Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-27 15:46:05    
Chemsha bongo "Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki" 3

cri
Viwanja na majumba ya michezo vya Michezo ya Olimpiki ya Beijing

Wasikilizaji wapendwa, ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua, leo tunawaletea makala ya tatu ya mashindano ya Chemsha bongo yasemayo: "Tukutane Beijing mwaka 2008 kwenye Michezo ya Olimpiki", ambapo tutawajulisha hali ya ujenzi wa viwanja na majumba ya michezo vitakavyotumika kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing.

Mashindano kwenye Michezo ya Olimpiki ya Beijing yanatakiwa kufanyika kwenye viwanja na majumba ya michezo 37 kwa jumla, mjini Beijing kumejengwa viwanja vipya na majumba mapya ya michezo yapatavyo 19, viwanja vingine 11 vimekarabatiwa, na 7 ni vya muda, gharama za jumla za ujenzi na ukarabati wa viwanja na majumba hayo ya michezo zinakadiriwa kufikia dola za kimarekani bilioni 2.67. Serikali kuu ya China na serikali ya mji wa Beijing zinatilia maanani sana ujenzi wa viwanja na majumba hayo ya michezo, na kuwashirikisha wasanifu na wajenzi wa kiwango cha juu wa nchini na nje katika kusanifu na kujenga viwanja na majumba hayo ya michezo. Majengo yamesanifiwa kwa mitindo mipya na mipangilio mwafaka, ambayo yanaonesha kiwango cha juu cha kisayansi na kiteknolojia na thamani kubwa ya elimu kuhusu ubora. Kwa mfano, Uwanja wa michezo wa taifa wenye umbo kama kiota, na Jumba la mchezo wa kuogelea la taifa, usanifu wake umesifiwa na watu wengi, majengo hayo yanatazamiwa kuwa majengo murua katika historia ya ujenzi wa viwanja na majumba ya michezo ya Olimpiki.

Uwanja wa michezo wa taifa ambapo sherehe za ufunguzi na ufungaji wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 zitafanyika, kutokana na umbo lake lililo kama kiota, hivi sasa unaitwa mara kwa mara kuwa kiota. "Kiota" hiki kinajengwa kuanzia mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2003 ndani ya Bustani ya Olimpiki iliyoko kaskazini mwa mji wa Beijing. Hivi sasa kwa ujumla, ujenzi wa umbo la nje la "kiota" umekamilika kimsingi, naibu mhandisi mkuu anayewajibika na ujenzi wa jengo hilo Bw. Li Jiulin alisema, siku zijazo wajenzi watafanya kazi ya kujenga "vazi" la nje kwa jengo hilo lililojengwa kwa mihimili ya chuma na chuma cha pua, vifaa vya "vazi" hilo vinafanana na kioo au plastiki, ambalo linaweza kupitisha mwanga na hewa, pia linaweza kuzuia mvua na mavumbi. Kutumia vifaa hivyo vya aina mpya bado ni nadra kuonekana duniani, hivi sasa kati ya majengo yaliyojengwa duniani, vifaa hivyo vya aina mpya vilitumiwa tu wakati wa kujenga uwanja mkubwa wa kombe la dunia la mpira wa miguu wa Munich, Ujerumani.

Kutumia teknolojia nyingi mpya, vifaa vipya na zana mpya pamoja na mpangilio mpya ni umaalum mkubwa katika ujenzi wa "kiota" hiki. Mhandisi Li alisema: "Wakati wa kujenga Uwanja wa michezo wa taifa yaani "kiota", usanifu wa jengo ni maalum zaidi, tulitumia teknolojia nyingi mpya kama vile kujenga umbo la jengo kwa mihimili ya chuma na chuma cha pua, na kutumia vifaa vinavyofanana na kioo na plastiki kujenga "vazi" la jengo, wakati wa kufanya hivyo tulikumbana na taabu kadha wa kadha za teknolojia za ujenzi wa jengo, kwani hatuwezi kuiga ufundi uliotumiwa katika ujenzi wa majengo yaliyojengwa zamani; aidha, usanifu maalum umepindukia kiasi cha utaratibu wa sasa, hivyo tulishindwa mara kwa mara kupata tegemeo la utaratibu wakati wa kusanifu, kujenga, kupima na kuthibitisha sifa ya ujenzi".

