Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-22 13:00:26    
Je, Wachina wana burudani gani baada ye kazi?

cri

Miaka zaidi ya 20 iliyopita, wakati ambapo watu wa China walikuwa wanajitahidi kujikimu katika maisha, burudani katika jamii ya China zilikuwa chache. Wakati huo watu wengi wakimaliza kazi, walikuwa wanakaa nyumbani kusoma vitabu au kusikiliza vipindi vya radio, na marafiki walikuwa wanakaa pamoja na kucheza karata na chesi tu.

Baada ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, maendeleo ya kasi ya uchumi yamekuwa yakiinua kiwango cha maisha ya wananchi na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii ya China. Burudani za aina mbalimbali zilianza kuingia na kuchukua nafasi muhimu kwenye maisha ya watu wa China, ambapo watu wengi walijiwekea malengo mapya kutokana na burudani na kujitambua kuwa wao wana uwezo mkubwa zaidi.

Bw. Lu Tongzhou mwenye umri wa miaka 33 anafanya kazi kwenye jarida moja. Alipokuwa mwanafunzi wa shule ya msingi, alikuwa anasafiri mara kwa mara na wazazi wake ili apate ufahamu wa mambo mengi mapya na ya ajabu. Katika miaka 20 iliyopita, kijana huyo amekuwa akishuhudia mabadiliko katika sekta ya utalii. Alisema  "Zamani hali ya kiuchumi ilikuwa duni. Kwa mfano nilipokuwa nasoma, kulikuwa hakuna barabara za kasi, wala sikuwa na hela za kulipia nauli ya ndege. Hata nikisafiri kwa reli, nilinunua tiketi za kukaa tu badala ya tiketi za kulala. Baada ya sera ya mageuzi na kufungua mlango ianze kutekelezwa, hivi sasa hakuna matatizo katika mawasiliano, zaidi ya hayo watu wamebadilisha mtizamo kuhusu utalii. Hivi sasa watu wanapendelea kujichagulia shughuli za utalii na kufanya utalii wenye umaalumu."

Watu wengi wa China wanakubaliana na anayozungumza kijana huyo kuhusu mabadiliko. Zamani katika jamii ya China, utalii ulitafsiriwa kuwa shughuli za kutembelea milima na mito na kuburudishwa kwa mandhari nzuri tu. Lakini hivi sasa utalii unahusu mambo mengi zaidi. Kwa mfano kijana Lu Tongzhou, anavutiwa na michezo ambayo kwa Kiingereza inaitwa "extreme sports", yaani kupanda milima, kuvuka sehemu yenye hali ngumu ya maumbile isiyo na binadamu, kupanda milima ya barafu na kutembea kwa miguu kwa muda mrefu. Kwa maoni ya watu wengine, hizi zinaonekana ni shughuli za kujitesa, lakini kijana Lu anafurahia michezo hiyo.

Alisema  "Nilianza kushiriki kwenye michezo hiyo mwaka 2002. Hadi sasa nimepanda hadi vilele vya milima mitano, kati ya milima hiyo, mitatu ina urefu wa zaidi ya mita elfu 6 na mmoja una urefu wa mita elfu 5. Tarehe 9 Julai mwaka huu, nilifanikiwa kupanda kilele cha Mlima Mushitage, mkoani Xinjiang, China, ambacho kinajulikana kama baba wa vilele vya barafu, kina urefu wa kilomita 7,546. Nimepanda kwenye kilele cha juu namna hii, inamaanisha kuwa nina kiwango kinacholingana na mchezaji wa ngazi ya kwanza ya taifa."

Michezo hiyo pia ilibadilisha mtizamo wa kijana huyo kuhusu utalii. Miaka minne iliyopita kijana Lu alipofanya matembezi kwa miguu, alifika kwenye sehemu ya milimani yenye watu maskini mkoani Sichuan, kusini magharibi mwa China. Baada ya kushuhudia jinsi wakazi wa huko wanavyosumbuliwa na hali duni ya kimaendeleo, alianzisha shughuli za kuchagisha fedha kwa ajili ya shule za huko kwa kupitia mtandao wa Internet. Wito wa kuchangisha fedha uliitikiwa na watu wengi nchini China, na fedha hizo zilitumika katika manunuzi ya vitabu kwa ajili ya shule hizo. Kuanzia hapo kijana Lu Tongzhou na mashabiki wengine wa utalii walianza kutembelea sehemu zenye hali duni mara kwa mara, wakiambatanisha utalii na shughuli za ufadhili. Mbali na hayo kijana huyo anatoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa kupitia tovuti yake ya utalii kwenye mtandao wa internet. Kuhusu mambo hayo kijana Lu Tongzhou alisema burudani hizo zina umuhimu kwake ambazo zinamsaidia aoneshe umuhimu wake kwa jamii.

Alisema  "Kutokana na kufanya utalii na shughuli za uhifadhi wa mazingira, naona kiwango changu cha maadili kimeinuka. Labda ni vigumu kugeuza tabia ya mtu, lakini angalau inasaidia kuinua kiwango cha maadili."

Tofauti na kijana Lu Tongzhou, Bi. Wang Qiqi anayefanya kazi katika kiwanda kikubwa cha serikali, anatumia muda wa mapumziko kuwa darasani. Dada huyo mwenye umri wa miaka 26 ni mtulivu. Aliwahi kusoma kwenye chuo kikuu kimoja cha lugha za kigeni, na mwezi mmoja uliopita, alijiandikisha kwenye somo la lugha ya Kifaransa wakati wa mwisho wa wiki. Miongoni mwa wenzake darasani, kuna wanafunzi wa shuleni, pia kuna watu wa makamo wenye umri mkubwa zaidi kuliko yeye, lakini wote wanajifunza kwa makini.

Bi. Wang Qiqi alisema jamii ya sasa ni jamii inayotetea moyo wa kujifunza, kwa hiyo kusoma mambo mengine wakati wa mapumziko ni jambo la maana.

Alisema  "Siku nyingine ninazungumza na wenzangu wa chuoni, marafiki na wafanyakazi wenzangu, nagundua wengine pia wanashiriki kwenye masomo kadha wa kadha baada ya kazi. Nimeamua baada ya kumalizika kwa somo la lugha ya Kifaransa, nitaendelea kusoma elimu ya bajeti ya miradi ya ujenzi. Kuwa kijana kunamaanisha kuwa, una muda mwingi binafsi, ukiutumia kwa ufanisi utanufaika katika maisha yako ya baadaye."

Burudani safi za aina mbalimbali si kama tu zinasaidia kupunguza shinikizo kubwa linalotokana na maendeleo ya kasi ya uchumi kwa watu wa China, bali pia zinawaletea furaha kubwa.

Idhaa ya kiswahili 2007-11-22