"Nilipokuja kufanya kazi hapa mkoani Guizhou, ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuja China. Kabla ya kuja China, marafiki zangu wengi walinielezea habari kuhusu China, na nilitafuta habari nyingi kuhusu China na mkoa wa Guizhou kwenye mtandao wa Internet na vitabu. Baada ya kuja hapa, sasa nafahamu mambo mengi kuhusu mkoa huo, na ninafurahi sana kupata fursa ya kufanya kazi hapa."
Tarehe 21 mwezi Mei mwaka huu ni siku muhimu kwa Bw. Kamal Sanusi anayetoka Malaysia. Hoteli ya Guihang ya kampuni ya Sheraton ilifunguliwa rasmi siku hiyo mjini Guiyang, ambao ni mji mkuu wa mkoa wa Guizhou. Kampuni ya Sheraton ya Marekani imeanzisha hoteli 34 nchini China. Baada ya kufanya ukaguzi, kampuni hiyo iliamua kumteua Bw. Kamal Sanusi kuwa naibu meneja mkuu na msimamizi mkuu wa shughuli za vyumba vya hoteli ya Guihang. Bw. Sanusi alisema,
"Napenda sana mkoa wa Guizhou, hasa mji wa Guiyang. Nilipofika hapa nilipenda mazingira ya mji huu. Watu wengi wanafanya kazi mjini humo, magari mengi yanakwenda barabarani. Mandhari ni nzuri wakati wa usiku, vyakula ni vingi, hasa jioni naweza kununua vyakula vingi vya kipekee."
Mkoa wa Guizhou unasifiwa kuwa sehemu yenye maelfu ya milima na mamia ya maporomoko ya maji. Mazingira ya kimaumbile na utamaduni wa makabila madogomadogo vimemfanya Bw. Sanusi aupende mkoa huo, alisema,
"Niliwahi kutembelea maporomoko ya maji ya Huangguoshu na mto Shamu ulioko kusini mashariki mwa mkoa huo, pia niliwahi kutembelea vijiji vya makabila ya Wamiao na Wadong. Nimejua mambo mengi kuhusu mji wa Guiyang. Napenda kutembea barabarani jioni, pia napenda kutembelea sehemu kando ya mji huo. Naupenda sana mji huu."
Mji wa Guiyang unasifiwa kuwa mji wa misitu na mahali pazuri kwa kukwepa joto katika majira ya joto. Lakini Bw. Sanusi ameona mengi zaidi kuhusu mji huo, alisema,
"Watu wa makabila mengi madogomadogo wakiwemo Wamiao na Wadong wanaishi hapa mkoani Guizhou. Makabila hayo madogo madogo yameupatia mkoa huo nguvu ya uhai, tunaweza kuona utamaduni tofauti kutoka kwa watu wa makabila hayo, na kujifunza kutoka kwa watu hao. Aidha utamaduni wa vyakula wa makabila madogomadogo pia ni wa kuvutia. Kwa mfano mji wa Kaili ulioko kusini mashariki mwa mkoa huo ni mji wenye sifa ya kipekee. Nitawaambia marafiki zangu waende kutalii huko, na kujionea utamaduni mbalimbali mkoani Guizhou."
Ni kweli watu wa makabila madogo madogo wanachukua theluthi moja ya watu wote wa mkoa wa Guizhou. Wao wanaishi pamoja kwa amani na masikilizano na kwa upendo. Bw. Sanusi alisema,
"Ninawapenda sana watu wa Guizhou, ninapoomba msaada, watu wengi hunisaidia, hata wakiwa na kazi nyingi, watanisaidia baada ya kumaliza kazi zao. Nchini kwetu watu wengi wanaona kuwa ni vigumu kujifunza kichina, na wao wana kazi nyingi, hawana wakati wa kuwasaidia watu wengine. Lakini hapa watu wengi wananisaidia kujifunza kichina na kuzoea vyakula vya hapa. Nafikiri watu wa Guizhou ni wakarimu na wenye moyo wa kirafiki."
