Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-12 19:45:07    
Mke na mume kutoka Ujerumani walioamua kuishi nchini China

cri

Kabla ya miaka kadhaa iliyopita Bw. Bauwer Braun toka Ujerumani alikuja China na kujifunza kichina mjini Xi'an. Alipokuwa mjini Xi'an alisikia kuwa mkoa wa Qinghai ulioko kwenye uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet ni sehemu yenye maajabu mengi, ambao una maliasili nyingi, mazingira ya kipekee, ambapo watu wa makabila mbalimbali wanaishi huko. Hayo yalimvutia Bw. Braun. Baada ya kumaliza masomo yake mjini Xi'a, Alikwenda mkoa wa Qinghai. Baada ya kufika huko, vitu vingi vilimvutia sana, alisema,

"Nafikiri mkoa wa Qinghai ni sehemu yenye utamaduni wa makabila mbalimbali. Watu wa makabila wa Wahan, Watibet, Wahui na Wamongolia wanaishi hapa. Kila kabila lina utamaduni wake kipekee, lugha yake, sanaa ya kipekee, na sikukuu zao. Nina hamu kubwa ya kujua mambo hayo. Ninavutiwa na utamaduni mbalimbali wa makabila madogo madogo."

Baada ya kuishi mkoani Qinghai kwa muda, Bw. Braun alijua mambo mengi zaidi kuhusu mkoa huo. Alitambua kuwa katika mkoa huo ambao ni moja ya sehemu tano za ufugaji nchini China, kuna wanyama na mimea ya aina mbalimbali, hasa ng'ombe aina ya Yak. Ng'ombe hao wanasifiwa kuwa mashua kwenye sehemu zinazofunikwa na theluji, wanaishi kwenye uwanda wa juu wa Qinghai-Tibet ulioko kwenye mwinuko wa mita 4000 kutoka usawa wa bahari, na wanakula nyasi zisizochafuliwa. Kutokana na mazingira na chakula cha kipekee, maziwa ya ng'ombe hao ni mazuri kuliko maziwa ya ng'ombe ya kawaida. Baada ya kujua jambo hilo, Bw. Braun alifikiri kujenga kiwanda cha Jibini kwa kutumia maliasili ya huko. Alipoanzisha kiwanda chake alikabiliwa na matatizo mengi, lakini wenyeji wa Qinghai wanamsaidia kutatua matatizo hayo, alisema,

"Nilipanga kuanzisha kiwanda cha jibini wilayani Zeku, lakini baada ya kiwanda changu kuanza kufanya kazi, nilikabiliwa na matatizo mengi. Wenyeji wa hapa wana moyo mema na urafiki, walinisaidia kuzalisha jibini. Hivi sasa mimi na wafanyakazi tunajifunza njia nzuri zaidi ya kutengeneza jibini, nina matumaini kuwa mwakani kiwanda chezo kitatengeneza jibini za aina mpya."

Mwishoni mwa mwaka 2006, Bw. Braun alianzisha kiwanda chake cha Jibini wilayani Zeku, iliyoko mashariki mwa mkoa wa Qinghai. Kiwanda hicho chenye wafanyakazi zaidi ya 100 kilianzishwa kwa uwekezaji wake na wa watu wengine. Hivi sasa yeye na wafanyakazi wanafanya utafiti na majaribio ya kutengeneza jibini za aina mpya. Anaamini kuwa biashara yake itapata maendeleo siku hadi siku.

Mwezi Machi mwaka 2007, mke na watoto wawili wa Braun pia walikwenda Qinghai. Familia hiyo inataka kuishi mkoani humo. Mwanzoni mke wake Bibi Jannifer Braun hakuweza kuzoea maisha kwenye uwanda wa juu, na hakuweza kuelewa kwa nini mumewe alichagua kuishi huko badala ya Ujerumani. Lakini hivi sasa Bibi Braun ameelewa uamuzi wa mumewe, na anapenda mkoa wa Qinghai. Alisema,

"Siku kadhaa baada ya kufika hapa kichwa changu kilikuwa kinauma kila siku. Kwa sababu hapa ni uwanda wa juu, na mwangaza wa jua ni mkali, lakini hivi sasa nimepona na kuzoea. Watu wa mkoa huu wanafuata desturi za jadi na wana urafiki. Watibet, Waislamu na Wahan wanaishi pamoja, nafiriki hilo ni jambo la kipekee. Hapa hali ya hewa ni nzuri, hakuna uchafuzi, tunaweza kwenda kupanda milima mara kwa mara."

