Katika miaka ya hivi karibuni, familia nyingi zaidi za China zimenunua magari. Watu wengi wanajua kampuni ya Toyota ya Japan ambayo ni kampuni maarufu ya utengenzaji wa magari, lakini ni watu wachache wanaojua kuwa kampuni ya Aisin ina uhusiano wa karibu na kampuni ya Toyota. Kampuni ya Aisin ya Japan ni moja ya kampuni 500 yenye nguvu kubwa zaidi duniani. Katika miaka miwili iliyopita, kampuni hiyo ilifungua tawi lake mjini Tangshan, China.
Eneo la maendeleo ya teknolojia mpya za hali ya juu la Tangshan lilianzishwa mwezi Aprili mwaka 1992, ni moja ya maeneo manane makubwa ya maendeleo ya uchumi mkoani Hebei. Mwaka 2005 kampuni ya Aisin iliwekeza dola za kimarekani milioni 99.5 kuanzisha kampuni ya kutengeneza vipuri vya magari vya Aisin huko Tangshan, ambayo ilianza kufanya kazi rasmi mwaka 2006. Hivi sasa vipuri vinne hadi vitano vya kila gari la Toyota la aina ya Corolla vinatengenezwa na kampuni hiyo.
Kampuni ya vipuri vya magari vya Aisin ya Tangshan ambayo ni kampuni inayohusiana na kampuni ya magari ya Toyota ya Tianjin, ilianzishwa mjini Tangshan badala ya Tianjin kutokana na sababu tatu. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Hiroshi Chono alisema,
"Kwanza, ikilinganishwa na mji wa Tangshan, ni vigumu zaidi kuchagua na kuajiri mafundi mjini Tianjin. Pili, kampuni ya vipuri vya gia ya Aisin ya Tangshan iko kilomita 20 kaskazini ya eneo la maendeleo ya teknolojia mpya za hali ya juu la Tangshan, hiki ni kiwanda cha kwanza kilichoanzishwa na kampuni ya Aisin mjini Tangshan, na kiliiwezesha kampuni ya Aisin ifahamu hali nzuri ya uwekezaji mjini Tangshan. Tatu, viongozi wa serikali ya mji wa Tangshan na idara mbalimbali zinazoshughulia kuvutia uwekezaji za eneo la maendeleo ya teknolojia mpya za hali ya juu la Tangshan ni wachangmfu na wakarimu sana. Hivyo tuliamua kuanzisha kampuni yetu hapa."
Katika miaka miwili iliyopita, kutokana na maendeleo ya haraka ya viwanda vya magari nchini China, kampuni ya vipuri vya magari ya Aisin ya Tangshan pia ilipata maendeleo makubwa. Idadi ya wafanyakazi iliongezeka kwa mara 5 katika mwaka mmoja uliopita, na hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu, thamani ya uzalishaji ya kampuni hiyo imefikia yuan milioni 30.
Lakini wakati kampuni hiyo inapoendeleza uzalishaji kwa haraka, haijapuuza uhifadhi wa mazingira. Tarehe 30 mwezi Aprili, kampuni hiyo ilitangaza sera kuhusu mazingira, na kuahidi kuwa itabana matumizi ya nishati na kutumia nyenzo kwa mzunguko kwenye uzalishaji, kuzuia uchafuzi na kupunguza utoaji wa maji taka na hewa chafu, kutumia ufundi na rasilimali zinazosaidia uhifadhi wa mazingira na kuzalisha bidhaa zisizosababisha uchafuzi mwingi. Bw. Hiroshi Chono alisema,
"Kanuni moja muhimu ya kampuni ya Aisin ni kuhifadhi mazingira wakati wa uzalishaji. Tumetunga sera kuhusu mazingira kwa msingi huo. Hivi sasa kampuni ya Aisin ina matawi 35 hadi 40 duniani. Hadi kufikia mwaka 2008, ni lazima matawi yote yapate uidhinishaji wa kigezo cha mazingira cha ISO14001. Kampuni yetu ikiwa ni tawi la Kampuni ya Aisin, inaitikia mwito wa kampuni kuu na kufanya juhudi ili kupata uidhinishaji wa kigezo cha mazingira cha ISO14001."
