Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-01-30 18:27:36    
Daktari wa matibabu ya jadi ya kichina kutoka Afrika Bw. Feilong

cri

Katika kipindi hiki tunawaletea maelezo kuhusu daktari mmoja wa matibabu ya jadi ya kichina kutoka Cameroon anayeitwa kwa kichina Bw. Feilong, ambaye sasa anafanya kazi kwenye hospitali ya kufufua uwezo kwa watu wenye ugonjwa wa kupooza kwa ubongo ya mji wa Taiyuan mkoani Shanxi.

Kwenye chumba kimoja cha matibabu cha hospitali hiyo, mwandishi wetu wa habari alimwona Bw. Feilong akiwapa wagonjwa watoto matibabu ya usingaji na akyupancha. Mtoto alipoona Bw. Feilong mara moja alianza kulia.

"anaogopa kudungwa sindano. Wanaogopa madaktari wote."

Katika hospitali hiyo watoto wengi wanamwita Bw. Feilong kuwa "mjomba mweusi". Huyo mjomba kutoka Cameroon alitumwa na serikali ya nchi hiyo kusomea shahada ya pili ya matibabu ya kufufua uwezo kwa watoto wenye matatizo ya mfumo wa neva katika chuo cha udaktari cha mkoa wa Shanxi, baada ya kuhitimu kutoka chuo hicho, aliendelea kufanya kazi za kujitolea katika hospitali hiyo. Bw. Fei Long mwenye umri wa miaka 32 alipofahamisha jina lake, alisema Fei inamaanisha Feizhou yaani Afrika, Long inamaanisha dragon yaani China. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa aliwahi kusomea udaktari alipokuwa nchini Cameroon. Bw. Fei Long alisema:

"nilipokuwa ninasoma katika chuo kikuu cha udaktari nchini Cameroon, nilianza kuvutiwa na mbinu za kimaumbile za matibabu. Katika upande huo, nadhani matibabu ya jadi ya kichina yameendelea vizuri kabisa. Naona kuwa matibabu ya akyupancha ni yenye ufanisi mkubwa. Lakini ni vigumu kuelewa nadharia na kanuni za matibabu hayo, hasa kwa wageni. Ingawa kuna vitabu vilivyotafsiriwa kwa Kiingereza, lakini bado ni vigumu kuvielewa."

Bw. Fei Long bado anakumbuka wazi hali ilivyokuwa wakati alipofika China kwa mara ya kwanza. Baada ya kushuka kwenye ndege, alivyoona vilimshangaza sana. Bw. Fei Long alisema:

"ilichukua muda wa zaidi ya saa moja kutoka uwanja wa ndege wa Beijing hadi kwenye hoteli niliyofikia. Nilikuwa nashangaa sana. Mji wa Beijing ni mkubwa mno na umeendelea sana. Nadhani asilimia 95 ya watu wanaotembelea China kwa mara ya kwanza watakuwa na hisia hiyo."

Baada ya kukaa kwa muda mfupi mjini Beijing, alikwenda Taiyuan mkoani Shanxi kwa ajili ya masomo ya shahada la pili kwenye chuo cha udaktari wa jadi ya kichina mjini humo. Wakati huo pia alianza kufanya kazi za kujitolea katika hospitali ya wagonjwa wa kupooza kwa ubongo ya mkoa huo. Mkurugenzi wa hospitali hiyo Bi. Guo Xinzhi alisema:

"mwanzoni wagonjwa walikuwa wanamwogopa, walikataa kupewa matibabu na 'mjomba yule mweusi', nikawaambia watoto hao kwamba huyo ni mtu mwema, wamruhusu awafanyie usingaji na wala wasiangalie uso wake."

Lakini baada ya muda mfupi, hali hiyo imebadilika. Bi. Guo Xinzhi alisema:

"kwa kuwa aliwafanyia usingaji kwa vitendo vya kawaida sana, watoto wakaanza kutaka yeye peke yake awape matibabu. Hivyo wagonjwa watoto wengi zaidi walitaka kupewa matibabu naye, hata alipaswa kurefusha muda wa kazi ili kukidhi mahitaji ya watoto hao."

Bw. Fei Long alisema: "nawapenda sana watoto hao, siwezi kuacha kazi kwa sababu ya kuchoka. Lazima nifanye juhudi kadri niwezavyo kuwatibu watoto hao."

Watoto wenye tatizo la kupooza kwa ubongo kwa kawaida wana matatizo katika akili na uwezo wa kufanya vitendo. Kwa hivyo matibabu ya kuwasaidia warejeshe afya ni kazi ya muda mrefu ambayo inahitaji uvumilivu mkubwa. Daktari Bw. Shi Xiaojie aliyefanya kazi pamoja na Bw. Fei Long alimsifu sana Bw. Fei Long, akisema:

"anafanya kazi kwa makini zaidi hata kuliko sisi. Pia ana upendo mkubwa kwa watoto hao wenye matatizo, na anapenda sana shughuli hizo."

Hivi sasa Bw. Fei Long anaona kuwa amezoea sana maisha ya huko na amekuwa kama mwenyeji wa Shanxi. Ameshuhudia mabadiliko makubwa ya mji huo, pia amefurahia sana mabadiliko hayo. Bw. Fei Long alisema:

"mji wa Taiyuan umekuwa tofauti kuliko zamani, barabara, majengo hata hali ya hewa imebadilika. Kama mtu alikuja Taiyuan mwaka 2003, akirudi mwaka 2007 au 2008 atasema huo ni mji mwingine kabisa, ni kama mji wa zamani umeondolewa na mpya kabisa umejengwa. "

Baada ya kazi na masomo, Bw. Fei Long anapenda kucheza Taiji na gongfu ya kichina. Maisha ya miaka minne nchini China yamekuwa na athari kubwa kwa mgeni huyo kutoka Afrika. Anatumai kuwa ataweza kuishi nchini China katika siku za baadaye. Bw. Fei Long alisema:

"naona nimebahatika kuwa na fursa ya kuishi nchini China kwa muda huo, kwa kuwa kila siku China inabadilika. Naweza kuishi pamoja na watu wa China pia naweza kuelewa maisha yao. Ni matumaini yangu kuwa nitaweza kuishi hapa kwa muda mrefu zaidi. Naupenda mji wa Shanxi, naipenda China. Ninatumai kuwa nitakuwa na familia nchini China, naichukulia China ni kuwa maskani yangu ya pili."

Bw. Fei Long alisema, anapenda kula tambi za kichina, pia ataweza kuongea kidogo lugha ya kienyeji ya Taiyuan. Moyoni mwake anaitakia China kila la heri.