Bibi. Braun aliweza kuzungumza na mwandishi wa habari kwa kichina. Alisema alianza kujifunza kichina katika chuo cha makabila cha Qinghai miezi kadhaa iliyopita, ili aweze kuwasiliana na wenyeji wa huko. Hivi sasa tatizo la mawasiliano limeondolewa, na amepata marafiki wengi. Kila akipata nafasi, anawatembelea marafiki zake, alisema,

"Ninakwenda nje na watoto wangu mara kwa mara. Tunawatembelea marafiki zetu na wazazi wa marafiki. Hivi sasa mtoto wangu wa kiume ana umri wa miaka 6, anakwenda nje kucheza na marafiki zake."

Familia ya Braun imezoea maisha ya huko. Watoto wawili wanasoma katika shule ya huko, wanajifunza na kucheza pamoja na watoto wa China. Wakati fulani wanatembelea sehemu mbalimbali ili kutazama mandhari nzuri ya mkoa wa Qinghai na utamaduni mbalimbali. Bibi. Braun alisema,

"Mwezi Julai tulitembelea ziwa Qinghai, mandhari ya huko ni nzuri. Hekalu la Taer pia ni kivutio kizuri cha utalii, tuliona vitu vingi vya dini ya kibudha."

Ziwa Qinghai na Hekalu ya Taer ni vivutio maarufu vya utalii mkoani humo. Ziwa Qinghai ni ziwa kubwa zaidi la maji ya chumvi nchini China. Kando ya ziwa hilo kuna mbuga kubwa, kambi ya wafugaji, ng'ombe na mbuzi wengi. Hekalu la Taer ni hekalu maarufu la dhehebu la kitibet la dini ya kibudha. Lina historia ndefu, na mtindo wa majengo ya hekalu hilo ni wa kipekee. Pia kuna michoro na vitabu vingi kwenye hekalu hilo. Bibi. Braun alisema mandhari ya mkoa wa Qinghai ni nzuri, dini ya kibudha ya kitibet pia ni ya kipekee.

Familia ya Bw Braun imekutana na wageni kadhaa mkoani Qinghai, akiwemo Bw. Joshua Lotz ambaye ni mwanafunzi kutoka Marekani. Katika miaka mitano iliyopita, Bw. Lotz anayejifunza kozi ya elimu ya matibabu ya kiviumbe alikwenda Qinghai wakati wa likizo, ili kufanya utafiti kuhusu dawa za kitibet. Katika miaka hiyo mitano, aliona mabadiliko ya Qinghai, alisema,

"Katika miaka mitano iliyopita, mabadiliko makubwa yametokea mkoani Qinghai, kwa mfano majengo ya mijini yamebadilika. Si kama tu majengo yamekuwa ya kisasa zaidi, bali pia kuna mtandao wa Internet na televisheni kwenye majengo hayo. Pia unaweza kuona vitu vingi ni vya kawaida kwenye miji mikubwa nchini China au duniani, kwa mfano mikahawa ya vyakula vya kimagharibi, ambayo unaweza kunywa kahawa nzuri huko. Miaka mitano iliyopita, kulikuwa hakuna vitu kama hivyo."

Hivi sasa wageni ambao wanafanya utalii, biashara na kusoma mkoani Qinghai wanaongezeka kuwa wengi zaidi mwaka hadi mwaka. Sawa na familia ya Bw Braun na Bw. Lotz, mwanzoni wanakuwa hawajui mambo mengi kuhusu mkoa huo, baadaye wanajua mambo mengi zaidi, na baadhi yao wanapenda mkoa huo, na hata wanaamua kuishi huko.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-12