Balozi wa China nchini Zimbabwe Bw.Yuan Nansheng hivi karibuni alipohojiwa na waandishi wa habari wa shirika la habari la China Xinhua alisema, tangu mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ufanyike hapa Beijing, mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Zimbabwe yamepata mafanikio makubwa. Wimbi la kujifunza lugha ya Kichina limetokea nchini Zimbabwe, vikundi vya maonesho ya michezo ya sanaa ya China yanashiriki kwenye tamasha huko kwa mara ya kwanza, na utaratibu wa mawasiliano ya elimu kati ya nchi hizo mbili umeanzishwa, hayo ni mambo matatu makubwa ya mawasiliano ya utamaduni yaliyotokea kati ya China na Zimbabwe.
Bw. Yuan Nansheng alisema, Chuo cha Confucius kilichoanzishwa na Ofisi ya lugha ya Kichina ya China na Chuo kikuu cha Zimbabwe kilifunguliwa rasmi mwanzoni mwa mwaka huu, mafunzo ya lugha ya Kichina nchini Zimbabwe yalianzishwa rasmi nchini Zimbabwe, na lugha ya Kichina imewekwa kwenye masomo ya Chuo kikuu cha Zimbabwe. China ilituma walimu watano nchini Zimbabwe kutekeleza majukumu ya kufundisha wanafunzi lugha ya Kichina, idara ya lugha ya Kichina na maktaba iliyojengwa kwa msaada wa Ofisi ya lugha ya Kichina ya taifa la China ilianza kutumika. Hivi sasa watu 57 kutoka sekta mbalimbali nchini Zimbabwe wamehitimu rasmi kutoka kwa Chuo cha Confucius, kati yao watu 20 walipewa udhamini wa masomo wa serikali ya China.
Bw. Yuan alisema kuanzishwa kwa Chuo cha Confucius kumewavutia wakazi wengi wa huko, pia kumesababisha kuwepo kwa wimbi la kujifunza lugha ya Kichina nchini Zimbabwe. Mke wa rais Robert Mugabe wa Zimbabwe na maofisa wengi waandamizi wa idara za serikali wametoa maombi wakiwataka walimu wa China wa chuo cha Confucius wawafundishe lugha ya Kichina. Hivi sasa wakazi wengi wanapenda kutumia maneno machache ya lugha ya Kichina kuwasalimu wachina, na kituo cha televisheni kinatangaza zaidi na zaidi vipindi vinavyojulisha utamaduni, utalii na filamu za China, filamu ya televisheni ya China "Xiyouji" yaani "Matembezi ya magharibi" imependwa sana na wazimbabwe wengi.
Bw. Yuan alisema mwezi Mei mwaka huu kikundi cha maonesho ya michezo ya sanaa cha Hunan kiliwakilisha China kushiriki kwa mara ya kwanza kwenye tamasha la kimataifa lililofanyika mjini Harare, na kufurahiwa sana na watu mbalimbali nchini Zimbabwe. Kikiwa daraja la urafiki kati ya China na Zimbabwe, kikundi hicho cha maonesho ya michezo ya sanaa kilionesha ngoma ya jadi ya China na usanii wa sarakasi, ambapo watazamaji wa huko wanaona kihalisi mvuto wa utamaduni wa China.
Bw. Yuan alisema baada ya mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana hapa Beijing, utaratibu wa mawasiliano ya elimu kati ya China na Zimbabwe ulikamilishwa hatua kwa hatua, hii ilitoa fursa mpya kwa ajili ya mawasiliano ya utamaduni kati ya nchi hizo mbili. Hivi sasa wizara za elimu za nchi hizo mbili zilianzisha utaratibu wa mazungumzo ya wakati fulani kati ya pande hizo mbili. Mawasiliano ya moja kwa moja kati ya vyuo vikuu vya nchi hizo mbili yanazidi kuongezeka, uhusiano wa kirafiki umejengwa kati ya Chuo kikuu cha umma cha China na Chuo kikuu cha Zimbabwe, na chuo kikuu cha sayansi na teknolojia cha Hunan na chuo kikuu cha sayansi na viwanda cha Harare. Aidha idadi ya wanafunzi wa Zimbabwe waliopewa udhamini wa masomo wa serikali ya China mwaka huu iliongezeka mara moja kuliko ile ya mwaka jana.
Bw. Yuan Nansheng vilevile alieleza kuwa ingawa China na Zimbabwe zimepata mafanikio makubwa katika mawasiliano ya utamaduni baada ya mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, lakini ikilinganishwa na ushirikiano wa kisiasa, na ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, mawasiliano ya utamaduni bado yako nyuma, na yanahitaji kurekebisha njia ya kijadi ya mawasiliano ya utamaduni, na kuanzisha utaratibu mpya wa mawasiliano.
