Hivi karibuni kitabu cha "Ripoti kuhusu Maendeleo ya Huduma za Kiutamaduni Mwaka 2007" kimetolewa na Taasisi ya Sayansi ya Jamii ya China. Kitabu hicho kimeeleza maendeleo ya huduma za kiutamaduni kwa pande zote ikiwa ni pamoja na shughuli za mambo ya sanaa, uandishi wa habari, uchapishaji, matangazo ya redio na televisheni. Hiki ni kitabu cha kwanza kuhusu hali ya maendeleo ya huduma za kiutamaduni nchini China. Kwenye uzinduzi wa kitabu hicho, wataalamu walisema, huduma za kiutamaduni kwa umma zimekuwa zikibadilika, serikali inazidi kutenga fedha nyingi ili wananchi wanufaike na maendeleo ya utamaduni.
Kwenye kituo cha utamaduni na michezo kilichopo katika sehemu ya Wukesong mjini Beijing kuna wakazi wengi wanaocheza diabolo. Diabolo ni kama gurudumu dogo lililotengenezwa kwa mwanzi, ndani yake ni tupu na kwenye mzunguko imechongwa midomo kama mdomo wa kipenga, inapozungushwa kwa uzi inatoa sauti inayoburudisha. Mchezo huo unachezwa sana katika mji wa Beijing. Mwaka uliopita mchezo huo uliorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni wa China. Kwenye kituo cha Wukesong tuliona baadhi ya watu wakicheza kwa uhodari mkubwa kama wanasarakasi. Bw. Tao Yuying aliyetoka mji wa Chongqing alisema, kwa kiasi fulani mchezo huo unamfanya aone furaha ya kuishi mjini Beijing. Alisema,
"Mwanzoni nilipokuja Beijing, nilikuwa sioni raha kuishi hapa na nilitaka kurudi nyumbani, lakini baadaye nilipopita hapa kituoni niliona watu kadhaa wakicheza diabolo, nilijifunza kwao na nikaweza. Baada ya mwaka mmoja kikundi cha wachezaji wa diabolo kilianzishwa, kikundi hicho kina mkuu, naibu mkuu na mwalimu wa kufundisha, mimi ndio mwalimu. Hivi sasa kikundi chetu kimekuwa na watu karibu 50, wote ni wakazi wa karibu na kituo hiki."
Kituo hicho ambacho bado kiko mbioni kujengwa kina eneo la hekta 52. Kati ya majengo yaliyopangwa kujengwa ni pamoja na jumba la mashindano ya mpira wa kikapu la michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 na miundombinu mingine ya michezo ya Olimpiki hiyo. Baada ya michezo ya Olimpiki kumalizika, wakazi wa sehemu hiyo ya Wukesong watanufaika na majengo hayo kwa ajili ya kuimarisha afya na burudani. Ingawa majengo hayo bado hayajakamilika, sehemu za pembezoni mwa majengo zinawavutia wakazi wengi kucheza michezo ya aina nyingi na kuimba kwa pamoja.
Kituo hicho kwenye sehemu ya Wukesong ni moja kati ya vituo vingi vinavyojengwa katika sehemu mbalimbali nchini China. Hivi sasa, katika sehemu nyingi nchini China zimejengwa maktaba, majumba ya makumbusho, majumba ya kuonesha michezo ya sanaa, majumba na viwanja vya michezo na sehemu za miti na majani. Vituo vya kutoa huduma za kiutamaduni kwa umma vinaongezeka haraka kote nchini.
Mtaalamu wa Kituo cha utafiti wa utamaduni cha Taasisi ya Sayansi ya Jamii ya China Bw. Zhang Jiangang alipozungumza na waandishi wa habari alisema, China imeandaa mpango wa kufikisha kwenye nchi nzima mtandao wa huduma bora za kiutamaduni kwa umma kabla ya mwaka 2020. Katika miaka ya hivi karibuni, pato la taifa la China linaongezeka haraka, toka mwaka 1999 hadi 2006 pato la taifa limeongezeka kwa mara mbili. Kutokana na msingi huo, fedha zinazotengwa kwa ajili ya huduma za kiutamaduni pia zinaongezeka mwaka hadi mwaka, hivi sasa mfumo wa huduma za kiutamaduni kwa umma umekuwa kwenye kipindi cha mabadiliko makubwa ya kihistoria.
"Katika miaka ya karibuni fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha huduma za kiutamaduni kwa umma zinaongezeka mwaka hadi mwaka, na ongezeko hilo linazidi kuliko kasi ya ongezeko la pato la taifa. Katika sehemu zinazostawi zaidi kiuchumi ongezeko hilo hata ni kubwa zaidi. Fedha zinazowekezwa kwa ajili ya huduma hizo zimeongezeka kutokana na msingi imara wa kiuchumi nchini China."
Bw. Zhang Jiangang alisema, ustawi wa uchumi umeiwezesha serikali kushughulikia huduma muhimu za kiutamaduni kwa umma. Mwaka 1998, ili kutatua matatizo ya kusikiliza matangazo ya redio na televisheni, Kamati ya Maendeleo na Mageuzi na Wizara ya Fedha na Idara Kuu ya Redio, Filamu na Televisheni zilitekeleza mradi wa kueneza matangazo ya redio na televisheni kwenye kila kijiji, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005 fedha zilizotengwa zilifikia yuani bilioni 3.6 kwa jumla, wakulima karibu milioni mia moja sasa wanapata matangazo ya redio na televisheni.
Mwaka 2002 Wizara ya Utamaduni na Wizara ya Fedha za China zilianzisha mradi wa kunufaika na habari za utamaduni kwa wananchi wote, maana yake ni kuwa watu wa sehemu za mbali na wakulima wanaweza kusoma vitabu na kuangalia michezo ya sanaa na teknolojia kwa kupitia mtandao wa internet. Katika muda wa miaka mitano iliyopita, kila mkoa umeanzisha tovuti tanzu ya mtandao na tovuti za vijijini zimefikia zaidi ya laki 3.5. Kutokana na mpango, hadi kufikia mwaka 2010 kimsingi China itakuwa imekamilisha mtandao unaofika kwenye miji yote na vijiji vyote nchini China.
Mwaka 2006 Idara Kuu ya Uandishi wa Habari na Uchapishaji ya China ilianzisha mradi wa kujenga "maktaba kote vijijini", kwa mujibu wa mpango huo katika muda wa miaka mitano maktaba laki mbili zitajengwa vijijini, na kila maktaba itakuwa na vitabu kiasi cha elfu moja, magazeti aina zaidi ya kumi na video zaidi ya aina mia moja, ili kuwapatia wakulima elimu kuhusu sera, teknolojia, afya na michezo ya sanaa.
Bw. Zhang Jiangang alisema katika miaka ya hivi karibuni kadiri ya uchumi unavyoendelea kukua, ndivyo fedha kwa ajili ya huduma za kiutamaduni zitaendelea kuongezeka.
|