Baada ya kutunga kwa sera kuhusu mazingira, sera hiyo ilichapishwa kwenye kadi ndogo, na kila mfanyakazi wa kampuni ya vipuri vya magari ya Aisin ya Tangshan alipewa kadi hiyo, ili afahamu wazo la kuhifadhi mazingira.
Licha ya kutunga sera maalumu kuhusu mazingira, kampuni ya Aisin pia inazingatia wazo la maendeleo endelevu kuwa lengo la kampuni hiyo. Bw. Hiroshi Chono alisema,
"Tunatilia maanani uwiano kati ya jamii na mazingira. Kampuni yetu ikiwa ni kiwanda cha uzalishaji, inazalisha bidhaa kwa kutumia nyenzo mbalimbali ambazo uchimbaji wake unaharibu mazingira kwa kiasi fulani, baada ya kuuza bidhaa masokoni, tunainua kiwango cha maisha na watu, na kuhifadhi mazingira na kupunguza uchafuzi wa mazingira ili kutimiza mzunguko mzuri.
Bw. Hiroshi Chono alisema kampuni ya Aisin imetambua kuwa serikali ya China ilitangaza sera na mawazo ya "kubana matumizi ya nishati na kupunguza utoaji wa hewa chafu na maji taka", "kuendeleza uchumi wa mzunguko" na "kutimiza maendeleo endelevu", pia imetambua nia na juhudi za serikali ya China katika utekelezaji wa sera hizo, na mabadiliko ya jamii ya China. Anaona kuwa wazo la maendeleo endelevu limekuwa maoni ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa, hali kadhalika kwa kampuni, alisema,
"Nilijiunga na kampuni ya Aisin mwaka 1972, hadi hivi sasa nimefanya kazi katika kampuni hiyo kwa miaka 35. Katika miaka 35 iliyopita, nimetambua kuwa maendeleo endelevu ya kampuni moja ni muhimu sana kwa wafanyakazi wake. Kampuni hiyo kuweza kuendelezwa kwa miaka 35 kunatokana na wazo la kutilia maanani uhifadhi wa mazingira, na uwiano kati ya mazingira maumbile na jamii. Maendeleo endelevu ya kampuni yanahitaji kutimiza mambo mawili, kwanza kampuni hiyo inaweza kuzalisha bidhaa zinazokubaliwa na watu wengi, pili kampuni hiyo inafuata njia ya maendeleo endelevu inayohifadhi mazingira ya kimaumbile. Jambo muhimu zaidi kwa meneja mkuu ni kujali maslahi ya wafanyakazi na kuifanya kampuni yake iendelezwe kwa miaka mingi zaidi."
Ni ukweli kuwa ni lazima kampuni moja itimize maendeleo endelevu, ili iweze kuzalisha mali kwa ajili ya jamii na kutoa uhakikisho kwa maisha na maendeleo ya wafanyakazi wake; na ni lazima jamii itimize uwiano kati yake na mazingira ili ipate maendeleo halisi. Wazo hilo limekubaliwa na wafanyakazi wengi wa kampuni ya Aisin. Msaidizi wa mkurugenzi wa ofisi ya mambo ya jumla ya magari ya kampuni hiyo Bibi Feng Yanying alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, mpango wa maendeleo wa kampuni hiyo umempatia fursa nyingi za kujiendeleza, alisema,
"Kampuni yetu iko katika eneo la maendeleo ya teknolojia mpya za hali ya juu, hivyo kampuni hiyo ina mustakabali mzuri wa kuendeleza teknolojia zake. Nikiwa ni mfanyakazi wa kampuni hiyo, nafikiri pia nina mustakabali mzuri sana."
|