Ndiyo maana, mchakato wa kujenga Uwanja wa michezo wa Taifa yaani "kiota" kikubwa, ndiyo mchakato wa kutatua matatizo moja baada ya nyingine. Wajenzi wa jengo hilo walifanya utafiti wa kisayansi na kiteknolojia katika kufanya usanifu maalum na uvumbuzi kuhusu miradi mbalimbali na kutatua matatizo yote. Tuna imani kuwa, baada ya kufunguliwa kwa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 mjini Beijing, hakika "kiota" hiki kitawavutia watu wengi duniani, na kuwa jengo lingine la alama ya mji wa Beijing.

Kutokana na mpango wa usanifu, ujenzi wa Uwanja wa michezo wa taifa umezingatia ipasavyo uwezo wa matumizi ya uwanja huo kwa ajili ya michezo ya riadha, shughuli za utamaduni na biashara, maonesho na mikutano, shughuli za utalii, mazoezi ya kujenga mwili na burudani, pamoja na hali ya uwanja huo ya kuunganishwa na barabara, njia ya mawasiliano ya habari na zana za usalama, ili kuweka nafasi kubwa kadiri iwezekanavyo kwa ajili ya shughuli za kibiashara za siku za baadaye, na kuweka mazingira yanayosaidia kuufanya uwanja huo wa michezo ya Olimpiki uweze kuleta manufaa kwa jamii na faida za kiuchumi.

Baada ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, Uwanja wa michezo wa taifa utakuwa uwanja mkuu wa Klabu ya mchezo wa soka ya Guoan ya Beijing, pia utakuwa kituo cha shughuli za biashara, mazoezi ya kujenga mwili na burudani. Naibu meneja mkuu wa Kampuni ya Uwanja wa michezo wa taifa Bw. Zhang Hengli alisema: Baada ya kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, tutafanya mipango mfululizo ya kujenga zana na majengo mbalimbali kwa ajili ya shughuli za kibiashara siku za baadaye.

Jumba kuu la mchezo wa kuogelea lililopewa jina lingine na watu kuwa ni "ujazo wa maji" liko kwenye sehemu iliyo karibu na Uwanja wa michezo wa taifa, wakati wa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, michezo ya kuogelea na kupiga mbizi na mchezo wa mpira kwenye maji itafanyika kwenye jumba hilo, jumba hilo lilijengwa kutokana na michango iliyotolewa na ndugu wa Hongkong, Makau, Taiwan na wachina wanaoishi katika nchi mbalimbali duniani, hili ni jumba pekee lililokubaliwa na Kamati ya maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing kwamba ujenzi wake ulitumia michango pekee iliyopokelewa na kamati hiyo, umbo la nje la jumba hilo lenye rangi ya buluu yenye hali ya kustaajabisha linawavitia sana watu macho.

Mwanzoni mwa kusanifu Jumba kuu la mchezo wa kuogelea, wasanifu walitaka kusanifu umbo lake nje kutokana na uwezo wake, hatimaye wazo kuhusu maji limeonesha kiajabu miundo ya chembechembe za maji yaani mapovu ya maji, miundo hiyo ikawa mfumo wa miundo ya ujenzi wa jumba hilo.

Aidha wazo kuhusu kuandaa Michezo ya Olimpiki bila uchafuzi kwa mazingira na kuandaa michezo hiyo kwa njia ya kisayansi na kiteknolojia, pia limeonekana kwenye ujenzi wa viwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing. Kwa mfano, Uwanja wa Qingdao wa mchezo wa mashua zenye matanga wa Michezo ya Olimpiki uko kwenye kando la ghuba ya Fushan kwenye eneo jipya la mji wa Qingdao, mashariki mwa China, eneo la uwanja huo ni hekta 45. Ukitembea kwenye uwanja huo unaweza kugundua kuwa wazo la kuandaa Michezo ya Olimpiki bila uchafuzi linaonekana kwenye kila kitu cha ujenzi wa uwanja huo.

