Wachina wa leo wanauchukuliaje utamaduni wao wa jadi?
Ilikuwa saa tano za usiku, muda mfupi baada ya wageni wa Bw. Xiao kuondoka na watu wa familia yake wakiwa tayari kulala baada ya kupanga panga nyumba, lakini wakati huo Bw. Xiao aliwasha televisheni bila kujali akihimizwa na jamaa zake "lala basi!"
Kila usiku wakati kama huo Bw. Xiao huwasha televisheni kutazama kipindi cha "darasa la mihadhara". Katika kipindi hiki maprofesa wanaeleza historia au utamaduni wa kale wa China. Bw. Xiao amekuwa akitazama kipindi hiki kwa zaidi ya nusu mwaka sasa. Siku hizi anavutiwa na mihadhara ya Profesa Yu Dan kuhusu kitabu cha "Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius", ambaye ni mwanafikra, mwanafalsafa na mwalimu mkubwa katika China ya kale.
"Kitabu cha 'Maneno Yaliyochaguliwa ya Confucius' kinatufundisha namna ya kuishi kimaadili, wawe wanadamu wa namna gani katika maingiliano na watu na kutenda mambo."
Hii ni sauti ya Profesa Yu Dan katika kipindi cha TV cha "darasa la mihadhara" .
Kutokana na umaskini Bw. Xiao aliweza kupata elimu ya msingi tu, lakini kipindi cha mihadhara inayotolewa na maprofesa kinamvutia sana, sababu ni kwamba wahadhiri wanafundisha elimu ya juu na kuwaelimisha raia wa kawaida utamaduni mkubwa wa jadi wa China kwa lugha nyepesi sana. Bw. Xiao alisema,
"Nasikiliza mihadhara yao kama ninavyosikiliza masimulizi ya hadithi, inanifahamisha historia yetu ambayo ni msingi wa taifa letu."
Mtoto wa Xiao anafanya kazi katika kampuni moja kubwa ya kompyuta mjini Beijing. Mwanzoni hakuelewa kwa nini baba yake anatazama sana kipindi hiki. Alisema,
"Baba yangu amekuwa mzee, kama anachelewa sana kulala si vizuri kwa afya yake, tena mambo yanayoelezwa ni ya zama za kale, hayana maana kubwa kwa leo."
Ingawa mtoto wake anasema hivyo, lakini alimnunulia baba yake diski ya mihadhara ya kipindi hicho katika duka la vitabu ili baba yake aweze kutazama na kusikiliza wakati wowote anapotaka, pamoja na diski hiyo naye pia alijinunulia kitabu kimoja kilichoandikwa na Profesa Yu Dan.
Bi. Yu Dan ni Profesa wa Chuo Kikuu cha Ualimu cha Beijing, anajulikana ndani na nje ya China kutokana na mihadhara yake katika televisheni. Kabla ya hapo Xiao Wenpeng hakuwahi kusoma kitabu cha "Maneno Yaliyoteuliwa ya Confucius". Alisema,
"Nataka kujua ni nini kinachovutia."
Lakini alipoanza tu kusoma mara alivutiwa na kitabu cha Yu Dan, na maelezo ya kina kuhusu maneno yaliyochaguliwa ya Confucius yanaambatana na maisha ya leo, Hata Xiao Wenping anaweza kutumia maneno ya Yu Dan kueleza matatizo yanayotokana na kazi yake. Alisema,
"Kinachosumbua zaidi ni kurudia rudia makosa, kwa sababu kosa angalau dogo linaweza kusababisha kazi ya siku nyingi kuwa bure. Baada ya kusoma 'maneno yaliyochaguliwa ya Confucius' nimefahamu kwamba kumbe Confucius alituambia hayo hata kabla ya miaka elfu mbili iliyopita."
Katika siku aliposoma kitabu hicho, Xiao Wenpeng alifahamu kuwa wenzake wengi wamewahi kusoma vitabu vingi vya kale vya China na vile vile wanaangalia kipindi cha "darasa la mihadhara". Kuwa na hamu ya kuelewa utamaduni wa kale wa China kumekuwa mtindo mpya wa kimaisha katika jamii ya leo nchini China. Bibi Chi Changyan ni mfanyakazi mwenzake XiaoWenpeng, yeye anapenda sana kusoma vitabu vya kale vya China. Alisema,
"Kutokana na kazi yangu, nawasiliana na watu wengi hata watu wa nchi za nje. Vitabu vya kale vya utamaduni wa China vimekuwa na athari kwangu kwa namna ya kuwasiliana na watu na kutenda mambo."
Utamaduni wa jadi wa China licha ya kuwa na athari katika maingiliano na watu pia umekuwa na athari kwa maisha ya familia yake, na hasa katika kulea watoto. Binti yake alianza kujifunza upigaji piano alipokuwa na umri wa miaka minne, na kabla ya hapo alipokuwa na uwezo wa kutamka Bibi Chi alianza kumfundisha kitabu cha "Maneno Matatu Matatu".
"'Maneno matatu matatu' ni kitabu cha kufundisha watoto utamaduni wa jadi wa China, kinahusiana na historia, unajimu, jiografia, maadili na masimulizi miongoni mwa watu. Kitabu hicho kimeandikwa kwa maneno matatu kila sentensi, ni rahisi kwa watoto kukumbuka, kitabu hiki kimeorodheshwa na UNESCO katika "vitabu vya mafunzo ya maadili kwa watoto duniani". Nia ya Bibi Chi kumfundisha binti yake mdogo kitabu hicho ni kumwekea msingi wa utamaduni wa jadi wa China ambao atanufaika nao katika maisha yake yote. Alisema,
"Sitaki mtoto wangu asahau johari walizotuachia wahenga wetu, asiwe kufahamu tu A B C D au elimu kwa ajili ya kufaulu mtihani tu."
Bw. Xiao na mtoto wake, Bi. Chi na binti yake, kila siku hawakosi kujifunza utamaduni wa jadi wa China. Hivi leo utamaduni huo umekuwa ukirudia tena maishani mwa Wachina. Nakala milioni 4 za kitabu cha mihadhara ya Yu Dan kuhusu "Maneno Yaliyochaguliwa ya Confucius" zimeuzwa nchini China na pia kinanunuliwa sana katika nchi za Japan, Korea ya Kusini na Malaysia.
Gazeti kubwa la China Ren Min Ri Bao liliwahi kuchapisha makala kwa siku saba mfululizo kuhusu hali ya utazamaji wa mihadhara ya Yu Dan. Lilisema tokea China ianze mageuzi, uchumi unastawi kwa kasi na watu wengi wanakuwa matajiri, wameanza kujijenga kwa kununua nyumba, magari na kujistarehesha kwa pesa nyingi, ustawi wa uchumi na starehe ya maisha haviwezi kukidhi matakwa yao ya moyo, upungufu huo wa utamaduni wa jadi utasababisha jamii kukosa masikilizano. Sasa Wachina wamegundua thamani ya utamaduni wao wa jadi na wameanza kunyonya virutubisho vya utamaduni wa kale wa China.
Idhaa ya kiswahili 2007-11-26
|