Kwenye tamasha la vitabu lililofanyika hivi karibuni mjini Beijing, biashara ya haki ya kunakili ilifana sana. Kwenye tamasha hilo wachapishaji kutoka nchini na nchi za nje walipata fursa nzuri ya kufanya ushirikiano na biashara ya haki ya kunakili.
Hili ni tamasha ambalo linafanyika kila mwaka mjini Beijing, moja ya shughuli zinazofanyika katika tamasha hilo ni biashara ya haki ya kunakili, wachapishaji wengi walishiriki kwa hamu kubwa kwenye tamasha hilo. Mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa haki ya kunakili katika Idara ya Usimamizi wa Haki ya Kunakili ya China Duan Yuping alisema,
"Mwaka 1990 sheria ya haki ya kunakili ya Jamhuri ya Watu wa China ilitangazwa rasmi na ilianza kutekelezwa tarehe mosi Juni mwaka 1991. Mwaka 1992 China ilianza kutekeleza sheria ya kimataifa ya haki ya kunakili, biashara ya haki ya kunakili nchini China inatakiwa kuheshimu sheria zote hizo mbili."
Kampuni kuu ya uwakala wa haki ya kunakili ni chombo kikubwa cha kushughulikia biashara ya haki ya kunakili nchini China. Katika miaka ya hivi karibuni kampuni hiyo ilikuwa na shughuli nyingi za biashara ya haki ya kunakili kati ya China na nchi za nje. Kwenye siku za tamasha hilo, kampuni hiyo ilisaini na Japan mkataba wa ushirikiano wa kimkakati. Pande mbili zitashirikiana katika juhudi za kuviwezesha vitabu vya upande mmoja kuingia kwenye soko la vitabu la upande wa pili, na zitaanzisha utaratibu wa kufanyiana matamasha ya vitabu na kutembeleana.
Kwenye tamasha hilo, Shirika la Uchapishaji la Vitabu kuhusu Sherila la China lilisaini mkataba na Shirika la Sayansi la Japan kuhusu kuchapisha na kusambaza nchini Japani kitabu kiitwacho "Fikra za Yu Dan baada ya Kusoma Kitabu cha Zhuang Zi". Kwenye kitabu hicho Bi. Yu Dan kwa mtazamo wa zama hizi amefafanua fikra za Zhuang Zi, mwanafalsafa aliyeishi kati ya mwaka 369 K.K. na 286 K.K., hasa kuhusu makala yake ya "Utalii wa Starehe", Bi. Yu Dan alisema, kila mtu ana matumaini kuwa maisha yake yatakuwa ya furaha katika miaka yote ya uhai wake, lakini anayeweza kujitambua tu ndiye anayeweza kufanikiwa. Lakini ni vigumu sana kujitambua namna alivyo. Mhariri mkuu wa Shirika la Sayansi la Japan Eiichi Satomura alipozungumzia ununuzi wa haki ya kunakili ya kitabu cha "Fikra za Yu Dan baada ya Kusoma Kitabu cha Zhuang Zi" alisema,
"Hivi leo watu wanakuwa wanachoka sana kutokana na shinikizo la kazi nyingi, hawataki kusoma vitabu ambavyo si rahisi kuvielewa kwa kina. Bi. Yu Dan ametupatia njia ya mkato, ametuwezesha kufahamu utamaduni wa kale wa China, hii ndio sababu yetu ya kununua haki ya kunakili ya kitabu cha Yu Dan. Sisi Wajapani tunampenda Bibi Yu Dan kwa sababu ametufahamisha utamaduni wa kale ulioandikwa kwa maneno magumu na kutuwezesha kuufuata katika maisha yetu. Hivi leo Wajapan hawana wakati wa kusoma vitabu vya kale ambavyo ni vigumu kwao kuelewa."
Kwenye tamasha hilo, kitabu cha "China kwa Ufupi" kilichotafsiriwa kwa lugha 11 kiliwavutia wachapishaji wengi wa nchi za nje. Baada ya kitabu hicho kuchapishwa kwa Kiingereza mwaka 2005 kilisomwa sana katika nchi za Magharibi. Mwaka 2007 Shirika la Uchapishaji la Bertelsmann lilichapisha kitabu hicho kwa lugha ya Kirusi, kisha mashirika ya nchi za Korea ya Kusini, Jamhuri ya Mongolia na Lebanon pia yalichapisha. Hivi sasa haki ya kunakili ya kitabu hicho inatazamiwa kununuliwa na mashirika ya nchi za Hispania, Italia, Ufaransa, Hungary, Czech na Poland. Mwandishi wa kitabu hicho Bw. Su Shuyang alisema,
"Hiki ni kitabu kinachoeleza kwa ufupi utamaduni wa jadi wa China tokea miaka elfu kadhaa iliyopita hadi leo. Kaulimbiu ya Shirika la Ushapishaji la Bertelsmann ni 'kwenda China baada ya kusoma vitabu kadhaa vya China", linaona kuwa kitabu hiki ni kizuri kuwafahamisha wasomaji China ilivyo. Hapo awali niliandika kitabu hicho kwa ajili ya vijana wa China."
Bw. Su Shuyang alipozungumzia fikra zake za kuchagua maudhui ya kuwaandikia wasomaji wa nchi za nje alisema, mwandishi ni lazima ajiwekee kwenye nafasi sawa na wasomaji na kuwasiliana na kujadiliana nao, na kueleza fikra kutoka pande zote kuhusu jambo linalowavutia wasomaji, na mwandishi ni lazima asimame kwenye kilele cha historia na kutupia macho kwenye historia yote ya China ili kugundua tabia na sifa zake, huku akiiweka historia ya China kwenye historia ya dunia."
Tamasha hilo lilipendekeza miswada ya vitabu 336 na kusambazwa kwa wachapishaji wote bila malipo. Tamasha hilo pia limeweka ofisi ya maulizo kuhusu sheria ya haki ya kunakili na kupokea miswada ya vitabu.
Tamasha la vitabu liliwahi kufanywa mara kadhaa, lakini shughuli za biashara ya haki ya kunakili zilianzishwa mwaka juzi tu. Kwenye tamasha la mwaka huu, waandishi wa vitabu na wachapishaji wamekubaliana kimsingi kuchapisha vitabu zaidi ya 100 kuchapishwa.
Imefahamika kwamba licha ya kampuni kuu ya uwakala wa haki ya kunakili nchini China, pia kuna idara zaidi ya 20 za uwakala wa haki ya kunakili mikoani. Pamoja na hayo baadhi ya mashirika ya uchapishaji na idara za utamaduni pia yanafanya biashara hiyo. Biashara ya haki ya kunakili imeharakisha maendeleo ya uchapishaji nchini China, na pia imestawisha biashara ya haki ya kunakili na nchi za nje.
Idhaa ya kiswahili 2008-01-28
|