Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-23 15:12:53    
Serikali ya mji wa Wulumuqi yawasaidia watu wa makabila madogo madogo kupata ajira

cri
Mkoa unaojiendesha wa kabila la Wauyghur wa Xinjiang uko kwenye mpaka wa kaskazini magharibi nchini China. Kwenye mkoa huo kuna watu wa makabila 46 madogo madogo. Kutokana na sababu mbalimbali, hali ya kupata ajira kwa watu hao si nzuri. Ili kuwasaidia kuondoa tatizo la ajira, katika miaka ya hivi karibuni serikali ya mji wa Wulumuqi imechukua hatua nyingi, na hatua hizo sasa zimeanza kuonesha mafanikio.

Robo moja ya idadi ya wakazi wa makabila madogo madogo wa mji wa Wulumuqi wanaishi kwenye mtaa wa Tianshan wa mji huo, kutokana na sababu mbalimbali hasa matatizo ya lugha, watu hao wanakabiliwa na tatizo kubwa katika kupata ajira. Mkurugenzi wa kituo cha usimamizi wa mambo ya ajira cha mtaa wa Tianshan Bw. Wang Long alisema,

"Watu wa makabila madogo madogo wanakabiliwa na tatizo kubwa zaidi la ajira kuliko watu wa kabila la Wahan. Hali hiyo hasa inatokana na lugha, lugha ya pamoja inayotumika mjini Wulumuqi ni lugha ya kabila la Wahan yaani lugha ya kichina, lakini watu wengi wa makabila madogo madogo wanajua lugha za makabila yao tu. Aidha baadhi ya watu hawajapata elimu ya kutosha."

Ili kuondoa tatizo la ajira kwa ajili ya watu wa makabila madogo madogo, idara ya ajira ya serikali ya mtaa wa Tianshan ilichukua hatua za upendeleo kwa watu hao. Kati ya hatua hizo, kuwafundisha ufundi wa kazi kunatiliwa mkazo zaidi. Takwimu zinaonesha kuwa tangu hatua hizo zianze kutekelezwa, kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Novemba mwaka jana, watu karibu 3100 wa makabila madogo madogo wa mtaa huo wamepata ajira, miongoni mwao watu 1900 walipata ajira baada ya kupewa mafunzo ya ufundi wa kazi. Hasi Yeti ni msichana wa kabila la Wauyghur anayeishi kwenye mtaa wa Tianshan. Baada ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari, hakupata ajira kwa miaka kadhaa. Hatimaye alishiriki kwenye semina iliyoandaliwa na serikali na kujifunza ufundi wa ushonaji kwa miezi sita, na mwanzoni mwa mwaka jana, alipata kazi ya ushonaji akisaidiwa na idara ya huduma ya ajira ya mtaa wa Tianshan. Sasa anaweza kuendesha maisha bila kutegemea ruzuku ya serikali. Hasi Yeti alisema,

"Baada ya kuhitimu kutoka shule ya sekondari sikuweza kupata ajira, wakati huo idara ya huduma za jamii ya mtaa wetu iliniandikisha kwenye orodha ya watu wanaotafuta kazi, na ilinisaidia kupata mafunzo ya ufundi wa kazi. Nilijifunza ufundi wa ushonaji kwenye kituo cha semina, na sasa nimepata ajira na ninaweza kupata mapato ya yuan mia tano kwa mwezi. Maisha yangu yameboreshwa sana."

Kituo cha semina za ufundi wa kazi pia kilitoa huduma za kutoa mafunzo kwa watu nyumbani. Kwa mfano wafanyakazi wa kituo hicho walikwenda kwenye kijiji cha Wulabo na maeneo ya ufugaji wanapoishi watu wa kabila la Wakazakh kuwafundisha ufundi wa kuendesha mikahawa. Mkurugenzi wa kituo cha semina za ufundi wa kazi Bw. Wang Long alisema,

"Kwa kufuata umaalumu wa makazi yao, watu wa kijiji hicho wanafaa kushughulikia mikahawa kwa ajili ya watu wanaofanya utalii kijijini, hivyo tuliwaandalia semina ya kuwafundisha elimu kuhusu shughuli hiyo kwenye kijiji chao."

Serikali ya mtaa wa Tianshan inaandaa semina za aina mbalimbali, mbali na mikahawa na ushonaji, ufundi wa uendeshaji wa magari, kompyuta na hesabu pia zinafundishwa kwenye semina hizo. Bw. Wang Long alisema,

"Watu wa makabila madogo madogo wanaweza kuchagua semina za ufundi wa kazi mbalimbali kama wanavyopenda. Baada ya kumaliza masomo kwenye semina hizo, watapewa hati za ufundi wa kazi mbalimbali, halafu wanaweza kupata ajira kwa msaada wa idara zinazohusika za serikali."

Mbali na mtaa wa Tianshan, mitaa na wilaya nyingine za mji wa Wulumuqi pia zinatekeleza sera za ajira za upendeleo kwa watu wa makabila madogo madogo. Mji wa Wulumuqi pia unatekeleza sera ya kuandikisha watu wasio na ajira kila mwezi, yaani kuwatuma wafanyakazi wa idara ya ajira ya serikali kuandishisha watu wasio na ajira kila mwezi, halafu kuwasaidia kupata ajira.

Aidha idara ya huduma za kazi ya mji wa Wulumuqi imechukua hatua mbalimbali ili kuwasaidia watu wa makabila madogo madogo kupata ajira, hatua hizo ni pamoja na kuongeza nafasi za ajira, na kuwahakikishia watu wa makabila madogo madogo wanapata nafasi mpya ya ajira. Mkuu wa idara hiyo bibi Zhu Wenzhi alisema,

"Kuendeleza uchumi kwenye sehemu za makabila madogo madogo ni hatua nzuri zaidi ya kuongeza ajira kwa watu wa makabila hayo. Tunaweza kuwasaidia watu hao kupata ajira katika sehemu za vivutio vya utalii na maduka. Wakati tunapoendeleza uchumi tunaongeza nafasi za ajira kwa ajili ya watu wa makabila madogo madogo."

Baada ya kutelelezwa kwa hatua hizo, tangu mwaka 2001 hadi mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka 2007, mji wa Wulumuqi uliwasaidia watu zaidi ya elfu 72 wa makabila madogo madogo, na watu hao wanachukua asilimia 23 ya watu wote waliopata ajira katika muda huo. Sera ya upendeleo ya ajira inawafurahisha sana watu wasio na ajira wa makabila madogo madogo.

Idhaa ya kiswahili 2008-01-23