Nyumba ina kazi muhimu ya kuwapa binadamu uhifadhi dhidi ya baridi, hasa kwa watu wanaoishi mkoani Jilin, kaskazini mashariki mwa China, ambapo kwa kawaida halijoto ni chini ya nyuzi sifuri katika majira ya siku za baridi. Mwaka huu watu waliokuwa wanaishi katika nyumba za muda walikuwa wamehamia kwenye nyumba za kisasa kabla ya kuwadia kwa siku za baridi kali.
Nyumba za muda ni nyumba zilizojengwa mijini kwa kutumia udongo na mawe miaka zaidi ya 50 iliyopita wakati China mpya ilipoanzishwa. Huko Changchun, mji mkuu wa mkoa wa Jilin, kulikuwa na nyumba za muda zenye eneo la mita za mraba milioni 7.
Majira ya baridi ni muda mbaya sana kwa wakazi wanaoishi kwenye nyumba za muda mkoani Jilin, kutokana na kuwa nyumba hizo haziwezi kukinga baridi kali na inayodumu kwa muda mrefu. Bw. Zhou Ruifan mwenye umri wa miaka 51 ni mkazi wa mji wa Changchun, alikuwa anaishi kwenye nyumba ya muda kwa miaka zaidi ya 20. Familia yake ya watu watano ilikuwa inaishi ndani ya nyumba moja yenye eneo la mita za mraba 20 tu. Bwana huyo alizungumzia kwa huzuni matatizo yaliyowakumba. Akisema "Nilikataa tamaa. Unajua? Mvua ikinyesha maji yaliingia ndani, msingi wa ukuta wa nyumba ulizama kwenye maji kiasi kwamba nyumba ilikaribia kuanguka."
Kutokana na msongamano kubwa wa nyumba, mikwaruzano ilikuwa inatokea mara kwa mara kati ya majirani. Mkazi mmoja Bibi Wei Chunli alikuwa anasumbuliwa na kuzuiliwa kwa bomba la maji taka. Alisema kila mvua ikinyesha, alikuwa anazuiliwa kwa bomba la maji taka nyumbani kwake, na maji taka kuingia kwenye nyumba za majirani. Matukio kama haya yaliharibu ujirani mwema.
Sambamba na utandawazi wa mji, majengo mengi mapya yenye ghorofa yalijengwa na watu wengi walihamia kwenye nyumba za kisasa. Lakini kununua nyumba za kisasa ni kama ndoto tu kwa wakazi wanaoishi kwenye nyumba za muda kwani wanategemea pensheni au mapato ya chini.
Mwishoni mwa mwaka 2005 serikali ya mkoa wa Jilin ilitoa mpango wa kuboresha mazingira ya kuishi kwenye maeneo ya nyumba za muda yenye eneo la mita za mraba milioni 15 ndani ya miaka mitatu. Kutokana na mpango huo wakazi wapatao milioni moja kutoka familia zaidi ya laki 3 watanufaika. Mpango huo ulianza kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka 2006.
Mwezi Novemba mwaka 2007 ujenzi ulipomalizika, Bibi Wei Chunli na majirani zake walipata ufunguo wa nyumba mpya za kisasa. Mama huyo alisema kwa furaha "Ni wakati wa furaha kabisa nilipopewa nyumba. Mtaa huu mpya ni mzuri sana, kuna nyasi, miti na maua. Sasa ninakaa kwenye nyumba ya ghorofa."
Badala ya nyumba ndogo ya muda, nyumba mpya ya Bibi Wen Chunli ina eneo la mita za mraba zaidi ya 60. Imefahamika kuwa, ili kuboresha mazingira ya kimsingi ya kuishi, kamati ya ujenzi ya mji wa Changchun imeamua eneo la nyumba mpya lisipungue mita za mraba 49. Wakazi walioishi kwenye nyumba za muda wanatakiwa kulipa tu gharama za eneo la nyongeza zaidi kuliko eneo la nyumba walizokuwa nazo hapo awali, na serikali inawatoza theluthi ya gharama za ujenzi. Na serikali inazilipa kampuni za ujenzi sehemu nyingine ya gharama.
Hivi sasa mkazi mwingine Bw. Li Yongchun anasubiri kwa hamu kuhamia kwenye nyumba mpya. Alisema "Taarifa inasema nitaweza kuhamia kwenye nyumba mpya tarehe 30 Oktoba mwaka 2008. Wakati huo kutakuwa na kiwanja cha nyasi, nyumba yenyewe itakuwa tayari, nitakuwa nimetimiza umri wa miaka 60 na kuishi siku za uzee kwa raha mustarehe."
Wakazi wengi walioamua kuendelea kuishi katika mitaa ya nyumba za muda baada ya mitaa hiyo kufanyiwa ukarabati wanatoka kwenye familia zenye mapato ya chini. Ili wakazi hao wamudu gharama za kuishi katika nyumba za kisasa, katika mitaa hiyo pia zilijengwa nyumba za kupanga kwa ajili ya shughuli za kibiashara, ambapo mkopo huo utatumika kulipa sehemu ya gharama za utendaji wa shughuli za umma ndani ya mtaa huo wa makazi, mbali na hayo utendaji wa shughuli hizo umeleta nafasi za ajira kwa wakazi wa mtaani.
Waziri wa ujenzi wa China Bw. Wang Guangtao alitembelea mtaa huo wa makazi, na yeye mwenyewe aliwakabidhi wakazi wa huko funguo za nyumba mpya. Bw. Wang alisema "Tunaowafuatilia ni wanyonge na siyo matajiri. Serikali ina nia ya kutatua suala la makazi linalowakabili wananchi wenye matatizo ya kiuchumi, hii ni kwa ajili ya kulinda usawa wa jamii."
Imefahamika kuwa serikali ya mkoa wa Jilin ilipanga kukamilisha shughuli za ukarabati wa maeneo ya nyumba za muda ndani ya miaka mitatu, na hivi sasa mpango huo utaweza kukamilika mwaka huu kabla ya muda uliowekwa. Zaidi ya hayo mkoa huo umetunga mpango wa mwaka 2008 unaohusu mambo ya makazi, ukiamua kujenga nyumba nyingi za kupanga kwa bei yenye unafuu ili watu wote wenye matatizo ya kiuchumi wapate nyumba za kuishi, vile vile serikali ya mkoa huo itatoa msaada kwa wakulima kukarabati nyumba zilizojengwa kwa udongo.
|