Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-19 20:41:45    
Kuangalia "vitu vitatu vya ajabu" kwenye kisiwa cha Junshan

cri

Ziwa la Dongting lililoko kwenye sehemu ya kati nchini China, ni ziwa lenye maji baridi linalochukua nafasi ya pili kwa ukubwa nchini China. Eneo la Ziwa hilo liko kwenye mikoa miwili ya Hubei na Hunan, umaalumu wa ziwa hilo ni kuwa linaungana na maziwa kadhaa madogo, na kuna milima katika maziwa. Katika kipindi hiki cha leo, tunawafahamisha kuhusu sehemu moja yenye mandhari nzuri ya kisiwa cha Junshan kilichopo kwenye ziwa la Dongting.

Kisiwa cha Junshan ni kisiwa kidogo kilichoko kwenye ziwa la Dongting lenye eneo la kilomita 400, kisiwa hicho kiko katika mji wa Yueyang, mkoani Hunan, kinatazamana na jengo maarufu la Yueyang kwa mbali, eneo la kisiwa hicho ni chini ya kilomita moja ya mraba, na ni sehemu yenye mandhari nzuri ya ngazi ya taifa nchini China. Wenyeji wa huko wanakiita kuwa ni kisiwa cha mapenzi, watalii kutoka nchi za nje waliotembelea huko, wanapenda kukiita kisiwa hicho kuwa ni Eden ya mashariki.

Katika kisiwa cha Junshan kuna aina tatu za vitu vya ajabu, ambavyo ni mianzi inayoweza kutokwa machozi, chai inayoweza kucheza ngoma na kobe wa kipekee wa rangi ya dhahabu.

Kabla ya miaka zaidi ya 4,000 iliyopita, mabinti wawili wa mfalme Yao wa china ya kale, waliolewa na mfalme Shun, hapo baadaye mfalme Shun alifariki wakati akifanya ziara ya ukaguzi kwenye sehemu ya kusini. Wake hao wawili wa mfalme Shun walimtafuta mume wao hadi kwenye kisiwa cha Junshan, walipopata habari kuwa mfalme Shun alishafariki, walikumbatia mianzi na walilia kwa siku tatu kutwa kucha, halafu walijitumbukiza majini, machozi yao yaliyodondoka kwenye mianzi, yalibaki na kuwa madoa yasiyofutika.

Hadi sasa bado kuna makaburi mawili ya wake hao wawili wa mfalme Shun kwenye kisiwa cha Junshan. Hivyo kisiwa cha Junshan kiliitwa na watu kuwa "kisiwa cha mapenzi". Mtalii kutoka mkoa wa Heilongjiang dada Chen Yufen alisema, yeye na rafiki yake walifahamiana kwenye kisiwa cha Junshan, alisema, walisaidiwa na mazingira ya mapenzi ya kisiwa cha Junshan.

"Hii ni safari yetu ya pili kufika hapa, juzi ilikuwa siku ya kutimiza miaka mitatu tangu sisi wawili kuwa wachumba. Tungefika hapa juzi, lakini tulikosa tikiti za ndege, hivyo tumefika leo. Mimi na mchumba wangu tulifahamiana katika mashua kwenye kisiwa cha mapenzi, tulibadilishana namba za simu zetu, tulidumisha mawasiliano, huenda tumesaidiwa na mazingira ya kisiwa cha mapenzi, tumekuwa marafiki kwa miaka kadhaa, tunapendana sana, naona hiyo ni bahati yetu."

Licha ya 'mianzi inayotokwa machozi", kwenye kisiwa cha Junshan kuna aina ya "chai inayoweza kucheza ngoma". Toka zamani za kale, michai iliota kwenye kisiwa cha Junshan, huko kuna aina maarufu ya chai inayoitwa "sindano za fedha za Junshan". Chai ya aina hiyo ni ya rangi ya manjano kama ya dhahabu, lakini ncha zake zina rangi nyeupe, hivyo chai hiyo inaitwa "jade iliyotiwa kwenye majani ya dhahabu". Ni tofauti na majani ya chai nyingine, majani ya chai ya aina hiyo, yanasimama wima yakitiwa maji moto katika kikombe, yanaonekana kama yanacheza ngoma, hivyo yanaitwa kuwa "chai inayoweza kucheza ngoma". Chai ya aina hiyo ni moja ya aina kumi maarufu za chai nchini China, na pia ni moja ya aina za chai zinazouzwa kwa bei kubwa kabisa. Katika zamani za kale, chai ya aina hiyo ilitumiwa na wafalme, hata mfalme aliweza kupata kilo 9 hivi kwa mwaka kutokana na uhaba wa chai ya aina hiyo.