Bw. Yuan alisema hivi sasa mawasiliano mengi ya utamaduni kati ya China na Zimbabwe ni ya ngazi ya kiserikali, inapaswa kupanua eneo la mawasiliano, kuimarisha nguvu za mawasiliano, kuzihimiza kampuni za China zioneshe umuhimu mkubwa zaidi, na kushirikiana na serikali ili kuhimiza maendeleo ya mawasiliano ya utamaduni kati ya nchi hizo mbili.
Bw. Yuan alisema utamaduni wa Zimbabwe una mvuto wa kiafrika, inapaswa kufanya maonesho ya michezo ya sanaa na muziki ya Zimbabwe nchini China, ili kuwajulisha wachina kuhusu utamaduni wa Zimbabwe.
Bw. Yuan pia alisema tangu mwaka jana, kuenea kwa mafunzo ya lugha ya Kichina ni kazi muhimu katika mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Zimbabwe, lakini wakati huo huo inapaswa kuwajulisha zaidi wazimbabwe utamaduni wa China wa aina mbalimbali kama vile vyakula, mavazi na mapambo, michezo ya Gongfu na kazi ya utarizi na kadhalika.
Alipohojiwa na waandishi wa habari, Bw. Yuan Nansheng pia alizungumzia ushirikiano uliopo kati ya China na Zimbabwe katika sekta ya uchumi na biashara. Bw. Yuan Nansheng alisema tangu mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ufanyike hapa Beijing, China na Zimbabwe zilipata maendeleo makubwa katika ushirikiano wa sekta mbalimbali, hasa sekta ya kilimo, lakini ushirikiano huo bado uko kipindi cha mwanzo, na una mustakabali mzuri na fursa nyingi.
Bw. Yuan Nansheng alisema kuna fursa nyingi katika ushirikiano kati ya China na Zimbabwe kwenye sekta ya kilimo. Zimbabwe ina msingi mzuri wa kilimo na raslimali nyingi za kilimo, na ina mazingira mazuri ya kuendeleza kilimo ya kisasa. China iliipa Zimbabwe mashine kadhaa za kilimo, na pia iliiuzia dawa za kilimo.
Bw. Yuan alisema, mwaka huu ushirikiano kati ya China na Zimbabwe katika ujenzi wa miundo mbinu ya kilimo umeonesha umuhimu katika maendeleo ya kilimo ya Zimbabwe. Ujenzi wa kituo cha vielelezo vya ufundi wa kilimo cha Zimbabwe kitakachojengwa chini ya msaada wa China uko tayari kuanza. Alieleza matumaini yake kuwa kwa kupitia kituo hicho, uzalishaji wa vyakula nchini Zimbabwe utaongezeka, hali ya upungufu wa vyakula italegea, ufundi wa kilimo wa kisasa wa China utaenea, na China na Zimbabwe zitatimiza ushirikiano wa kunufaishana.
Bw. Yuan Nansheng alisema bado kuna fursa nyingi kwa China na Zimbabwe katika kupanua ushirikiano wa ujenzi wa miundo mbinu ya kilimo kati yao. Zimbabwe inahitaji uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje katika miundo mbinu kama barabara, mawasiliano na maji. Alizishauri kampuni za China nchini Zimbabwe ziongeze uwekezaji na kuharakisha mchakato wa ujenzi wa miradi zinazoshughulikia, vilevile alizitaka kampuni zenye nguvu za China zigombee kandarasi za miradi nchini Zimbabwe, ikiwemo upanuaji wa ujenzi wa uwanja wa ndege.
Bw. Yuan alisema kiwango cha shughuli za utengenezaji nchini Zimbabwe ni cha juu katika sehemu ya kusini mwa Afrika, mustakabali wa ushirikiano kati ya China na Zimbabwe katika sekta hiyo ni mzuri sana. Bw. Yuan Nansheng alisema China na Zimbabwe zina fursa nyingi katika ushirikiano kati ya kwenye sekta mbalimbali, vile vile zinakabiliwa na matatizo makubwa, kama upungufu wa fedha za kigeni, mafuta na umeme, matatizo hayo yameathiri imani ya wawekezaji kutoka nje. Lakini inaweza kutazamiwa kuwa, baada ya muda mfupi ujao, hali ya kisiasa na uchumi nchini Zimbabwe itaboreshwa zaidi.
|