Kuanzia miaka 70 ya karne iliyopita China ilipoanza kufungua mlango, wageni wengi kutoka nchi za nje walikuja China kufanya kazi, kusoma na kuishi. Mwanzoni wengi kati yao waliishi katika miji iliyoko pwani ya kusini mashariki mwa China, lakini sasa watu kutoka nchi za nje pia wanapenda kuishi, kufanya kazi na kusoma katika miji iliyoko katikati na magharibi mwa China. Katika kipindi hiki kwa wiki tatu mfululizo tutawaletea maelezo kuhusu mzee wa kijapan Bibi Shizuko Sakamato anayeishi mjini Chengdu na kufanya kazi ya kujitolea.
Mliyosikia ni sauti ya Bibi Shizuko Sakamato alipokuwa anawafundisha wachina kuimba wimbo wa kijapani. Kila wikiendi, katika shule hii ya lugha ya kijapani iliyoko kwenye Jumba la urafiki kati ya China na Japani la Chengdu, huandaa shughuli mbalimbali kwa wakazi wa Chengdu wanaopenda kujifunza lugha ya kijapani na kuelewa hali ya Japani, na kuwafahamisha desturi na utamaduni wa Japani.
Bibi Shizuko amefanya kazi katika shule hii ya lugha ya kijapani kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2004. Alikwenda Chengdu kufanya kazi ya kufundisha lugha ya kijapani kutokana na safari aliyofanya nchini China katika mwaka 1988. Alisema,
"Katika safari hiyo ya siku 7, nilitembelea Beijing, Chengdu, Guilin, Guangzhou na Hongkong. Wakati nilipokaa mjini Chengdu mvua ilinyesha kwa siku mbili, niliona kuwa Chengdu ni mji wenye rangi ya kijivu."
Lakini anaukumbuka mji wa Chengdu. Kwa sababu alikutana na Bibi Li Huiqun ambaye alikuwa anafanya kazi katika duka moja la bidhaa za utalii. Bibi Shizuko alimpiga picha Bi. Li Huiqun, kwani aliona tabasamu yake inamvutia, na aliahidi kuwa atamtumia picha hizo baada ya kurudi nyumbani Japan. Lakini baada ya kurudi nchini Japan, picha hazikutokea kutokana na filamu kutowekwa vizuri. Alisikitika sana na alimwandikia barua Bibi Li Huiqun. Alisema:
"kwa sababu wakati huo sikuweza kuongea kichina, hivyo nilimwandikia barua kwa kijapani. Nilikuwa na matumaini kuwa mtu anayeelewa kijapani ataweza kumsomea. Baada ya mwezi mmoja, nilipata barua kutoka kwa Li Huiqun, pamoja na muhuri wenye jina langu. Nilifurahi sana. Ingawa sikuielewa barua ile, niliwauliza watu wengi, baada ya nusu mwaka niliielewa vizuri barua ile."
Baadaye Bibi Shizuko alimwandikia tena barua Bibi Li Huiqun. Lakini hakupata majibu na kupoteza mawasiliano naye. Baada ya miaka mitatu, Bibi Shizuko alikutana na mtu mmoja kutoka Chengdu ambaye alikuwa anasoma huko Hiroshima, na kupata habari ya Bibi Li Huiqun. Tangu hapo, watu hao wawili waliwasiliana sana na kuwa marafiki mzuri.
Mume wa Bibi Li Huiqun Bw. Xie Zhengfu alituambia kuwa, mwanzoni alikuwa hakubali Bi. Li Huiqun afanye mawasiliano na Bibi Shizuko. Kwani katika vita dhidi ya uvamizi wa Japan iliyotokea miaka ya 30 hadi miaka ya 40 ya karne iliyopita, jamaa kadhaa wa Bw. Xie walidhuriwa hata kuuawa. Baada ya muda fulani, aliambiwa kuwa Bibi Shizuko ni mtu anayepinga vita, hivyo alibadilisha maoni yake. Alisema,
"Yeye anaipenda China. Niliambiwa kuwa familia yake pia ilipata madhara katika vita hiyo, yeye anapinga sana vita. Pia yeye ni mjumbe wa shirikisho la urafiki kati ya Japan na China la mji wa Hiroshima, hivyo nilibadilisha maoni yangu."
Idhaa ya kiswahili 2007-12-27
|