Kitu cha aina ya tatu cha ajabu kilichoko kwenye kisiwa cha Junshan ni "kobe wa dhahabu", ambao wanapatikana huko tu. Pembezoni mwa mgongo wa kobe wa aina hiyo ni wa rangi ya manjano, hivyo kobe wa aina hiyo wanaitwa "kobe wa dhahabu", watu wanasema kobe hao wanaleta baraka kwa watu. Watu waliofika kwenye kisiwa cha Junshan huambiwa kuwa wakipapasa mgongo wa kobe hao wataishi umri wa miaka mia moja, wakipapasa kichwa cha kobe, hawatakuwa na shida katika maisha yao yote.

Mbali na vitu vitatu visivyo vya kawaida, kwenye kisiwa hicho kuna vitoweo maarufu vinavyopendwa pia na watalii. Kwa mfano kuna misemo iliyokuweko toka zamani kuwa "mtu aliyekwenda kwenye kisiwa cha Junshan bila kula samaki, atasikitika katika maisha yake yote", "karamu haiwi karamu bila kuwa na samaki". Katika karamu rasmi, lazima kuwe na asusa ya samaki, kitoweo rasmi cha samaki, mpaka hapo baadaye, vitoweo vyote vya mezani ni vyenye samaki vikijulikana kuwa ni "vitoweo vya samaki vilivyokamilika vya Balin".

"Vitoweo vya samaki vilivyokamilika vya Balin" ni vitoweo zaidi ya 20 vilivyopikwa kwa mapishi ya aina mbalimbali yakiwemo ya kukaangwa, kupikwa kwa mvuke, kukaangwa kwa mafuta mengi, kukaangwa kwanza kabla ya kuchemshwa, n.k. Kwa hiyo, wageni baada ya kufika kisiwa cha Junshan, wasiwe na wasiwasi juu ya mazoea yake kuhusu chakula na malazi, kwani huko kuna hoteli za aina mbalimbali zenye huduma nzuri na vyakula vya kila aina, mgeni atajisikia kama yuko nyumbani kwake. Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Jenny Simone ya Marekani Bibi Simone, ambaye wakati huo alikuwa akitalii kwenye kisiwa cha Junshan, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa amezoea kabisa maisha ya huko, alisema,

"Ninaona raha kubwa kwenye hoteli niliyofikia. Upangaji wa vyumba vya hotelini na vitu vya ndani pamoja na mapambo yaliyowekwa ndani ya vyumba vya hoteli, unavutia sana kufurahisha. Wakati wa chakula, ninapenda sana kuchagua chakula cha huko. Siku ya kwanza tulipofika, nilipata chakula nilichokipenda sana, malazi yalikuwa mazuri na nimeona mambo mengi ya kiutamaduni."

Kuna sehemu nyingi zenye mandhari nzuri na mabaki ya zamani ya kiutamaduni kwenye kisiwa cha Junshan, katika mlima wa huko kuna visiwa vitano, majengo manne, vibanda 36 na mahekalu 48. Kila mabaki ya kale yana historia ndefu, na kila hadithi iliyotokea zamani inafurahisha. Ofisa mmoja wa sehemu yenye mandhari nzuri kisiwani, Bw. Zeng alituambia huko ni mahali pa kutimiza mambo yaliyootwa ndotoni, alisema ni matarajio yake kuwa wageni wengi zaidi watafika kwenye kisiwa cha mapenzi. Alisema,

"ninawakaribisha vijana kutoka nchi mbalimbali, watu wa makamo na wazee, watoe maombi ya mambo wanayopenda, ninawatakia watu wanaopendana waweze kufanikisha mapenzi yao na kufunga ndoa. Kwa niaba ya wakazi wote wa kisiwa cha mapenzi cha Junshan nawakaribisha."