Mkurugenzi wa Idara ya uhandisi na uhifadhi wa mazingira katika Kamati ya maandalizi ya mchezo wa mashua zenye matanga ya Qingdao Bw. Li Zhipeng alijulisha kuwa, sayansi na teknolojia za uhifadhi wa mazingira zinatumiwa vilivyo katika ujenzi wa uwanja huo, hasa ni pamoja na teknolojia za kutumia nishati ya jua, teknolojia ya kutumia pampu kufyonza maji ya baharini ili kuleta joto, na teknolojia ya kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo. Mfumo wa kutumia nishati ya jua umefungwa kwenye nyumba za wanamichezo kituo cha utoaji wa vifaa na huduma, mfumo huo unaweza kutoa joto kwa ajili ya madimbwi ya kuogelea na kutoa nishati safi kwa kuhakikisha uendeshaji wa kituo cha udhibiti wa hali ya joto au hali ya baridi ya jumba zima, ambao unaweza kuokoa umeme kwa unit zaidi ya laki 9 kwa mwaka.

Ili zana zinazotoa joto kwa nishati ya jua zilingane na hali nzuri ya jengo, wasanifu walitumia zana za kisasa duniani zilizo bapa, zimefungwa kwenye paa la jengo lenye umbo la upinde au umbo la bapa na kulifanya jengo lionekane kuwa la kupendeza zaidi. Na pampu ya kufyonza maji ya baharini ili kuleta joto, inatumika kwenye mfumo wa kudhibiti hali ya joto na hali ya baridi kwenye kituo cha vyombo vya habari. Pampu kama hiyo inatumia hali ya maumbile ya Jumba la mchezo wa mashua zenye matanga la Qingdao ambalo liko kwenye sehemu iliyo karibu na bahari, hivyo inaweza kutumia tofauti ya hali joto ya maji ya baharini kufanya kazi ya kudhibiti hali ya joto au hali ya baridi kwenye vyumba bila kutoa uchafuzi wowote. Aidha taa nyingi zinazotumia nishati ya upepo na nishati ya jua pia zinatumika kwenye Jumba la mchezo wa mashua zenye matanga la Qingdao. Bw. Li Zhipeng alieleza matumaini yake kuwa, kwa kupitia matumizi ya zana hizo za kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira, wazo la kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 katika mazingira yasiyo na uchafuzi litatia mizizi mioyoni mwa watu wengi zaidi. Alisema: "Tunatumia mbinu na teknolojia hizo za hali ya juu kwenye ujenzi wa Jumba la mchezo wa mashua zenye matanga, kwa ajili ya kufanya kazi ya kutoa vielelezo kwenye jamii, ili wananchi wengi zaidi waelewe wazo kuhusu kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 katika mazingira yasiyo na uchafuzi".

Uwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki tuliyojulisha ni kama majumuisho ya viwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing, tokea Beijing ikabidhiwe rasmi jukumu la kuandaa Michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 tarehe 13 Julai mwaka 2001, Beijing imetunga mpango kabambe wa maandalizi, na kuutekeleza hatua kwa hatua. Kuanzia mwishoni mwa mwaka 2003, ujenzi wa viwanja na majumba ya michezo ulianzishwa mjini Beijing, mpaka sasa ujenzi wa viwanja na majumba mengi ya michezo kati yao umekamilika kimsingi. Mwenyekiti wa Kamati ya uratibu wa Michezo ya Olimpiki ya majira ya siku za joto ya mwaka 2008 katika Kamati ya Olimpiki ya kimataifa Bw. Hain Verbruggen alisifu sana ujenzi wa viwanja na majumba ya Michezo ya Olimpiki mjini Beijing. Alisema: "Nasema kwa furaha kwamba, ujenzi wa viwanja na majumba hayo ya michezo unaendelea kwa mwendo sahihi, maana ujenzi wa miradi yote unafanyika kwa kufuata kwa makini mipango iliyowekwa, na ujenzi wa miradi yote uko kwenye njia sahihi. Hivyo nilipoona ujenzi wa viwanja na majumba ya michezo unakamlika katika hali nzuri, nilifurahi sana".

Wasikilizaji wapendwa, sasa tunatoa maswali mawili:

1. Ni viwanja na majumba ya michezo mangapi yanahitajika kwa ajili

ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008?

2. Uwanja wa michezo wa taifa ambako sherehe ya ufunguzi na ufungaji

wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing zitafanyika, unaitwaje kwa jina lingine?

Idhaa ya kiswahili 2007-11-27