Karibuni katika kipindi hiki cha daraja la urafiki kati ya China na Afrika, leo katika kipindi hiki tunawaletea mahojiano kati ya mwandishi wetu wa habari na Bibi Deng Bier, daktari mmoja wa China anayependa bara la Afrika. Tangu mwaka 1963 kikundi cha kwanza cha madaktari na wauguzi wa China kilipowasili barani Afrika, katika miaka 45 iliyopita, vikundi vya madaktari na wauguzi wa China viliendelea kutoa misaada ya matibabu katika nchi na sehemu mbalimbali barani Afrika, ujuzi, uhodari na maadili ya madaktari wa China yanasifiwa sana na serikali za nchi za Afrika na wananchi wao. Wakati huo huo, muda waliokuwepo madaktari wa China barani Afrika pia umekuwa ni kumbukumbu zao nzuri.
Bi. Deng Bier mwenye umri wa miaka 69 aliwahi kuwa kiongozi wa kwanza mwanamke wa kikundi cha madaktari cha China katika historia ya kutoa misaada ya matibabu kwa China nchini Morocco. Mwaka 1987 Bi. Deng aliyekuwa na umri wa miaka 48, aliongoza kikundi cha madaktari wa China kwenda nchini Morocco, nchi ya Afrika ya kaskazini. Ingawa ni miaka 21 imepita sasa, lakini hivi sasa Bi. Deng bado anakumbuka wazi hali ya wakati ule, alisema,
"Zamani Morocco iliwaalika madaktari kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Russia, lakini baadaye wamorroco waliona kuwa madaktari wa China wanafanya juhudi zaidi kuliko madaktari wa nchi nyingine. Hivyo Morocco ilipunguza hatua kwa hatua idadi ya madaktari wa nchi nyingine, na kuwaalika madaktari wa China tu. Wakati nilipokwenda Morocco, kulikuwa na vikundi sita vya madaktari wa China nchini Morocco, ambavyo vilikuwa vinatoa huduma za matibabu kwenye sehemu mbalimbali nchini humo."
Bi. Deng alijulisha kuwa katika miaka ya 70 karne iliyopita, Morocco ilikuwa na madaktari wenyeji wachache sana, iliwaalika madaktari kutoka nchi nyingine za nje. Mwaka 1975 China na Morocco zilianzisha ushirikiano wa matibabu, na hospitali ya chuo kikuu cha pili cha matibabu cha China mjini Shanghai ilituma kikundi cha kwanza cha madaktari nchini Morocco. Ingawa madaktari walikuwa wanakabiliana na mazingira magumu barani Afrika, lakini madaktari waliotumwa nchini Morocco bado walikamilisha vizuri majukumu yao, na kusifiwa na wananchi wa huko. Hali hii iliweka msingi mzuri kwa ushirikiano wa matibabu kati ya nchi hizo mbili katika siku za baadaye. Tangu hapo chuo kikuu cha pili cha matibabu cha China kilituma vikundi vya madaktari nchini Morocco, kila baada ya miaka miwili. Kikundi cha madaktari kilichoongozwa na Bi. Deng kilitumwa kwenye hospitali ya Hassan II mjini Agadir. Bi. Deng alisema,
" Kikundi chetu kiliundwa na wachina 14, mmoja ni mkrimani, mmoja ni mpishi, na wengine 12 ni madaktari."
