Kwenye sehemu kati ya mkoa wa Yunnan na mkoa unaojiendesha wa kabila la Wazhuang wa Guanxi, iliyoko sehemu ya kusini magharibi ya China, kuna mlima wenye theluji wa Meili, ambao unaheshimiwa na watu wa kabila la Watibet kuwa ni mungu wao, na watu wa kabila hilo wanakwenda kuhiji kwenye mlima huo mwaka hadi mwaka. Mlima wa Meili una vilele 13 vyenye mwinuko wa zaidi ya mita 6,000 kutoka usawa wa bahari, na kilele chake kikuu kina urefu wa zaidi ya mita 6,700, ambacho hadi hivi sasa bado hakuna mtu aliyewahi kufika juu.
Ukisafiri kutoka wilaya ya Shangri-La, mji mkuu wa wilaya ya Diqing, gari linapita kwenye milima, kwenye kando mbili za barabara kuna milima mirefu na mawingu yaliyofunika milima. Mara kwa mara gari linasafiri katika mawingu, hata milima mikubwa inakuwa imefunikwa na mawingu. Watalii wanaokwenda kuangalia mlima wenye theluji, wanaweza kuona mandhari nyingi nzuri njiani ikiwa ni pamoja na mazao ya kilimo yaliyoko kwenye mabonde, misitu na majani yaliyopo kwenye uwanda wa juu. Tulipopumzika njiani, mwandishi wetu wa habari aliongea na dereva wa huko Bw. Yuan Liuwen, ambaye amefanya kazi ya dereva kwa zaidi ya miaka 20, alisema,
"Watalii wanaotoka sehemu hii, hasa wanakwenda kuangalia mlima wa Meili. Barabara hii inatoka mkoa wa Yunnan kwenda mkoa wa Tibet, kabla ya katikati ya mwezi ujao, watu wanaweza kuingia mlimani, lakini baada ya hapo watu hawawezi tena kwenda huko, kwani barabara inakuwa na theluji na barafu."
Mwishoni mwa mwezi Septemba, hali ya hewa ya sehemu hiyo bado inakuwa ni masika, ambapo mara kwa mara watu hawawezi kuona mlima vizuri. Mlima wenye theluji wa Meili ni Mungu wa milima machoni pa watu wa kabila la watibet, hivyo kila mwaka kuna watu wengi wanaokwenda kuhiji kwenye mlima huo. Baada ya kusikiliza maelezo ya mwongoza watalii Bi. Dawazhuoma wa kabila la watibet, mwandishi wa habari alikuwa na shauku kubwa zaidi ya kuuona mlima wa Meili.
"Kwa kalenda ya kabila la Watibet, mwaka 2003 ni mwaka wa Mungu wa Kawagebo, watibet wanaamini kuwa wakienda kuhiji kwenye mlima wa Meili mwaka huo, ni sawa na kuwahiji miungu wote walioko kwenye sehemu ya Tibet. Kwa hiyo katika mwaka 2003, watibet wanaoishi kwenye sehemu mbalimbali za mikoa ya Tibet na Qinghai, walifika hapa kuhiji mlima wa Meili."
Mnamo saa 12 hivi ya siku ya pili, gari la waandishi wa habari lilifika kwenye hekalu la Feilai. Ingawa kulikuwa bado hakujapambazuka, lakini huko kulikuwa na kundi kubwa la watu, wakiwemo watalii na watibet wanaoishi kwenye vijiji vya karibu. Ukitazama kutoka mbali, kilele cha mlima chenye theluji, kinajitokeza kwenye mawingu na kinaonekana kama kiko mbinguni, hali hiyo inazidisha heshima kubwa kuhusu mlima wa Meili. Watalii wanaweza kuomba Mungu awabariki kama wanavyofanya watu wa kabila la watibet, kuchoma udi na kutundika vitambaa virefu vilivyoandikwa maneno yaliyopo kwenye msahafu wa dini ya kibudha ya kitibet. Mtalii kutoka mji wa Guangzhou, sehemu ya kusini ya China, Bi. Zhong Ning alimaliza kutundika vitambaa hivyo vya kidini, akiwa pamoja na marafiki zake waliokuwa wanasubiri kutokea kwa mlima wa Meili.
