa, mradi wa ujenzi wa uwanja huo uliidhinishwa na serikali kuu ya China. Kama ilivyotarajiwa na Bw. Gesangdunzhu, uwanja wa ndege ulileta mabadiliko makubwa kwa wilaya ya Diqing. Mwaka 1991, watu waliotalii kwenye sehemu ya Diqing hawakufikia elfu kumi, na mapato yote ya wilaya ya Diqing yalikuwa yuan zaidi ya milioni 40, lakini baada ya kuzinduliwa kwa uwanja huo, mwaka 1999 watalii kwa Diqing walikuwa milioni 1.12, na mapato kutokana na utalii yaliongezeka na kuwa yuan milioni 540. Bw. Gesangdunzhu alizaliwa katika familia moja maskini kwenye wilaya ya Diqing, ana hisia maalumu kwa maskani yake. Aidha akiwa mwanachama wa Chama tawala cha Kikomunisti cha China, anaona kuwa kuendeleza wilaya ya Diqing na kuboresha maisha ya wakazi wa sehemu hiyo ni wajibu wake wa kimsingi. Alipokuwa mkuu wa wilaya ya Diqing, mbali na kufanya juhudi za kuboresha miundo mbinu ya Diqing, Bw. Gesangdunzhu pia alijitahidi kutafuta njia mpya ya kuendeleza wilaya hiyo. Siku moja ya mwezi Februali mwaka 1996, mwongozaji mmoja wa watalii aitwaye Sun Jong alimwonesha Bw. Gesangdunzhu kitabu cha Lost Horizon kilichoandikwa mwaka 1933 na mwandishi maarufu wa Marekani Bw. James Hilton. Bw. Gesangdunzhu alisema, "Bw. Sun Jong alinionesha kitabu kimoja na kuniambia kuwa, mandhari ya Diqing inafanana sana na Shangri-la iliyosimuliwa kwenye kitabu hicho, kuna uwezekano mkubwa kuwa Shangri-la ni sehemu fulani ya wilaya ya Diqing." Baada ya hapo, Bw. Gesangdunzhu alihimiza sana juhudi za kutafuta Shangri-la kwa hatua madhubuti. Mwezi Septemba mwaka 1997, serikali ya Yunnan ilitangaza kuwa Shangri-la iliyokuwa inatafutwa duniani kwa muda mrefu duniani iko kwenye wilaya ya Diqing, China. Mwaka huu watalii kutoka nchi mbalimbali kwenye wilaya ya Diqing waliongezeka na kufikia laki 5.4, na ni mara kumi zaidi kuliko watalii wa mwaka 1994. Baada ya kuzinduliwa kwa uwanja wa ndege wa Diqing, watalii wengi zaidi wanatembelea sehemu hiyo. Mwezi Desemba mwaka 2001 baraza la serikali la China liliidhinisha kubadilisha jina la mji mkuu wa wilaya ya Diqing kuwa Shangri-la. Mwaka 1998, Bw. Gesangdunzhu aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa kamati ya mambo ya makabila madogo madogo ya mkoa ya Yunnan. Alipofunga safari ya kwenda kufanya kazi mpya, wakazi wengi walimwaga, wakampa heshima ya Baba wa Shangri-la. Yunnan ni mkoa wenye makabila madogo madogo mengi zaidi nchini China, una makabila 25 madogo madogo, watu wa makabila hayo ni theluthi moja kati ya idadi yote ya watu wa mkoa huo. Akiwa mkurugenzi wa kamati ya mambo ya makabila madogo madogo ya Yunnan, Bw. Gesangdunzhu anaelewa vizuri hatua za serikali kuu ya China za kuwasaidia watu wa makabila madodo madogo. Alisema tangu mkutano mkuu wa 16 wa Chama cha Kikomunisti cha China ufanyike, serikali kuu inatilia maanani sana kazi za makabila madogo madogo, na imetekeleza sera na sheria mbalimbali kuhusu mambo ya makabila hayo. Kutokana na mchango mkubwa aliutoa kwa maendeleo ya sehemu za makabila madogo madogo, Bw. Gesangdunzhu alichaguliwa kuwa mjumbe wa mikutano mikuu ya 15, 16 na 17 ya Chama cha Kikomunisti cha China. alisema, "Rais Hu Jintao alitaja mambo ya makabila madogo madogo mara nne kwenye ripoti aliyotoa kwenye mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China. Nikiwa mjumbe kutoka kwenye makabila madogo madogo wa mkutano huo, nitaendelea na juhudi zangu kwa ajili ya kuimarisha umoja, ustawi na maendeleo ya makabila madogo madogo." Idhaa ya kiswahili 2007-11-14
|
|