Kwa maoni ya dada Mahire, kusafisha nyumba ni sehemu tu ya huduma zinazotolewa na kampuni yake, kwa hiyo kampuni hiyo inapaswa kuwa na wafanyakazi wenye sifa nzuri.
Baadaye Mahire alitoa matangazo ya nafasi za ajira kwenye magazeti, na kuwataka watakaoomba nafasi hizo wawe wahitimu wa vyuo vikuu. Ingawa dada Mahire mwenyewe alikuwa na shauku ya kujua kama vijana waliopata elimu ya juu watapenda kupata ajira ya kampuni ya huduma za nyumbani, hali isiyotarajiwa na bosi huyo ilitokea, vijana zaidi ya 10 waliohitimu vyuo vikuu walitoa maombi ya ajira.
Kijana Selkinur Asraf ni miongoni mwa wahitimu hao wa vyuo vikuu waliotoa maombi ya ajira. Hivi sasa kijana huyo anafanya kazi ya kupiga picha kwenye kampuni hiyo. Alielezea kuwa mbali na nafasi hiyo ya ajira, alikuwa anaweza kupata kazi ya ualimu katika shule moja ya sekondari. Lakini aliona anavutiwa zaidi na kazi anayofanya hivi sasa. Kijana Asraf alisema "Awali serikali ilibeba jukumu la kuwapa ajira wahitimu wa vyuo vikuu, manufaa yake ni kupewa ajira yenye pato la uhakika, lakini dosari yake ni kuwa vijana walishindwa kuchagua ajira wanazopenda. Ingawa hivi sasa kuna ushindani mkali sokoni, lakini tuna imani ya kutosha kukabiliana na ushindani."
Miaka zaidi ya 10 iliyopita vijana wa China wakimaliza masomo ya vyuo vikuu, walikuwa wanapewa kazi na serikali. Wakati huo ilikuwa hakuna mtu aliyesumbuliwa na tatizo la kukosa ajira, lakini kwa upande mwingine kama walipewa ajira wasioipenda hawakuwa na chaguo lingine ila tu kuikubali.
Tangu mwishoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianza kuwaacha vijana wahitimu wa vyuo vikuu wajitafutie ajira, hali ambayo inawapa vijana wenye tabia ya kuvutiwa na changamoto, kama dada Mahire na kijana Asraf fursa nyingi za kutimiza ndoto zao. Hivi sasa kila mwaka vijana zaidi ya milioni 4 wanahitimu kutoka kwenye vyuo vikuu mbalimbali nchini China, wanachagua ajira kutokana na uelekezaji wa vyuo vikuu.
Mkurugenzi wa ofisi ya ajira ya idara ya ajira na uhifadhi wa jamii katika mkoa unaojiendesha wa Xinjiang Uygur Bw. Xiao Ming alitoa ufafanuzi zaidi, akisema "Hivi sasa tunasisitiza kuwa, vijana wanaposoma kwenye vyuo vikuu, inapaswa kuongeza kuwapatia mafunzo kuhusu sera ya ajira na kuwapa uelekezaji wa ajira, ili wajenge mtizamo wa kujiamulia ajira na kufahamishwa hali ya soko la ajira. Hivi sasa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wamebadilisha mtizamo kuhusu ajira, wakimaliza masomo na kupata utaalamu fulani, wanapenda kuanzisha shughuli zao wenyewe."
Hivi sasa kuna waajiriwa 9 katika kampuni ya huduma za nyumbani ya dada Mahire, ambao wote ni wahitimu wa vyuo vikuu. Hii imethibitisha kuwa hatua hiyo ya Mahire imefanikiwa, kwani kampuni hiyo sasa inajulikana sana miongoni mwa wakazi wa huko kutokana na kuwa, watu wa kampuni hiyo ya huduma za nyumbani toka mkuu mpaka wafanyakazi, wote ni wenye elimu ya juu.
Bi. Mahire alisema"Narudia kuwaambia waajiriwa kuwa, kwanza ni lazima tujenge mtizamo sahihi ya kujitweza au kujikweza. Wahitimu wa vyuo vikuu ni sawa na wafanyakazi wengine, na hakuna tofauti ya kazi inayothaminiwa na isiyothaminiwa, ila tu kazi yenyewe inapaswa kunufaisha jamii na wafanyakazi wenyewe."
Kutokana na sifa nzuri ya wafanyakazi, kampuni ya huduma za nyumbani ya dada Mahire inapata ustawi. Na kinachomfurahisha zaidi ni kuwa, mama yake amebadilisha kwa kiasi fulani mtizamo kuhusu uamuzi wake wa kuacha kazi ya utumishi wa serikali na kujishughulisha na biashara.
Dada Mahire alisema "Hivi sasa kampuni yangu inakua hatua kwa hatua, inaonekana kuwa mama yangu anafurahi, akisema anaona shughuli ninazofanya zinafaa."
Dada huyo aliongeza kuwa, ana imani kuna siku ambayo atapata sifa za dhati kutoka kwa mama yake, na anajitahidi kutimiza lengo hilo kwa vitendo halisi.
Idhaa ya kiswahili 2008-01-31
|