"Nimekuja pamoja na hawa marafiki zangu, tunataka kuangalia mlima wenye theluji na kutalii kwenye sehemu hiyo. Tulilala hapa jana usiku, tuliambiwa kuwa ni vigumu kuona hali ya hewa nzuri kama ya sasa, ninafurahi sana leo hakuna mvua."
Baada ya kupambazuka zaidi, na baada ya mawingu yaliyokuwa yameufunika mlima Meili kuanza kutoweka polepole, kilele kikuu cha mlima chenye theluji mara kilionekana machoni pa watu, na mara kikafunikwa tena na mawingi, lakini baada ya muda kilele cha mlima kilifunikwa kabisa na mawingu. Mkazi mmoja wa kitibet alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kile ndio kilele kikuu cha mlima Meili, na kinaitwa Kawagebo.
Mwandishi wa habari aliuliza, "katika hali ya hewa ya hivi sasa, tunaweza kuona mlima wenye theluji?"
Mtibet alijibu, "katika hali ya hewa ya hivi sasa, huenda utaweza kuuona mlima."
Mwandishi wa habari alisema, "mwanzoni tuliona kilele kidogo, lakini sasa hivi kimefunikwa na mawingu."
Mtibet alisema, "sawa, kile kilichoonekana ndicho kilele cha Kawagebo."
Hauchi hauchi kumbe umekucha! Mwangaza wa jua ulipita katika mawingu na kuangazia sehemu ile, mawingu mengi yalisogea kwa upande mmoja, kidogo kidogo mlima ulianza kuonekana vizuri. Vilele vya mlima vinaonekana kwenye mbingu, kilele chenye theluji kilikuwa na rangi ya dhahabu chini ya mwangaza wa jua. Theluji iliyoko kwenye vilele vya mlima iliang'ara sana chini ya mwangaza wa jua na kuumiza macho ya watu. Bibi Hu Dongmei kutoka mkoa wa Sichuan, alitembelea huko miaka 6 iliyopita, alivutiwa na mandhari nzuri ya mlima, na aliamua kuanzisha nyumba ya wageni na kuishi huko, alifikiri kwa upande mmoja kuwa anaweza kupata watalii, na kwa upande mwingine anaweza kuburudishwa na mandhari ya mlima wenye theluji. Alisema,
"Ninaona hapa ni pazuri sana, mimi sitaki kurejea Sichuan. Wanakijiji wa hapa ni wema sana, wao ni wakarimu kabisa. Hebu angalia, mandhari ya hapa ni ya kupendeza sana, tena hapa ni penye usalama kabisa, magari yakiegeshwa hapa hakuna wasiwasi, hata hakuna mtu anayelinda wakati wa usiku."
Hekalu la Feilai ni kituo cha kwanza cha kuangalia mlima wa Meili, endapo mtu akitaka kuangalia mlima wenye theluji kwa karibu zaidi, basi anatakiwa kupanda gari hadi chini ya mlima. Jambo lililomsikitisha mwandishi wetu wa habari ni kuwa alilazimika kuondoka kwa kukosa nafasi, isipokuwa aliwakuta baadhi ya watalii waliotoka Beijing, ambao wakati ule walikuwa wakitoka mlimani, dada Xu Meng aliwaambia,
"jana tulilala hapa ili tuweze kuuona mlima wa Meili, lakini tulishindwa, hivyo tuliamua kuingia mlimani. Baada ya kufika kwenye kijiji cha Yubeng, tulisikia kuwa kule kuna milima miwili yenye theluji, na tuliiona. Lakini ni shida sana kuweza kuuona mlima wa Kawagebo. Kawagebo ni mlima wa mungu kwa watu wa kabila la watibet, watibet wanaamini kuwa ni wale wenye uhusiano na dini ya kibudha, wanaweza kuuona, endapo mkipata nafasi ya kwenda huko, msikose kuuona mlima huo wa mungu, ambao ni mzuri ajabu."
Idhaa ya kiswahili 2007-11-26
|