Kabila la Wajing ni kabila dogo nchini China, idadi ya watu wa kabila hilo ni karibu elfu 20. Watu hao wanaishi kwenye visiwa vitatu vya Wanwei, Wutou na Shanxin vilivyoko kusini mwa China. Leo tutawaletea maelezo kuhusu maisha mapya ya watu wa kabila la Wajing wanaoishi kwenye kijiji cha Wanwei.
Kijiji cha Wanwei kiko kwenye pembe ya kusini mwa visiwa vitatu vya kabila la Wajing. Kwenye kijiji hicho, nyumba nzuri zenye gorofa za wakazi zilijengwa kwenye kando mbili za barabara, hata mbele ya nyumba nyingi, kuna magari madogo mapya yaliyoegeshwa. Kwenye kijiji hicho kuna mawasiliano mazuri ya barabara, malori yanasafirisha samaki kutengenezwa kwenye viwanda mjini. Ofisa wa kijiji cha Wanwei Bw. Li Mingfang aliwaambia waandishi wetu wa habari kuwa, miaka zaidi ya 30 iliyopita hiki ilikuwa kijiji cha wavuvi kilichokuwa nyuma kimaendeleo, wanakijiji walimudu maisha yao kwa kutegemea uvuvi wa samaki baharini. Kutokana na kuwa na magadi mengi, ardhi ya kijiji cha Wanwei haifai kwa kilimo. Ili kupata nafaka, wakazi wa kijiji hicho walilazimika kuwatafuta wakulima wa sehemu za milimani ili kubadilisha nafaka kwa samaki. Bw. Su Mingfang alisema,
"Wakati huo tulikumbwa na taabu kubwa za mawasiliano ya barabara, tuliweza tu kutoka nje baada ya maji ya bahari kupwa."
Bw. Su Mingfang alisema katika miaka ya 60 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianzisha mradi wa kuzuia maji ya bahari, na kuunganisha visiwa vitatu vya Wanwei, Wutou na Shanxin na bara kuu, ili kuongeza mashamba ya kilimo kwa mara moja. Baada ya hapo sera ya mageuzi na kufungua mlango ilileta hali mpya katika visiwa hivyo. Kwa kutumia fursa ya kurejeshwa kwa biashara kati ya sehemu za mpakani za China na Vitnam na kuwepo kwa sera ya upendeleo kwa makabila madogo madogo, watu wa kijiji cha Wanwei walianza kushughulikia ufugaji wa samaki na utengenezaji wa mazao ya baharini, ambapo wanakijiji wengine waliojua lugha ya KivitNam walianzisha biashara mpakani. Aidha watu wa kabila la Wajing walijishughulisha na mambo ya utalii kwa kutumia umaalumu wa utamaduni wa kabila hilo. Kwa mfano desturi za kuimba za kabila hilo ya "Changha" sasa inawafurahisha zaidi watalii.
Wapendwa wasikilizaji, sauti mlikosikia ni ya watu wa kabila la Wajing wakiimba wimbo yaani "Changha". Watu wa kabila hilo ni hodari katika kucheza ngoma na kuimba nyimbo, wanafanya sherehe ya Changha kila baada ya siku kumi. Siku ya sherehe hiyo, watu huvaa nguo nzuri na kukusanyika kwenye sehemu maalumu, wanacheza ngoma na kuimba. Bw. Li Mingfang alisema Changha ni sherehe muhimu zaidi ya watu wa kabila la Wajing. Alisema,
"Sherehe hiyo inafanyika mara tatu katika siku za tarehe 10, tarehe 20 na tarehe 30 kila mwezi. Watu kutoka kijiji cha Wanwei na vijiji vingine, na hata wachina wanaoishi nchi za nje ambao wanarudi kuwatembelea jamaa zao wana hamu kubwa ya kushiriki kwenye sherehe hiyo."
Shughuli za biashara na utalii zimebadilisha maisha ya watu wa kabila la Wajing. Bw. Zheng Xianfang mwenye umri wa miaka 64 ni mkazi wa kijiji cha Wanwei, alipozungumzia maisha yake ya sasa alisema,
"Maisha yetu yanaboreshwa siku hadi siku, kuna nyumba nzuri nyingi zenye gorofa katika kijiji chetu, na hata watu wengi wamenunua magari madogo. Kwa mfano familia yangu ina watu sita, tuna nyumba ya ghorafa , gari la kifahari, pikipiki mbili na baiskeli tatu. Zamani hatukuwa na vitu hivyo vyote."
Zamani watu wa kabila la Wajing waliishi katika nyumba zilizojengwa kwa kutumia nyasi na matope, lakini hivi sasa asilimia 90 ya familia kwenye kijiji cha Wanwei zinaishi katika nyumba nzuri za ghorofa zilizojengwa kwa nondo na saruji, na kila familia ina televisheni. Wakazi wa kijiji hicho wana simu zaidi ya 2,000 za mkononi, na vijana wanaweza kutumia mtandao wa Internet nyumbani.
Serikali ya kijiji cha Wanwei ilichukua hatua mbalimbali Ili kuongoza mambo ya burudani kwa wanakijiji hao, Bw. Su Mingfang alisema,
"Wanakijiji wetu wamekuwa na uwezo, tunataka kuwasaidia wazee wa kijiji chetu waishi kwa furaha zaidi, kwa kuwa wakiishi furaha, watoto wao watafanya kazi kwa bidii zaidi. Mwaka jana tulipanga wazee zaidi ya 20 wa kijiji chetu kutembelea mji wa Beijing ili wajionee hali ya mji mkuu wa nchi yetu. Walifurahi sana baada ya kurudi. Sasa tunapanga kuwapeleka wazee wengine kutalii mjini Beijing."
Mwezi Julai mwaka 2007, Bw. Zheng Xianfang alishiriki kwenye ujumbe wa watalii uliopangwa na serikali ya kijiji cha Wanwei, na kutembelea mji wa Beijing. Alipozungumzia safari hiyo alisema,
"Nimekuwa na umri wa miaka zaidi ya 60, sikuwa na matarajio ya kutalii mjini Beijing. Nilipokuwa mjini Beijing, nilipigiwa simu na kuambiwa kuwa baba yangu ananitaka nirudi nyumbani kwa kuwa anaumwa. Lakini baada ya kurudi nyumbani nilimwonesha picha nilizozipiga mjini Beijing, baba alifurahi sana."
Mwishoni mzee Zheng Xianfan alisema visiwa vitatu vya kabila la Wajing ni sehemu nzuri, kuna pwani yenye mchanga wa rangi ya dhahabu, misitu ya asili na mila maalumu za kabila la Wajing, na anawakaribisha marafiki wote duniani kwenda kutalii kwenye maskani yake.
Idhaa ya kiswahili 2008-01-30
|