Katika shule ya kwanza ya sekondari ya kampuni ya utengenezaji wa mashine ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, kuna mwalimu mmoja msichana kutoka Marekani, jina lake la Kichina ni Chen Yusi, alikuja China kujitolea kufanya kazi ya kufundisha kiingereza miaka mitatu iliyopita.
Mwaka 2005, Bi. Chen Yusi aliyehitimu kutoka chuo kikuu alijiunga na kampuni ya raslimali ya kimataifa ambayo inashughulikia kutuma walimu wanaojitolea kwenye sehemu mbalimbali duniani. Kutokana na njia hiyo, Bi. Chen Yusi alikuja China na kuanza kazi kwenye shule hiyo. Lakini hiyo haikuwa mara yake ya kwanza kuja China. Bi. Chen Yusi aliwahi kuja nchini China mwaka 2004, na kuwa mwalimu wa kambi ya mafunzo ya Kiingereza kwa muda wa miezi miwili. Katika miezi hiyo miwili, Bi. Chen Yusi alianza kuipenda China na kuwapenda watoto wa China. Alisema:
"nawapenda watoto hao, kwa hivyo baada ya kuhitimu kutoka kwenye chuo kikuu nchini Marekani, niliamua kurudi China na kuanza kazi ya kufundisha Kiingereza."
Mwanzoni, Bi. Chen Yusi alikuwa anataka kwenda kwenye mji wa pwani Dalian, lakini kampuni yake iliamua kumtuma kwenda mji wa Baotou kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani. Alitafuta habari kuhusu mji huo na kugundua kuwa mji huo una dhoruba ya mchanga na baridi kali. Bi. Chen Yusi alisema:
"nilipofika kwenye mji huo, nilikuwa nadhani Baotou kweli ni mji mdogo sana, hakuna majengo marefu wala wakazi wengi. Halafu tulipanda gari na kufika kwenye sehemu ya katikati ya mji huo, niliona kuwa mji huo unaendelezwa. Lakini katika muda wa miaka mitatu ambayo nilikaa mjini humo, nilishuhudia mabadiliko mengi na mji unaendelea kuboreka."
Kutokana na tofauti za utamaduni kati ya China na Marekani, kila mara Bi. Chen Yusi alipokwenda madukani, watu wengi walikuwa wanamwangalia, mwanzoni hakujisikia vizuri. Bi. Chen Yusi alisema:
"mwanzoni nilikuwa nashangaa sana, kwa kuwa watu wote walikuwa wananiangalia kama kuwa mimi ni nyota. Nilichukua kitu kutoka kwenye shubaka la bidhaa, watu wengi walikuwa wanasimama nyuma yangu wakishangaa, anaangalia nini? amechukua kitu gani? Hii ni njia tofauti ya maisha, mwanzoni ilikuwa ni vigumu kuzoea."
Lakini baadaye Bi. Chen Yusi alianza kuzoea na ukarimu wa wakazi wa huko. Alisema hivi sasa, anajua kuwa watu hao ni marafiki wakarimu hasa kwa wageni.
Ili kuizoea jamii ya huko, Bi. Chen Yusi alianza kujifunza lugha ya Kichina. Katika muda wa miaka mitatu, ameweza kuzungumza Kichina vizuri na kuwasiliana na wanafunzi wake bila matatizo. Wanafunzi wakiwa na shida pia wanaweza kumwambia mwalimu huyo. Bi. Chen Yusi amekuwa mwalimu na rafiki mkubwa wa wanafunzi. Bi. Chen alisema:
"wanafunzi wa China wanakabiliana na shinikizo kubwa, na baadhi ya wakati wanachoka sana. Najua wanaishi kwa furaha, naona wakicheza pamoja na kufanya mazungumzo, wana marafiki wengi, wanaonekana wanafurahi, lakini naweza kuona shinikizo kwenye macho yao. Wao hawana budi kujifunza kwa bidii ili kujiunga na vyuo vikuu. Hata wakijiunga na vyuo vikuu, watafikiri kama wataweza au la kupata ajira nzuri baada ya kuhitimu vyuo vikuu. Kweli wanakabiliwa na shinikizo kubwa."
Kutokana na hali hiyo, Bi. Chen Yusi alifundisha Kiingereza kwa njia ya kimichezo, ili kuongeza hamu ya wanafunzi kujifunza lugha hiyo, pia michezo inaweza kusaidia kuwapunguzia shinikizo kwa muda. Baada ya masomo, Bi. Chen Yusi aliwaalika watoto kuwenda nyumbani kwake, kuwapikia kwa vyakula vya kimarekani na kuwafahamisha kuhusu utamaduni wa Marekani. Mwanafunzi wake Zhang Jing alisema:
"naona yeye ni mwalimu hodari, kweli anatufundisha mambo mengi halisi, kama vile utamaduni wa Marekani, matumizi ya Kiingereza fasaha cha kimarekani, au tofauti kati ya Kichina na Kiingereza katika maandishi. Kweli tunaweza kujifunza mambo mengi. Pia anashiriki kwenye michezo pamoja nasi. Naona mwalimu huyo ni mzuri sana, ana uvumilivu mkubwa."
Mbali na kazi, Bi. Chen Yusi pia anapenda kufanya urafiki na watu wa China. Kwenye tafrija moja mwaka jana, Bi. Chen Yusi alikutana na mchumba wake mchina. Bi. Chen Yusi alisema:
"nafurahi kuwa nilikuja Baotou, nina marafiki wengi hapa, na nimechumbiwa na mwenyeji wa hapa, tutafunga ndoa mwakani. Kwa hiyo ni Mungu aliyenituma kwenye mji huo, kwa kuwa alijua nitakuwa na furaha hapa, nitakutana na mume wangu katika mji huo."
Uhusiano wao unaungwa mkono na wazazi wao, na wanapanga kufunga ndoa mwaka kesho nchini Marekani. Bi. Chen Yusi alisema:
"tutafunga ndoa mwezi Agosti mwaka 2008, kwenye kanisa la Bibi yangu, kanisa hilo ni zuri sana, kwa hivyo tutafunga ndoa huko. Lakini baadaye tutarudi na kuishi nchini China kwa miaka kadhaa."
|