Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-04 14:05:45    
China yafanya juhudi kuendeleza uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi

cri

Madini ni maliasili muhimu, pia ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii. Kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China, mahitaji ya madini yamekuwa ni makubwa zaidi, lakini tatizo la uchafuzi wa mazingira linalosababishwa na uchimbaji wa madini limekuwa kubwa zaidi, ambalo linazuia maendeleo ya uchimbaji wa madini. Kuwa na migodi isiyosababisha uchafuzi wa mazingira na kuendeleza uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi kunakubaliwa na dunia nzima.

Mkutano wa 9 wa kimataifa wa uchimbaji wa madini wa China ulifanyika hivi karibuni mjini hapa Beijing. Maofisa wa serikali na wataalamu zaidi ya 2000 wa uchumi, biashara, sayansi na teknolojia kutoka nchi na sehemu zaidi ya 30 walihudhuria mkutano huo, na walifanya utafiti na majadiliano kwa mujibu wa kauli mbiu ya mkutano huo ambayo ni "kujipatia maendeleo kwa njia ya kisayansi, kuendeleza uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi". Kwenye mkutano huo waziri wa ardhi na maliasili wa China Bw. Xu Shaoshi alisema,

"Kutokana na maendeleo ya kasi ya uchimbaji wa madini, serikali, makampuni na watu husika wa nchi mbalimbali wanafuatilia zaidi masuala kadhaa makubwa yakiwemo uchimbaji na matumizi ya maliasili yasiyoharibu mazingira na uhifadhi wa mazingira. Kuendeleza uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi kumekuwa maoni ya pamoja ya watu duniani. China inafanya juhudi kujipatia maendeleo kwa njia ya kisayansi, kuendelea kushikilia kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira kuwa sera ya kimsingi ya taifa, na kuendeleza viwanda vya aina mpya kwa njia ambayo haitatumia nishati kwa wingi na kusababisha uchafuzi mwingi. Kauli mbiu ya "kujipatia maendeleo kwa njia ya kisayansi, kuendeleza uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi" imeonesha kuwa China inaendeleza viwanda vya aina mpya kwenye shughuli za uchimbaji wa madini."

Uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi unamaanisha kuwa si kama tu watu wanachimba madini kwa njia ya kisayansi, bali pia wanadhibiti athari ya uchimbaji wa madini kwa mazingira ya sehemu za migodi na sehemu zilizo kando ya migodi, na watu wanachukua hatua za kisayansi ili kuhakikisha kunakuwa na uwiano kati ya shughuli za migodi na uhifadhi wa mazingira. Shirikisho la uchimbaji wa madini la China linalenga kusukuma mbele shughuli za uchimbaji wa madini nchini China, mkuu wa shirikisho hilo Bw. Li Yuansheng alisema,

"Katika miaka ya karibuni, tumeimarisha utafiti kuhusu masuala makubwa, tumewasilisha serikalini vigezo vya kiwango cha chini kabisa cha uchimbaji wa madini muhimu na utafiti kuhusu vigezo vya kutathimini uchumi wa mzunguko wa maliasili ya madini, na kuandaa mwongozo kuhusu kubana matumizi ya maliasili ya madini na matumizi ya maliasili kwa njia mbalimbali."

Ujenzi wa migodi isiyosababisha uchafuzi ni mradi wenye utatanishi, ambao unaweza kuonesha kiwango cha matumizi ya migodi, uwezo wa kupata maendeleo endelevu na uwezo wa kuhakikisha uwiano kati ya maendeleo na uhifadhi ya mazingira ya sehemu fulani. Kampuni ya makaa ya mawe ya Datong iliyoko mkoani Shanxi ni moja ya makampuni yanayozalisha makaa ya mawe kwa wingi zaidi nchini China, ambayo kila mwaka inazalisha zaidi ya tani milioni 100 za makaa ya mawe. Mwezi Julai mwaka 2006, kampuni hiyo ilijenga eneo la uchumi wa mzunguko wa makaa ya mawe la Tashan, ambalo ni kituo kikubwa cha kisasa cha uzalishaji wa makaa ya mawe. Mkurugenzi wa ofisi ya uchunguzi wa madini ya kampuni hiyo Bw. Liu Sheng alisema,

"Tunapendekeza kuendeleza kampuni ambayo haitasababisha uchafuzi na inaaminika kwa njia ya kisayansi. Ikiwa ni kampuni inayoshughulikia maliasili, tunachimba madini bila ya kuchafua mazingira. Eneo la uchumi wa mzunguko wa makaa ya mawe la Tashan, ni mfano mzuri wa kuendeleza uchumi wa mzunguko. Kampuni yetu siku zote inafuata lengo hilo na lengo la kujenga jamii yenye masikilizano inayohifadhi mazingira na kubana matumizi ya nishati lililotolewa kwenye mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha Kikomunisti cha China, ili kutoa mchango wetu kwa maendeleo ya makampuni ya kiserikali na jamii ya China."

Kampuni ya madini ya Zijin ya China ni kampuni nyingine inayofanya uzalishaji kwa mujibu wa vigezo vya uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi. Kampuni hiyo iko katika mkoa wa Fujian ulioko kusini mashariki mwa China. Kampuni hiyo inatilia maanani uhifadhi wa mazingira kwenye uzalishaji, na inashikilia kanuni ya kutoendeleza kampuni kwa njia inayochafua mazingira. Katika miaka ya hivi karibuni, kwa ujumla kampuni hiyo imetumia fedha zaidi ya Yuan milioni 100 katika uhifadhi ya mazingira. Naibu meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Luo Yingnan alisema,

"Katika miaka ya hivi karibuni, Kampuni yetu imepata maendeleo ya haraka na ilinunua migodi mingi, hasa migodi ya watu binafsi. Baada ya kununua migodi hiyo, tuligundua kuwa kwenye migodi hiyo kuna vifaa vichache vya kuhifadhi mazingira. Hivyo mwaka huu tumesimamisha kazi za migodi kadhaa, hivyo faida ya kampuni yetu imeathiriwa, lakini nafikiri tunapaswa kufanya hivyo, ili kampuni yetu isishindwe na kutimiza maendeleo endelevu yenye masikilizano."

Juhudi zilizofanywa na makampuni ya uchimbaji wa madini ya China kuendeleza uchimbaji wa madini usiosababisha uchafuzi, zinatambuliwa na kusifiwa na idara za uchimbaji wa madini duniani. Mkurugenzi wa idara ya uwekezaji wa shughuli za uchimbaji wa madini ya kampuni ya mambo ya kifedha ya kimataifa ya Benki ya Dunia Bw. William Bulmer alisema,

"Benki ya Dunia inafurahi kuona kuwa serikali ya China, makampuni ya uchimbaji wa madini na idara nyingi husika za China zimetambua kuwa zinatakiwa kuchukua hatua kwa makini, ili hifadhi mazingira wakati zinapofanya uchimbaji wa madini nchini China au katika nchi za nje. Hii inaonesha wazi kuwa zina wazo la kujipatia maendeleo endelevu, tunaamini kuwa makampuni ya uchimbaji madini ya China yatafanya kazi muhimu zaidi, na yatakuwa mfano mzuri wa maendeleo endelevu ya shughuli za uchimbaji madini.