Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-11 18:10:29    
Mila na desturi za mwaka mpya wa jadi wa China

cri

Kwa mujibu wa kalenda ya kilimo ya China tarehe 7 Februari ni sikukuu ya mwaka mpya wa Kichina, yaani sikukuu ya Spring. Kwa Wachina siku hiyo ni muhimu sana, sherehe yake inaanzia leo na kuendelea kwa siku 15. Katika kipindi hiki cha siku 15 shamrashamra za aina nyingi zitafanyika katika sehemu mbalimbali nchini China, na mila na desturi zilizoanza toka zama za kale zinaendelea kufuatwa hivi leo. Makala hii inahusu mila na desturi hizo.

Katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa jadi wa China Wachina wanatakiana salamu za mwaka mpya. Asubuhi na mapema wazee na watoto wakiwa wamevaa nguo mpya wanatoka majumbani kwenda kutoa salamu zao au kusubiri nyumbani kupokea salamu za wengine, watu wanapokutana husalimiana kwa kusema "Furaha ya mwaka mpya!", "Nakutakia heri ya mwaka mpya!"

Wakati wa kutakiana salamu za mwaka mpya, watoto huwa wa kwanza kuwasalimia wazee, na wazee huwapa watoto pesa zikiashiria kuwaondolea bahati mbaya.

Lakini kama watoto wamepewa pesa hizo katika usiku wa kuamkia siku hiyo, wazee hawatawapa tena.

Hapo kabla pesa zilikuwa kidogo sana na watoto walitumia pesa hizo kununua peremende na vitu vya kuchezea tu, lakini hivi leo, maisha yamekuwa bora, pesa hizo zimeongezeka, watoto wengi wanalimbikiza pesa hizo na kuwasaidia watoto wanaoshindwa kusoma shuleni wanaoishi katika sehemu maskini, wanaona kutumia pesa hizo vizuri, ni jambo la maana zaidi.

Kuwasha fataki ni mila ya jadi katika siku ya kwanza ya mwaka mpya, watu wanaona kwamba bahati mbaya na mambo ya usumbufu yote yatafukuzwa na vishindo vya fataki na bahati nzuri na furaha zitakuja nyumbani.

Kutokana na jinsi jamii inavyoendelea na watu wanavyozidi kuthamini usafi wa mazingira, tokea mwaka 2005 serikali ya Beijing iliamua kudhibiti uwashaji wa fataki kwa kuweka maeneo na muda maalumu, ili kuhakikisha mbingu na hewa mjini Beijing inakuwa safi. Kwa kiasi fulani watu wanazuiliwa kuwasha fataki, lakini hamu yao ya kusikiliza vishindo vya fataki haijapungua.

Kwa hiyo, kwenye tovuti za mtandao wa internet umewekwa mchezo wa kuwasha fataki ili watu wajipatie raha.

Ukibonyeza tu kwenye mtandao wa internet unweza kuona na kusikia vishindo vya fataki za aina mbalimbali.

Katika siku ya pili ya mwaka mpya wa jadi wa China wazee na watoto huwa wanakwenda magulioni kuangalia shamrashamra za kila aina na kuonja vyakula vyenye mapishi mahsusi ya kisehemu. Kwenye magulio kuna michezo ya jadi ya aina nyingi ikiwa ni pamoja na kuchezesha dragoni na simba waliotengenezwa kwa vitambaa na kucheza michezo ya ngongoti.

Mchezo wa ngogoti unavutia zaidi. Wachezaji wanaigiza kama watu mashuhuri wa kale wakiwa wamefunga miguu kwenye fimbo na kutembea kama kawaida. Ni ajabu kwamba hata wanaweza kucheza ngoma na kurukaruka.

Katika siku hiyo ya pili ya mwaka mpya wa jadi wa China, binti aliyeozwa huwa anarudi nyumbani kwa wazazi. Kutokana na mila ya Wachina, mwanamke baada ya kuolewa anaishi kwa mume wake na hapati nafasi nyingi za kurudi nyumbani kuwatembelea wazazi wake. Lakini katika siku hiyo ni lazima arudi nyumbani na kujiunga na wazazi wake. Katika siku hiyo wazazi huwakaribisha binti na mkwe wao kwa chakula kitamu.

Kwa kawaida binti aliyeolewa anapowatembelea wazazi wake huwa na zawadi kwa wazazi na ndugu zake. Kuna wimbo mmoja uitwao "Kurudi nyumbani kwa mama yangu", ni wimbo uliosikia hivi punde. Wimbo huo unasema, "mkono wa kushoto umeshika kuku, mkono wa kulia umeshika bata, na mgongoni nambeba mtoto wangu", ni wimbo unaoeleza vizuri jinsi binti aliyeolewa anavyorudi nyumbani kwa wazazi akiwa na zawadi.

Katika siku ya tatu ya mwaka mpya, wageni wanatoka na kuingia nyumbani. katika siku hiyo marafiki hutembeleana na zawadi, kwa kupitia matembezi hayo wanaongeza urafiki kati yao. Hapo kabla, watu walipowatembelea marafiki walikuwa na zawadi za aina tofauti za keki zilizotiwa ndani ya boksi la karatasi.

Lakini kadiri maisha yanavyobadilika kuwa mazuri, "boksi" la keki linapuuzwa na badala yake kunakuwa na mvinyo na vyakula vya kujenga afya.