Leo tunawaletea maelezo kuhusu hospitali ya msalaba mwekundu mjini Nanjing mkoani Jiangsu, Hii si hospitali ya kawaida, kwa kuwa inalenga kuwahudumia watu wenye pato la chini na inasifiwa na watu hao kuwa "hospitali ya kunufaisha umma". Hilo ni jaribio lililofanyika mjini Nanjing kwa ajili ya kuufanyia mageuzi utararibu wa matibabu wa mji huo na kuwezesha kila mkazi apate huduma za matibabu.
Hosptali ya msalaba mwekundu ya mji wa Nanjing ilianzishwa mwaka 2002. kwenye eneo la wodi la hospitali hiyo, mgonjwa wa saratani bibi Luo Yiying alikuwa anapumzika baada ya kupewa tiba ya kemikali, akitazama kipindi cha michezo ya Opera kwenye televisheni. Binti yake Bi. Zhuo Sibao alisema:
"hosptali hii ina mazingira mazuri, tunaweza kutazama televisheni. Huduma pia ni nzuri. Wauguzi na madaktari wote ni watu wema."
Bibi Luo mwenye umri wa miaka 73 ana watoto watano, lakini hivi sasa watoto wake wote hawana ajira. Katika miaka kadhaa iliopita, mzee huyo aligunduliwa kuwa na satarani ya mifupa, kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ya familia hiyo, Bi. Zhou Sibao alikuwa na wasiwasi sana, hospitali ya kunufaisha umma ndiyo iliyoondoa wasiwasi wake. Bi. Zhou Sibao alisema,:
"mama yetu amepatwa na ugonjwa huo wakati sisi hatuna ajira, akienda kupewa matibabu kwenye hospitali kubwa, itagharamia yuan elfu kumi kadhaa, kweli hatuwezi kumudu. Sasa serikali imeweka hospitali za kunufaisha umma, kwa kweli ni hatua nzuri, gharama nyingi za matibabu zimefutwa, sasa kwa ugonjwa huo, gharama za kipindi kimoja cha matibabu ya ugonjwa huo zimepunguzwa hadi kufikia yuan elfu 2 hadi elfu 4, zimepungua sana kuliko zamani. Sera hiyo kweli ni nzuri kwetu."
Hospitali za kunufanisha umma zinatekeleza sera 13 zenye nafuu au kufuta gharama kwa wagonjwa wenye matatizo makubwa ya kiuchumi waliothibitishwa na idara ya mambo ya kiraia. Wagonjwa wanaweza kunufaika kutokana na sera hiyo wakionesha kitambulisho cha wenye pato la chini tu. Si kama tu gharama za uandikishaji, uchunguzi wa magonjwa na matibabu ya msingi zimefutwa, gharama za kulipia kitanda, upasuaji na upimaji zimepunguzwa kwa nusu.
Kwenye ofisi ya fedha ya hospitali hiyo, ofisa alimwonesha mwandishi wetu wa habari orodha ya gharama za dawa zilizopunguzwa kwa wagonjwa kama ilivyokuwa kwa Bi. Luo Yiying.
Wagonjwa wenye matatizo ya kiuchumi wanaopewa matibabu au kulazwa kwenye hospitali za kunufaisha umma kwa wastani wanapewa nafaa za kupunguziwa asilimia 30 hadi 50 ya gharama, kama wakifanyiwa upasuaji au upimaji mwingine, watanufaika na nafuu kubwa zaidi ya malipo. Katika miaka mitano iliyopita, hospitali hiyo imetoa misaada ya matibabu kwa wagonjwa zaidi ya elfu 80, kwa jumla imefuta au kupunguza gharama za matibabu zaidi ya yuan milioni 4. wagonjwa waliopokewa na hospitali hiyo wanachukua karibu nusu ya watu wenye matatizo ya kiuchumi mjini Nanjing.
Mkuu wa hospitali hiyo Bw. Li Yuanhuai alipozungumzia mchango wa sera hizo katika kusaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi kupata matibabu, alisema:
"sera hizi kweli zimetatua matatizo kadhaa kwa wagonjwa wenye matatizo ya kiuchumi, hivi sasa masuala ya ugumu wa kupata matibabu na gharama kubwa za matibabu yamekuwa ni makubwa katika jamii. Watu hao wenye mapato ya chini wanamudu maisha ya msingi tu, hawawezi hata kidogo kumudu gharama za matibabu. Kutekeleza sera maalumu za kunufaisha umma, kunaweza kutatua suala la kupata matibabu kwa wakazi laki 1.3 wenye kipato cha chini."
watu wengine wana wasiwasi kuwa gharama za matibabu zikipunguzwa, hospitali itafanya nini ili kuhakikisha mapato, na sifa ya huduma na miundombinu hospitalini vinaweza kushuka kutokana na sera hizo? Daktari wa satarani wa hospitali hiyo Bi. Li Guifang alisema,
"miundombinu ya hospitali hiyo ni mizuri, kama vile wagonjwa wanaweza kuoga kwa maji ya moto, hospitali nyingi nyingine hazina huduma hii. Pia katika wodi kuna televisheni, vyombo vya kutoa Oxygen na mfumo wa kisasa wa kuita madaktari. Aidha, hospitali hiyo inataka madaktari kuwafanyia upimaji wagonjwa kwa makini na uvumilivu. Wagonjwa wanaridhika sana na huduma zetu."
Watumishi wengi kwenye hospitali hiyo wanafanya kazi bila malipo. Bi. Li Guifang ambaye alikuwa daktari mkurugenzi wa idara ya magonjwa ya damu na satarani kabla ya kustaafu, aliwahi kutibu magonjwa mengi magumu na ana sifa kubwa katika kazi hiyo. Hospitali nyingi zimewahi kumwalika kufanya kazi baada ya kustaafu, lakini hatimaye alichagua hospitali ya kunufaisha umma na kuhudumia wagonjwa maskini. Bi. Li Guifang alisema:
"nataka kutoa mchango wangu, sitaki malipo hata kidogo. Nakuja kuhudumia watu wenye matatizo ya kiuchumi. Kutokana na uzoefu wa miongo kadhaa, nadhani inanipasa kutoa mchango wangu."
Bei nafuu na huduma bora zimeziletea sifa nzuri hospitali za kunufaisha umma moyoni mwa wakazi wa Nanjin. Maoni hayo ya pamoja pia yamehimiza zaidi maendeleo ya hospitali hizo.
Mjini Nanjing kuna hospitali 12 nyingine kama hospitali ya msalaba mwekundu. Kuanzisha hospitali hizo ni moja ya hatua zilizochukuliwa na serikali kwa ajili ya kutatua suala la ugumu wa kupata matibabu kwa watu wenye matatizo ya kiuchumi.
|