Dawa za kuongeza nguvu ni tatizo kubwa linaloikabili michezo mbalimbali duniani. Wakati Michezo ya Olimpiki ya Beijing inapokaribia, China ikiwa nchi mwenyeji ya michezo hiyo, kazi yake katika kupambana na dawa za kulevya inafuatiliwa sana. Kuanzia mwishoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, wachina waligundua hatari zinazosababishwa na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, na katika miaka 20 iliyopita wamekuwa wakipinga matumizi ya dawa hizo. Hivi karibuni mkurugenzi wa Idara ya sayansi na elimu ya Idara kuu ya michezo ya China Bw. Jiang Zhixue alieleza hatua ya maendeleo ya China katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu. Bw. Jiang Zhixue alisema:
"Mwaka 1989 China ilipitisha sheria kanuni kuhusu kupiga marufuku, kufanya uchunguzi na kutoa adhabu kali kwa matumizi ya dawa za kuongeza nguvu. Mwaka 1990 kituo cha kupima matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kinachofikia kiwango cha kimataifa kilianzishwa nchini China, na mwaka 1992 Kamati ya kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu ya Kamati ya Olimpiki ya China pia ilianzishwa, na mafunzo kuhusu mapambano dhidi ya dawa hizo yalianza kutolewa. Kamati hiyo inashughulikia uchunguzi kuhusu utaratibu wa mapambano dhidi ya matumizi ya dawa hizo. Mwaka 1995 Sheria ya michezo ya Jamhuri ya watu wa China ilitangazwa na kuanza kutekelezwa baada ya kupitishwa kwenye bunge la umma la China, na mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu yaliwekwa kwa mara ya kwanza kwenye sheria ya nchi. Mwaka 2004 baraza la serikali ya China lilitangaza na kutekeleza Kanuni kuhusu mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, na China ilikuwa moja kati ya nchi chache iliyotangaza na kutekeleza sheria na kanuni maalum kuhusu shughuli hiyo duniani.
Aidha, China pia ilikuwa ni moja kati ya nchi iliyosaini mapema zaidi kanuni kuhusu mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu duniani, na pia ilikuwa nchi ya kwanza barani Asia iliyosaini Makubaliano ya kimataifa kuhusu mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kuongeza nguvu katika michezo ambayo ilitangazwa na Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa. Kabla ya Michezo ya Olimpiki ya Sydney ya mwaka 2000, ujumbe wa China uliwafukuza wachezaji 27 walioshindwa kupitia upimaji wa matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, na hatua hiyo yenye msimamo mkali ilisifiwa na mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa wa wakati huo Bw. Juan Antonio Samaranchi. Mwaka 2006 asilimia 1.98 ya wachezaji walithibitishwa kutumia dawa hizo, lakini kiasi hicho nchini China kilikuwa asilimia 0.4 tu mwaka jana.
Mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka 2007, kituo cha kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu cha China kilianzishwa, na hii ni moja kati ya maabara zinazoshughulikia upimaji wa dawa za kuongeza nguvu, ambayo imepewa cheti cha uthibitisho cha Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa na Shirika la kupambana na dawa za kuongeza nguvu duniani. Mwenyekiti wa Shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu duniani Bw. Richard Pound alisifu uwezo wa China katika upimaji wa dawa za kuongeza nguvu, anaona kuwa uwezo wa China katika shughuli hizo unalingana na kiwango cha Michezo ya Olimpiki. Bw. Pound alisema:
"Kuna maabara nzuri sana mjini Beijing, pia kuna zana mbalimbali nzuri, aidha waendeshaji wa maabara ni wanasayansi hodari, ambao wana uwezo wa kufanya vizuri kazi ya upimaji na uchunguzi unaohusika."
Ili kuiandaa Michezo ya Olimpiki isiyoathiriwa vibaya na dawa za kuongeza nguvu, idara ya michezo ya China inaimarisha kazi ya udhibiti wa matumizi wa dawa hizo kwa wachezaji. Ofisa wa Kamati ya kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu iliyo chini ya Kamati ya Olimpiki ya China Bw. Zhao Jian alisema:
"Tunaweka mkazo katika upimaji wa dawa hizo katika sekta zinazokabiliwa na hatari kubwa zaidi kutokana na matumizi ya dawa hizo ikiwa ni pamoja na riadha, kuogelea, kunyanyua uzito, mieleka, baiskeli, mbio za mashua, na Kayak na Canoe, na kati ya wachezaji mbalimbali tunatilia maanani katika wachezaji hodari."
Bw. Zhao Jian alisema mwaka 2006 kamati ya Olimpiki ya China ilifanya upimaji mara 9400, na wachezaji hodari kama Liu Xiang ambaye ni bingwa wa Michezo ya Olimpiki ya mchezo katika mbio za mita 110 za kuruka viunzi anapaswa kufanyiwa upimaji mara kumi kadhaa kwa mwaka.
Shirika la kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu duniani limefanya marekebisho kuhusu Kanuni ya kupambana na matumizi ya dawa hizo duniani mwezi Novemba mwaka 2007, na muda wa kupiga marufuku wachezaji waliogunduliwa kutumia kwa mara ya kwanza dawa za kuongeza nguvu kushiriki kwenye mashindano umeongezwa hadi kufikia miaka minne kutoka miaka miwili ya zamani. Akizungumzia kuhusu hatua hiyo Bw. Zhao Jian alisema:
"Mimi binafsi nakubaliana na uamuzi huo. Kwani matumizi ya dawa za kuongeza nguvu ni kitendo cha kukiuka maadili. Lakini baadhi ya wachezaji bado wana fursa ya kurejea kwenye uwanja wa michezo hata kama wakiadhibiwa kupigwa marufuku kushiriki kwenye mashindano ndani ya miaka miwili tu. Naona kuwa haipaswi kutoa fursa hiyo kwa wachezaji kama hao, ili kuhakikisha usafi wa uwanja wa michezo."
Lakini watu wanaoshughulikia michezo nchini China pia wamegundua kuwa elimu ni njia yenye ufanisi ya kuondoa matumizi ya dawa hizo, na wanafanya juhudi katika kazi hiyo. Bw. Zhao Jian alisema:
"China imefanya juhudi kubwa katika kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu, na wachezaji wa China hawakukiuka kukiuka kanuni zinazohusika katika mashindano mbalimbali duniani yaliyofanyika katika miaka ya hivi karibuni. Naona mafanikio hayo yanategemea njia yetu yenye umaalum. Mbali na kufanya ukaguzi, pia tunaweka mkazo katika kuimarisha usimamizi wa timu ya michezo, na kueneza ujuzi na elimu zinazohusika kwa wachezaji. Naona hii ni njia yenye ufanisi ya kutatua suala hilo, na tulifanya vizuri katika upande huo."
Wachina wana matumaini ya kuiandaa Michezo ya Olimpiki isiyoathiriwa vibaya kutokana na matumizi ya dawa za kuongeza nguvu. Kwani hiyo si kama tu ni kanuni ya Michezo ya Olimpiki, bali pia ni matumaini ya pamoja ya watu wanaopenda michezo duniani.
Idhaa ya kiswahili 2008-02-12
|