Walipowasili nchini Morocco, Bi. Deng na wenzake walianza kazi zao katika hospitali. Walitambua kuwa kulikuwa na magonjwa mengi yanayowakabili watu barani Afrika, kuliko yale ya nchini China. Bi. Deng alisema,
"Kulikuwa na magonjwa mbalimbali ya maambukizi. Kabla ya kwenda Morocco, ingawa nilikuwa nimefanya kazi nchini China kwa miaka zaidi ya 20, lakini nilifahamu magonjwa mengi kwa njia ya vitabu au masomo tu, sikuwahi kuona watu wanaoumwa magonjwa hayo. Lakini baada ya kuwasili Afrika, nilikutana na watu wenye magonjwa hayo yote. "
Hospitali ya Hassan II ya wakati ule ilikuwa na vitanda zaidi ya 200 vya wagonjwa, na wauguzi wote walikuwa ni wamorocco. Madaktari wa China walikuwa wanashughulikia kupokea na kutibu wagonjwa, na kufanya operesheni. Bi. Deng alisema,
"Wagonjwa wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuja kwenye hospitali tuliyokuwa tunafanya kazi, asubuhi na mapema ya kila siku kulikuwa na wamorocoo wengi waliokuwa wamevaa mavazi ya kiarabu waliokuwa wanatusubiri. Baada ya kufanya upimaji kuhusu wagonjwa hospitalini, tulipokea madaktari waliokuwa wanasubiri. Kila siku tulifanya kazi mchana na usiku, pia hatukuwa na mapumziko ya wikiendi"
Madaktari wa China waliwatibu wagonjwa wa huko, waliheshimiwa na kusifiwa na watu wa huko. Wagonjwa wengi walimwita Bi. Deng kuwa "Mama". Wagonjwa wengi walitaka kuwashukuru madaktari wa China kwa kuwapa zawadi, lakini madaktari wa China walikataa. Bi. Deng alisema,
"Wagonjwa wengi walifurahi sana baada ya kutibiwa kwenye hospitali yetu. Waliwaalika madaktari wote wa kikundi chetu nyumbani kwao, walitaka kutupa zawadi lakini tulikataa, tuliwaambia kuwa sisi madaktari wa China hatupokei zawadi za wagonjwa."
Katika kipindi cha miaka miwili nchini Morocco, madaktari wa China si kama tu walijenga uhusiano wa kirafiki na wagonjwa, bali pia walijenga urafiki na wauguzi wa Morocco. Bi. Deng alipiga soga mara kwa mara na wauguzi wakati wa mapumziko, ili kuzidisha maelewano kati yao, pia Bi. Deng aliongeza uwezo wake wa kuongea kwa lugha ya Kifaransa kwa kupitia mazungumzo na wauguzi, hii ilimsaidia kufanya mawasiliano vizuri zaidi na wagonjwa. Hata baada ya Bi. Deng kurudi nchini China, wauguzi wengi wa Morocco bado walimwandikia barua Bi. Deng mara kwa mara, na kuonesha upendo wao kwake. Wakati muda wa kikundi hicho ulipokwisha, mkurugenzi wa idara ya afya ya huko alimtaka Bi. Deng abaki nchini Morocco, hata alimwalika mume wa Bi. Deng kwenda Morocco pia.
Baada ya kurudi nchini China, kila aliposoma habari kuhusu Afrika hasa Morocco, Bi. Deng alifurahi kufuatilia. Bi. Deng alisema, katika miaka ya hivi karibuni, uhusiano kati ya China na Afrika uliendelezwa kwa kasi, wakati alipokumbuka kuwa aliwahi kushiriki kwenye ujenzi wa urafiki kati ya China na Afrika, yeye aliona fahari sana. Baada ya kustaafu, Bi. Deng alitembelea nchi nyingi zikiwemo Russia, Korea ya Kaskazini na Canada. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika siku za baadaye atakwenda kutalii barani Afrika, na anapenda kurudi nchini Morocco ili aonane na marafiki zake wa zamani. Akisema,
"Kama nitakaporudi nchini Morocco, hakika watu wengi watakuwa wananifahamu. Kwa kuwa wachina wengi waliorudi nchini China kutoka Morocco waliniambia kuwa, wamorocco wengi waliwaonesha picha yangu na kuwataka wanisalimu. Naipenda sana Morocco na wananchi wake, ingawa katika miaka miwili hiyo, nilikuwa niko mbali na familia yangu, pia nilikabiliana na matatizo mengi, lakini bado niliona kipindi hicho kinastahili kwangu."
Idhaa ya kiswahili 2008-01-25
|