Hoteli ya Guihang ya kampuni ya Sheraton iko katikati ya mji wa Guiyang. Iko karibu na kituo cha garimoshi na uwanja wa ndege wa Guiyang. Bw. Sanusi alisema,
"Hoteli yetu ikiwa ni hoteli kubwa ya kwanza ya kimataifa mkoani Guizhou, ni lazima tufuate hali ya hapa, na tuwe na mtindo wa kipekee wa hapa. Tunatoa huduma za aina mpya, ili kuanzisha chapa maarufu."
Katika miaka ya karibuni, mkoa wa Guizhou ulifanya juhudi kuendeleza shughuli ya utalii. Mwaka jana mkoa huo ulipokea watalii zaidi ya milioni 47, na mapato ya shughuli za utalii yalifikia Yuan bilioni 38.7. Bw. Sanusi alisema,
"Habari hizo ni nzuri kwa mkoa wa Guizhou, mji wa Guiyang na hoteli ya Sheraton. Watu wengi wanakuja hapa kufanya utalii na kununua vitu, na wameupatia mkoa huu fursa nzuri, lakini tunatakiwa kufikiri njia ya kutumia fursa hii ili kuendeleza mkoa huu."
Kutokana na maendeleo ya shughuli za utalii, hoteli za ngazi ya juu zimeanzishwa mkoani Guizhou. Lakini katika mkoa huo ambao uko nyuma kiuchumi, kuhakikisha kuwavutia watu wa kutosha kukaa hotelini bado ni kazi ngumu kwa Bw. Sanusi, alisema,
"Kutokana na gharama kubwa katika hoteli yetu, kuhakikisha kuwavutia watu wa kutosha kukaa hotelini bado ni changamoto. Watu wa Guizhou wametupa moyo, na wafanyabiashara na idara za serikali ya hapa zimetupatia uungaji mkono."
Ingawa kuna matatizo, Bw. Sanusi ana imani kubwa kuhusu maendeleo ya hoteli yao, alisema,
"Zamani watu walikuwa wanaona kuwa mkoa huo hauna maendeleo, lakini baada ya kufungua mlango, watu wenye ujuzi wanakuja hapa, hata wafanyabiashara wa nje wanakuja hapa. Nilipofika hapa, niliona kuwa maendeleo ya hapa ni ya haraka. Biashara imepata maendeleo ya kasi, na maendeleo ya shughuli nyingi zikiwemo upashanaji habari, magari na mikahawa yote yameonesha maendeleo makubwa ya mkoa huu. Nafiriki maendeleo hayo makubwa yataendelezwa katika muda mrefu ujao."
Idara ya utalii ya China inatarajia kuwa, soko la utalii la China litastawi ifikapo mwaka 2015. Mkoa wa Guizhou una raslimali nyingi za utalii, Bw. Sanusi alisema,
"Sijui kama kampuni yetu itaanzisha hoteli katika miji mingine mkoani Guizhou. Hivi sasa kampuni yetu inaangalia uwezekano mijini Beijing na Shanghai. Licha ya kampuni yetu ya Sheraton, makampuni mengine ambayo ni matawi ya kampuni ya Starwood yakiwemo kampuni Westin, Four Points na Le Meridien huenda yataanzisha hoteli mkoani Guizhou."
Hivi sasa Bw. Sanusi amefanya kazi mjini Guiyang kwa miezi kadhaa. Anaona kuwa Guizhou ni sehemu ambayo watu wanasaidiana, na ni mahali pazuri kwa kuishi na kufanya kazi. Ukimwuliza mkoa wa Guizhou una uzuri gani, atakuambia kwa kichina akisema,
"Mandhari ya Guizhou ni nzuri! Hali ya hewa ni nzuri, watu wa Guizhou ni wenye moyo wa kirafiki!"
Idhaa ya kiswahili 2008-01-15
|