Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-10 19:01:10    
Tamasha la nane la maonesho ya sanaa la China laonesha mafanikio mapya ya utunzi wa michezo ya sanaa

cri

Tamasha la nane la michezo ya sanaa linalofanyika kila baada ya miaka mitatu, imefungwa hivi karibuni mkoani Hubei.

Kuanzia tarehe 5 Novemba kwenye majumba zaidi ya 30 katika miji 6 mkoani Hubei, vikundi vya wasanii kutoka sehemu mbalimbali nchini China vinaonesha michezo yao na kugombea "tuzo ya Wenhua" ambayo ni tuzo ya ngazi ya juu kabisa kati ya tuzo za michezo ya sanaa nchini China.

Opera ya Chuan ni aina ya opera inayojulikana sana mkoani Sichuan. Kwenye tamasha hilo Kundi la Opera ya Chuan la mji wa Chengdu lilionesha opera ya aina hiyo iliyohaririwa kutoka kwenye mchezo wa kuigiza wa nchi za nje. Hadithi ya mchezo huo wa kuigiza ilihaririwa kuwa hadithi iliyotokea katika China ya kale kwamba, mzee wa familia moja tajiri alimfanya mtoto wake kama mtumwa, alilimbikiza mali nyingi, baadaye alioa msichana mrembo na kupata mtoto mwingine, alikuwa na matumaini kuwa mtoto huyo mdogo atarithi mali za familia yake. Hadithi hiyo imeeleza vilivyo jinsi wanafamilia walivyogombania mali kwa njama. Ingawa hadithi ni ya kale lakini mambo yanayoelezwa pia yanatokea sana katika jamii ya leo. Mwanafunzi Qin Shao ambaye kwa mara ya kwanza alitazama opera hiyo alisema, opera hiyo inamvutia kutokana na maneno ya waigizaji na vitendo walivyoigiza, na ilimfurahisha na kumhuzunisha. Alisema,

"Hadithi inavutia sana, mwanzoni inachekesha na kwenye mwishoni inahuzunisha, na inawaachia watazamani mambo mengi ya kudadisi zaidi. Mazingira ya jukwaani kama muungurumo wa radi, mwangaza wa taa, vinaongeza uzuri wa opera hiyo."

Mwanafunzi Qin Shao pia alisema, tofauti na opera za kawaida, muda wa opera hiyo si mrefu, matumizi ya mwangaza wa taa ni ya kisasa na mavazi pia ni maridadi.

Kwenye tamasha hilo, opera nyingi zinaoneshwa baada ya kuhaririwa kutoka kwenye opera asili za sehemu mbalimbali, zikionesha kwamba wasanii walifanya juhudi nyingi ili kuwavutia watazamaji na kuzifanya ziende na wakati. Opera ya Chu imekuwa na historia ya miaka zaidi ya 150 na inajulikana sana katika mkoa wa Hubei. Opera ya aina hiyo ina sifa ya kusimulia vilivyo wahusika walio ndani ya hadithi na inaeleza maisha ya kiraia. Lakini namna ya kuwavutia watazamaji na kuifanya opera hiyo ipendwe na vijana ni tatizo kwa opera za aina zote asili. Kundi la Opera ya Chu la Mkoa wa Hubei limefanikiwa kutunga mchezo uitwao "Harufu Nzuri ya Majani ya Chai" kwa opera ya aina hiyo ili kukidhi matakwa ya vijana.

"Harufu Nzuri ya Majani ya Chai" inaeleza jinsi msichana mmoja wa miaka ya 40 aliyebeba majani ya chai aliyochuma na kwenda mjini Wuhan kutafuta mchumba wake Tian Cheng, akitamani kufunga ndoa naye, lakini baada ya kufika aligundua kwamba Tian Cheng alimgeukia kwa kuwa mfanyabiashara tajiri mwenye ujeuri. Mwongozaji wa opera hiyo Bi. Chen Wei alisema, mtindo wa kimkoa, muziki uliohaririwa kwa mtindo wa kisasa na hadithi yenye maana kwa siku za leo, yote ni sababu za kuvutia watazamaji. Alisema,

"Kwa mujibu wa mahali ilipotokea hadithi hiyo mazingira ya jukwaani ni ya mji wa Wuhan wa zamani, barabara yenye maduka mengi, meli za mtoni na magati ambayo ni sura ya zamani ya Wuhan, na muziki wa opera umehaririwa kwa kuchanganya mtindo wa kisasa."

Bi. Chen Wei alisema, kupata watunzi vijana na kuhariri upya kwa mujibu wa opera ya jadi, ni njia nzuri ya kustawisha opera asili. Mwanamuziki mwenye umri wa miaka 70 Bw. Hu Xin alipotunga muziki wa opera ya "Harufu Nzuri ya Majani ya Chai" alifuata mahadhi ya opera ya jadi ya Chu lakini pia amechangana muziki wa aina nyingine. Anaona kuwa opera jadi inapaswa kuwa na umalumu wake na pia inapaswa kufanya marekebisho ili kukidhi furaha ya watazamaji wa leo. Alisema,

"Kama tukishikilia yale yale ya asili bila kurekebisha, watazamaji watayachoka, wanaona ni ya zamani na yamepitwa na wakati. Kwa hiyo tumeingiza mtindo mpya, kwa mfano, kuimba kwa mtu mmoja, watu wawili, watu watatu na hata kwa kwaya, lakini mahadhi hatukuyabadilisha, namna ya kuwaelezea wahusika wa hadithi haikubadilika, kwa hiyo watazamaji wanaposikiliza wanafurahi, hata waigizaji wanapoanza tu kuimba mara wanapigiwa makofi."

Madhumuni muhimu ya tamasha hilo ni kuhamasisha utunzi wa makundi mbalimbali ya wasanii. Kwenye tamasha hilo, michezo ya kuigiza, opera jadi, opera ya muziki na opera ya kuimbwa zimeibuka na mvuto wa kipekee.

Kundi la Opera la Mkoa wa Xinjiang limetunga opera ya muziki ya "Mgeni kutoka Milima ya Barafu" iliyohaririwa kutoka kwenye riwaya yenye jina hilo. Kwenye opera hiyo nyimbo ambazo ziliimbwa katika filamu ya hadithi hiyo zilipoimbwa jukwaani mara ziliitikiwa na watazamaji. Opera hiyo imeoneshwa kwa zaidi ya mara zaidi ya mia moja tokea ilipoanza kuoneshwa, na inapendwa sana na watazamaji. Mkuu wa kundi hilo Bw. Nusilet Wajidi alisema,

"Opera hii ni tofauti na opera ya Kimagharibi, tumekamilisha opera hiyo kwa muziki ambao watazamaji wameuzoea na wanaoelewa zaidi."

Bw. Nusilet Wajidi alisema, tofauti na opera jadi, opera ya muziki inalingana zaidi na matakwa ya watazamaji wa leo. Opera ya muziki kama hiyo iliyohaririwa kwa riwaya za zamani inaweza kupata soko kubwa.