Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-19 20:36:59    
Mtunzi mashuhuri wa muziki Guo Wenjing

cri

Bw. Guo Wenjing ni mtunzi mashuhuri wa muziki nchini China, gazeti la New York Times lilisema, "yeye ni mtunzi pekee wa muziki nchini China aliyepata heshima kubwa duniani ambaye hakuwahi kuishi kwa muda mrefukatika nchi za nje". Muziki wake unapigwa katika matamasha mengi ya kimataifa ya muziki.

Siku chache zilizopita opera aliyotunga ya "Mshairi Li Bai" ilioneshwa mjini Beijing baada ya kuoneshwa mara nyingi nchini Marekani. Opera ya "Mshairi Li Bai" ilitungwa kwa mujibu wa maisha ya mshairi huyo aliyeishi katika Enzi ya Tang miaka zaidi ya elfu moja iliyopita. Mshairi Li Bai aliandika mashairi mengi ambayo yanajulikana sana miongoni mwa Wachina. Katika opera hiyo kuna wahusika wanne tu, lakini kati ya wahusika hao mmoja tu ni mtu halisi na wengine ni "pombe", "mwezi" na "mashairi" wakiwakilisha sehemu ya maisha ya mshairi Li Bai. Bw. Guo Wenjing alipoeleza kuhusu opera hiyo alisema,

"Katika opera hiyo ya kuonesha maisha ya Li Bai, mwezi unawakilisha mwanamke, pombe inawakilisha marafiki, na mwanamke na marafiki wote ni watu ambao hawakosekani katika maisha ya mtu, na mashairi ni matokeo baada ya kupata yote hayo. Wazo la kutunga muziki huo ni la aina yake, Li Bai ni mtu pekee halisi na wahusika wengine watatu ni pombe, mwezi na mashairi ambavyo ni sehemu muhimu katika mashairi ya Li Bai, vikionesha hulka yake ya uadilifu. Katika mashairi ya Li Bai mwezi unazungumzwa mara nyingi."

Bw. Guo Wenjing alizaliwa mwaka 1956 mkoani Sichuan nchini China. Alipokuwa na umri wa miaka 18 kwa mara ya kwanza aliposikiliza "simfoni ya 11" ya Shostakovich, alikuwa anafurahi zaidi kuliko anaposikia muziki wote mwingine, tokea hapo aliamua kuwa mtunzi wa muziki. Mwaka 1978 alijiunga na Chuo Kikuu cha Muziki cha Beijing kwenye kozi ya utunzi wa muziki. Baada ya kusoma kwa miaka minne alipohitimu alisifiwa kuwa ni mmoja kati ya watu hodari wanne wa muziki katika chuo chake. Katika muda wa miaka 30 iliyofuata Bw. Guo Wenjing alipata mafanikio yasiyo ya kawaida katika utunzi wa muziki, muziki mwingi aliotunga ni pamoja na "Shajara ya Mwendawazimu", "Karamu ya Usiku", "Utalii wa Mbali", "Barabara Yenye Vilima na Mashimo Mkoani Sichuan", "Mazishi ya Majeneza Gengeni" na mwingine zaidi ya kumi. Muziki wa "Barabara Yenye Vilima na Mashimo Mkoani Sichuan" umechaguliwa kuwa ni "muziki ulio bora kabisa wa Kichina katika karne ya 20". Zaidi ya hayo, aliwahi kutunga muziki kwa ajili ya filamu ya "Masafa Marefu" iliyopigwa chini ya uongozaji wa Bw. Zhang Yimou, filamu ya "Katika Siku Zenye Mwangaza wa Jua" na filamu nyingine za televisheni zaidi ya 40. Lakini njia yake ya utunzi wa muziki haikuwa shwari. Alisema,

"Nimechagua maisha ya muziki, nilipokuwa mtoto nilipiga fidla, lakini mwishowe niliuza vitabu vyangu vyote vya muziki wa fidla kwa ajili ya kununua vitabu vya elimu ya utunzi wa muziki. Baada ya kuhitimu masomo ya chuo kikuu maisha yangu yalikuwa magumu sana, hata hivyo nia yangu haikuwahi kutikisika kutokana na upendo wangu mkubwa, shughuli zangu zote za muziki zinatokana na upendo, najipongeza kuwa kazi yangu pia ni furaha yangu."

Mwaka 1987 Bw. Guo Wenjing alitunga simfoni yenye nyimbo za kwaya kubwa kwa mujibu wa mashairi ya Li Bai. Huu ni muziki wenye kwaya na bendi kubwa. Muziki huo ulipopigwa kwa mara ya kwanza katika mwaka huo ulitingisha jamii ya wanamuziki na ulichaguliwa kuwa ni "muziki ulio bora kabisa wa Kichina katika karne ya 20".

Miaka karibu elfu mbili iliyopita mkoa wa Sichuan ulikuwa ni Dola la Shu nchini China, utamaduni wa kale ulikuwa na athari kwenye utunzi wa muziki wake, lakini hapendi muziki wa kale unaoeleza hisia za furaha au huzuni kutokana na mandhari ya maji na milima, bali anaona muziki ni lazima ufungamane na mustakabali wa taifa, hali ya maisha ya wananchi, ndio maana aliamua kutunga muziki wenye fikra pana.

Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita ambapo wanamuziki wengi walitumia kila njia kwenda nchi za Magharibi Bw. Guo Wenjing alibaki nchini akiwa anafundisha utunzi wa muziki katika Chuo Kikuu cha Muziki cha Beijing na huku akitunga muziki wake. Katika miaka ya karibuni maombi kutoka nchi za nje ya kumtaka atunge muziki yamekuwa mengi, lakini Bw. Guo Wenjing anashikilia tabia yake bila kufuata matakwa ya watu wengine. Alisema,

"Sijali kama muziki wangu unakidhi kigezo kinachotakiwa na serikali au umma wa China, wala sijali kama muziki wangu unalingana na kigezo kinachotakiwa na wanamuziki wa nchi za Magharibi, mimi naandika muziki ninaoupenda."