Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-08 15:10:50    
Barua 0106

cri

Msikilizaji wetu Gunyanyi Patson wa sanduku la Posta 110 Chavakali, Kenya ametuandikia barua anasema yeye anaishi huko maragoli.wilaya ya vihiga,ambapo amekuwa anasikiliza vipindi vya Radio China Kimataifa kila siku,kwa miaka minne iliyopita,na amejifunza mengi kuhusu bara la Afrika,nchi ya china na dunia kwa jumla. Anasema wakati anaposikiliza kipindi kama Jifunze kichina hujiandaa kwa kuwa na kalamu na daftari. Huandika maneno kidogo kwa sauti ya kichina, na maana ya maneno hayo kwa Kiswahili. Ametoa mfano wa maneno hayo kama vile, Siesie ? Asante, Ni hao ? Hujambo, Nien ? mwaka

Anasema yeye pamoja na rafiki zake hupitia maneno hayo ya kichina hadi wajue maana yake.

Anaendelea kusema kuwa hiyo ndiyo njia pekee kwao ya kuweza kujifunza kichina, lugha wanayotamani sana kuijua katika maisha yao, kwani akipata nafasi ya kuja China ataweza kuwasiliana na wachina bia kuwa na msaidizi. Kila siku anaomba apate chuo ili aweze kujifunza kichina. Pia wakati wa vipindi huandaa ramani inayoonesha nchi ya China na kutazama mito, milima, mikoa, miji, na visiwa vya China.

Anasema alishangaa kuona kuwa sehemu kubwa ya China ni jangwa na milima kama Afrika. Hivyo anaomba wachina na waafrika wote wafanye bidii ili kustawisha sehemu hizo. Anaishukuru nchi ya China kwa misaada yote ambayo inatoa kwa nchi za Afrika.

Alifurahi aliposikia china imefuta madeni inayoidai Kenya,na aliwaombea kwa mungu viongozi wa china wawe na afya njema na maisha mazuri. Anasema alikosa usingizi kwa wiki nzima mwaka jana, aliposikia kuwa China imewaalika viongozi wote wa Afrika kuja mjini Beijing kwa ajili ya mashaurino ya kiuchumi, kwani alitamani kuwa miongoni mwa watu walioalikwa.

Anasema nchini Kenya yeye ni mnunuaji mzuri wa bidhaa za China. Bidhaa hizo za China ambazo yeye hununua ni pamoja na Radio, sahani, viatu, kofia, nguo na vikombe. Ana matumaini kuwa uhusiano kati ya Kenya na China utazidi kuendelezwa. Pia anasema alifurahi sana mwaka 2004,wakati China ilipopata mafanikio katika michezo ya olimpiki huko Athens. Anasema kitu kinachomsumbua kwa hivi sasa ni kama atahudhuria michezo ya olimpiki itakayofanyika mjini Beijing mwaka huu wa 2008.

Kwa upande mwingine anasema huwa anasikitika sana anapopata habari kuhusu majanga yanayoikumba nchi ya china na Afrika. Anaendelea kusema kuwa siku moja walipokuwa darasani mwalimu wao wa somo la Jiografia aliwaambia kuwa tetemeko kubwa la ardhi liliwahi kutokea katika mji wa Tangshan, mkoani Hebei nchini China na watu wengi walipoteza maisha. Anasema alishtuka kwa ghafla na moyo wake ulianza kudunda kwa kasi na siku hiyo hakuweza kuelewa chochote darasani kwani akili yake ilikuwa kwa wachina waliopoteza ndugu zao.

Pia anasema mwezi mmoja uliofuata wakati akisikiliza taarifa ya habari kutoka Radio China Kimataifa, alisikia tetemeko la ardhi limetokea mkoa wa Mongolia ya ndani na watu wengi wamekufa. Anasema alizima Radio na kuacha kusikiliza vipindi vyote na kuanza kuwaombea wachina walioathirika na kimbunga, dhoruba na mafuriko wa mikoa ya Hubei, Fujian, Guangdong, Guizhou, Guangxi na Jiangxi.

Lakini pia huwa anapata huzuni anaposikia milipuko imetokea katika migodi ya makaa ya mawe, kumwagika kwa sumu katika mto huko Harbin na Heilongjiang, ajali ya ndege huko Baotou, Mongolia ya ndani pamoja na magonjwa kama SARS na homa ya mafua ya ndege.

Anasema kwa kwa kuwa ni mara yake ya kwanza kutuandikia, hivyo anapenda tumtambue kama mmoja wa wasikilizaji wetu. Anaomba watayarishaji wa vipindi kwenda kutembelea nchi ya Kenya na kuona mambo mbali mbali kama vile picha zinazoonesha bara la Afrika.

Tunamkaribisha kwa mikono miwili kuwa mwanachama wa Radio China Kimataifa, ni matumaini yetu kuwa, ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo yake.

Mwisho anapenda tumtumie kadi za salamu na gazeti la picha(Fotografia) na majina ya viongozi wa zamani wa China na mikoa waliyozaliwa. Marais na mawaziri wakuu wa China toka uhuru, mikoa waliyozaliwa na muda walioongoza. Mawaziri wa sasa na mikoa wanayotoka, ukuta mkuu, mfereji wa maji, mito Changjiang na Huanghe, milima ya manjano na jangwa la Gobi.

Pia anapenda kuwasalimia wafuatao.

Chahale Elvis wa Sundi,Maragoli

Adolwa Kennedy,Amisi Edwin,Evans Lumadede,

Lusina Stephen na Jananga Fednant waote wa Chavakali.

Sandaki Godfrey wa Buruburu,Nairobi

Ujumbe: Je wanajua kuwa Radio China Kimataifa, ndiyo mwanzo wa maisha mapya?

 

Idhaa ya kiswahili 2008-01-08