Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-12-11 15:06:50    
Biashara yenye nguvu kubwa ya uhai kati ya China na Russia huko Manzhouli

cri

Tukizungumzia biashara ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, kaskazini mwa China na nje, hatuna budi kutaja mji wa Manzhouli. Mji huo uko kaskazini mwa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, unapakana na Russia na Mongolia, ambao ni forodha kubwa kabisa ya nchi kavu kati ya China na Russia. Katika miaka ya hivi karibuni, Manzhouli imekuwa inatumia ubora wake wa kijiografia, na kuendeleza biashara na Russia, na kiwango chake cha maendeleo ya kiuchumi kimekuwa kinainuka.

Katikati ya karne ya 19, China na Russia zilianza kufanya biashara ya mpakani huko Manzhouli. Hivi sasa, mji huo umekuwa forodha kubwa kabisa ya nchi kavu ya China kwa Russia, na kila mwaka bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na zinazouzwa kwa nje ambazo zinapitia kwenye mji huo zinachukua asilimia 60 ya biashara kati ya China na Russia.

Mjini Manzhouli, mtaa wenye ustawi kabisa wa biashara umekuwa kituo cha Warussia kununua bidhaa za China. Katika soko la mauzo ya jumla kwa Warussia na maduka yanayouza bidhaa za China, wafanyabiashara wa Russia wanaonekana kila mahali, na bidhaa wanazoulizia nyingi ni nguo na vyombo vidogo vya umeme vya nyumbani. Katika duka moja, mwandishi wetu wa habari alizungumza na mwenye duka Bw. Ye Xicheng, ambaye anatoka mji wa Yiwu mkoani Zhejiang, China. Bw. Ye alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, biashara yake huko ni nzuri, Warussia wanapenda sana bidhaa za China, alisema:-

"Nimekuwepo hapa Manzhouli kwa miaka mitatu au minne, nauza nguo, viatu, na bidhaa nyingine ndogo ndogo. Wateja wangu wengi kabisa ni Warussia, kila mwezi thamani ya uuzaji ni Yuan za RMB 10,000 hivi. Naona kuwa mustakabali wa biashara ya mpakani ni mzuri."

Kwa kuwa Bw. Ye Xicheng anafanya biashara na Warussia mara kwa mara, sasa hivi anaweza kuongea Kirussia vizuri. Sasa anafanya bidii kujifunza lugha ya Kimongolia, kwani watu wengi wa Mongolia pia wanafanya biashara huko Manzhouli. Baada ya kuagana na Bw. Ye Xicheng, katika duka lingine la nguo, mwandishi wetu wa habari alikutana na Bw. Vladislav anayetoka sehemu ya Baykal, Russia. Alimwonesha mwandishi wetu wa habari suruari aliyonunua kutoka kwenye duka la mchina. Alisema,

"Ninanunua vitu hapa Manzhouli mara kwa mara. Nina marafiki wengi hapa, naupenda mji wa Manzhouli. Mji huo ni mzuri. Nimewahi kununua nguo, suruari, viatu na simu hapa. Sifa ya bidhaa za China ni nzuri, tena bei ya bidhaa hizo ni ya chini."

Licha ya biashara hizo zenye thamani ndogo zinazofanywa mpakani, katika miaka ya hivi karibuni biashara kubwa kwa Russia mjini Manzhouli pia zimekuwa nyingi siku hadi siku. Ofisa wa huko Bw. Cao Haizheng alidokeza kuwa, zamani mji wa Manzhouli ulifanya kazi ya kupitisha bidhaa tu, ulisafirisha bidhaa za China na Russia kwa sehemu za ndani za nchi hizo mbili, lakini sasa, mji huo pia umeanza kuendeleza viwanda vya utengenezaji wa bidhaa zinazouzwa nje ambavyo vinafaa sehemu hiyo. Alisema,

"Mwaka jana, tulianza kufanya utengenezaji wa vifaa vya mbao vinavyoagizwa kutoka nje, sasa tunaweza kutengeneza vifaa vya mbao vyenye ujazo wa mita milioni 3 kwa mwaka. Pia tunafanya utengenezaji wa mboga na matunda kwa kuuza nje. Sasa tunafanya utengenezaji mwingi wa mboga, na mboga nyingi zinazouzwa kwenye sehemu za Russia zinatoka Hulunbeier mjini Manzhouli. Pia tuna viwanda vingine vya utengenezaji na uunganishaji wa vitu, vikiwemo zana za usafi, malori ya kilimo, vyombo vya umeme nyumbani na nyinginezo, ambavyo pia vimekuwa eneo la utengenezaji wa bidhaa zinazosafirishwa nje mjini Manzhouli."

Bw. Cao Haizheng alisema, Manzhouli inaweza kutimiza maendeleo hayo kutokana na kuwa na nguvu bora ya kituo cha usafirishaji. Kila siku magarimoshi karibu 10 kutoka Russia yanayobeba mafuta ghafi na mbao yanafika kwenye forodha ya Manzhouli, na magari yanayotengenezwa na China, mitambo ya umeme, nguo, matunda na mboga pia zinabebwa na magarimoshi hayo na kusafirishwa kwenda nchini Russia. Naibu mkurugenzi wa ofisi ya bandari ya Manzhouli Bw. Liu Weihe alisema,

"Forodha yetu kwenye njia ya reli hasa inashughulikia mizigo inayopita kwenye forodha, mwaka jana tulisafirisha mizigo tani milioni 21.71, na lengo letu la mwaka huu ni kusafirisha tani milioni 24 za mizigo. Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu tulisafirisha tani zaidi ya milioni 12 za mizigo, ambayo imezidi nusu ya lengo letu."

Imefahamika kuwa, miaka minane iliyopita kutokana na mazingira ya bandari ya Manzhouli kutokuwa nzuri, usafirishaji wa mizigo ulikuwa ni tani milioni 3 hivi kwa mwaka. Ili kuimarisha vivutio vya forodha hiyo, na kuhimiza ongezeko la kasi la usafirishaji kwenye forodha hiyo, kuanzia mwaka 1999 mji wa Manzhouli ulianza kuboresha mazingira ya forodha hiyo, na kufanya juhudi kuinua ufanisi wa kupitisha mizigo kwenye forodha. Kwa mfano, ili kuharakisha uuzaji wa mboga na matunda kwa nchi za nje, idara ya ukaguzi na karantini ya Manzhouli iliingiza zana za kukagua dawa za kilimo zinazobaki kwenye vyakula, ili kufupisha mchakato wa ukaguzi hadi siku moja kutoka siku tatu au nne, na kuhakikisha matunda na mboga zinazouzwa nchi za nje zikaguliwe na kupitishwa siku hiyo hiyo. Aidha forodha ya Manzhouli pia ilianzisha utaratibu wa usimamizi na udhibiti wa usafirishaji wa mizigo kwenye forodha, na kutumia teknolojia ya kisasa kabisa nchini China. Hatua hizo zimeongeza sana uwezo wa forodha ya Manzhouli wa kupitisha mizigo.

Mazingira mazuri ya forodha na ufanisi kasi wa kupita mizigo unakubaliwa na wafanyabiashara wa China na Russia. Mfanyabiashara wa China anayeshughulikia utengenezaji wa mbao Bw. Zhang Tieqiang alisema,

"Muda unaookolewa unabadilishwa kuwa fedha. Gharama ya sanduku moja imepungua kwa karibu Yuan za RMB 2,000."