Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-03 16:19:13    
Wakulima wajitahidi kustawisha biashara ya utamaduni ili kuondoa umaskini

cri

Uliyosikia ni sauti kutoka kwenye ukumbi wa kufanya mazoezi ya nyimbo na dansi katika mji wa Xining mkoani Qinghai, kaskazini magharibi mwa China. Vijana wafugaji kutoka sehemu mbalimbali mkoani walikuwa wakifanya mazoezi ya michezo yao. Ili kuhifadhi mazingira, serikali ya mkoa inatekeleza sera ya kuacha utumia mbuga kwa malisho, ili kupata mbuga za majani kama ilivyokuwa hapo awali, lakini wafugaji wamepungukiwa mapato. Serikali imechukua hatua nyingi ili kuwasaidia wafugaji kuongeza mapato yao. Moja ya hatua hizo ni kuwasaidia wafugaji wawe wasanii wa kuonesha michezo yao ya sanaa katika sehemu mbalimbali za vivutio nchini China.

Qinghai ni mkoa wenye wakazi wa makabila mengi, raslimali za utamaduni wa kikabila ni nyingi. Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya mkoa imekuwa inajaribu kuwawezesha wafugaji kuongeza mapato yao kwa njia ya kustaswisha biashara katika sekta ya utamaduni wa kikabila, na njia hiyo imekuwa na matokeo mazuri. Mfano ni kikundi cha Aysamai cha nyimbo na ngoma cha wilaya ya Ping An.

Mwaka 2004, naibu mkuu wa Idara ya Uenezi wa Utamaduni mkoa wa Qinghai Bw. Wang Xuande aliunda kikundi cha Aysamai kwa mkopo wa Yuan 8,000 kutoka benki. Katika miaka ya hivi karibuni kikundi hicho kilichokuwa na watu 66 hapo mwanzo, kimestawi na kuwa na watu 520, michezo ya sanaa ya kikundi hicho inaoneshwa karibu kote nchini China, na mapato yao yanaweza kuwa mara zaidi ya kumi kuliko wanakijiji wenzao. Bw. Wang Xuande alipokumbuka jinsi wanakijiji walivyokuwa nyumbani kwake kutoa shukurani, aliwaambia waandishi wa habari kwa furaha, alisema,

"Kwa kuonesha michezo kwa siku kadhaa tu, kila mmoja wa kikundi hiki amerudi nyumbani na Yuan elfu 12. Watu wa familia zao walisema 'Tunafurahi kweli, kumbe utamaduni umetuongezea mapato yetu."

Kutokana na ufanisi wa kikundi hicho, serikali ilishirikiana na makampuni ya utamaduni kuanzisha kituo cha mafunzo ya michezo ya sanaa kwa vijana. Meneja mkuu wa Kampuni ya Kiraia ya Utamaduni mkoani Qinghai Bw. Wang Xiaobo alisema.

"Wakazi wa Mkoa wa Qinghai wana mila ya kuimba na kucheza ngoma, na sifa hiyo inafaa kustawishwa. Kuandaa wasanii wa nyimbo na ngoma katika sehemu za ufugaji licha ya kuweza kuinua kiwango cha usanii wa kikabila, kuleta nafasi nyingi za ajira na pia kumestawisha soko la utamaduni."

Kwa mujibu wa matakwa ya Idara ya Utamaduni ya Mkoa wa Qinghai, mwanafunzi anatakiwa kuweza kucheza vizuri ngoma kumi katika muda wa mwezi mmoja. Ingawa wafugaji vijana wana kipaji cha kucheza ngoma, lakini katika muda mfupi kama huu kuweza kucheza ngoma za aina kumi pia ni taabu kwao. Tatizo hilo linatatuliwa vipi? Mwalimu wa ngoma ya kabila la Wamongolia mwenye uzoefu wa kufundisha ngoma zaidi ya miaka kumi Bi. Bao Guihua alisema,

"Kwa kifupi tunawafundisha kila kitendo kwa kuwashika mikono, na wakipata maendeleo walau kidogo tunawasifu, ili kuwapa moyo."

Mwalimu mwenye umri wa miaka 24 Bw. Cai Gongtai alikumbuka wakati alipokuwa anajifunza. Aliondoka nyumbani na kwenda kwenye mji mkubwa, alifanya juhudi nyingi ili kujipatia ufanisi wa kazi, hali ya vijana hao ilikuwa nzuri sana ikilinganishwa na hali yake alipokuwa mjini, serikali imewawekea mazingira mazuri ya mafunzo, Bw. Cai Gongtai mara kwa mara anawatia moyo akisema,

"Baada ya kumaliza mafunzo hapa msirudi nyumbani bali mwendelee na safari mpaka kwenye jukwaa la Beijing na hata nchi za nje. Ingawa safari hii itakuwa na milima na mabonde lakini mkiwa na nia mtafanikiwa."

Kutokana na kutiwa moyo na mwalimu huyo, wanafunzi hao wamejawa na matumaini makubwa kuhusu siku za mbele. Msichana wa Tibet Chimaocuo alisema,

"Tumaini langu ni kuonesha ngoma yangu ulimwenguni. Nataka kuwaambia marafiki wenzangu mafunzo yangu na hisia zangu, natumaini kuwa Watibet wengi watakuja kujifunza na kuonesha ngoma katika sehemu nyingine na kuboresha zaidi maisha yao."

Akiwa na furaha kuona maendeleo ya wanafunzi wake, mwalimu Cai Gongtai anatumai kuwa wanafunzi watakuwa na mtazamo wa mbali zaidi. Alisema,

"saulicha ya ngoma zao kuweza kuboresha maisha yao na kutangaza ngoma za kabila lao pia kutawasaidia Watibet waonee ufahari wa kabila lao."

Hivi sasa wafugaji wameongeza mapato yao kutokana na kufanya maonesho ya nyimbo na ngoma, pia wanapata mapato kutokana na kufanya maonesho ya picha za kuchorwa, ufinyanzi wa sanamu, utarizi, na picha za kukatwa za karatasi. Ili wafugaji waimarishe biashara yao ya sanaa, serikali ya mkoa wa Qinghai inawaunga mkono kwa hali na mali. Mkuu wa Idara ya Utamaduni ya Mkoa wa Qinghai Bi. Cao Ping alisema,

"Kila mwaka serikali ya mkoa inafanya maonesho ya vitu vya sanaa, na gharama kwa ajili ya nafasi za maonesho zinalipwa na serikali, na pia inatoa msaada kwa gharama za chakula, malazi na nauli."

Kutokana na kusaidiwa na serikali ya mkoa, biashara katika sekta ya utamaduni imepata maendeleo makubwa. Biashara hiyo licha ya kuwawezesha wafugaji kupata mapato pia inasaidia kustawisha uchumi mkoani humo. Naibu mkuu wa Mkoa wa Qinghai Bw. Ji Di Ma Jia alisema,

"Kwa kustawisha biashara ya sekta ya utamaduni, utamaduni wetu wa jadi wa kikabila umepata warithi wake. Tutaufanya utamaduni wetu wa kikabila utoe mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya uchumi wa mkoa wetu."

Idhaa ya kiswahili 2007-12-03