Kadiri makampuni mengi ya Korea ya Kusini yanayowekeza mjini Qingdao mkoani Shandong, China yanavyoongezeka zaidi, ndivyo mji wa Qingdao unavyokuwa sehemu wanakoishi Wakorea Kusini wengi kabisa nchini China. Watu hao kutoka Korea Kusini wanaishi kwa furaha na kufanya kazi kwa bidii nchini China, na wamekuwa sehemu isiyoweza kukosekana katika kuhimiza maendeleo ya uchumi wa huko. Katika miaka ya hivi karibuni, Wakorea Kusini wengi wamekuwa wanakwenda kuishi na kufanya kazi mjini Qingdao. Hivi sasa Wakorea Kusini karibu laki 1 wanaishi mjini humo, na mji huo umekuwa maskani yao ya pili.
Lee Sung hoon mwenye umri wa miaka 10 anaishi mjini Qingdao pamoja na wazazi wake, yeye anaweza kuongea lugha za Kikorea, Kiingereza na Kichina. Alisema yeye amekuwa Mqingdao halisi. Alisema:
"Mama aliniambia kuwa, niliwahi kuja hapa Qingdao kabla ya kuzaliwa. Na siku 100 baada ya kuzaliwa kwangu nchini Korea ya Kusini, nilirudi tena hapa Qingdao. Hatuna nyumba nchini Korea ya Kusini, tunaporudi nchini Korea ya Kusini, tunaishi nyumbani kwa nyanya wangu. Naipenda makazi yetu hapa China, naona nyumbani kwangu ni hapa China."
Kuna watoto wengi wa Korea Kusini kama Lee Sung Hoon mjini Qingdao. Walikuja China walipokuwa watoto, hata baadhi yao walizaliwa nchini China, wamepata rafiki na Wachina, wanachezea vitu vinavyotengenezwa na China, na kutazama katuni za kichinakwa hiyo kwao China sio nchi ngeni, bali ni maskani yao.
Kufundisha lugha ya Kiingereza kwa watoto wa Korea Kusini nchini China ni lengo la kwanza la Bw. Yang Yong kyu, ambaye ni mkuu wa shule ya Xiaolong inayofundisha lugha ya Kiingereza. Bw. Yang Yong kyu alipozungumzia sababu ya kwenda Qingdao kuanzisha shule hiyo alisema,
"Mimi nilikuwa na shughuli zangu nchini Korea Kusini, lakini marafiki zangu walikuwa wananiambia kuhusu mambo ya kuwekeza nchini China, baadaye niliamua kuja hapa kufanya ukaguzi wa kina, nikagundua kuwa hali ya hewa ya hapa ni nzuri, na mazingira ya uwekezaji pia ni mazuri, ambayo yanafaa Wakorea Kusini kuishi, hivyo nikaamua kuja hapa."
Nyumba ya Bw. Yang Yong kyu nchini Korea ya Kusini iko Seoul, huko pia alianzisha shule ya wanawake. Miaka minne iliyopita, yeye na mke wake walikwenda mjini Qingdao kuanzisha shule ya dragon mdogo ya kufundisha lugha ya Kiingereza. Alipofikiria kuchagua jina la shule alichunguza vitu vingi, hatimaye alichagua "Xiaolong", maana yake ya Kichina ni dragon. Bw. Yang Yong kyu alisema,
"Kuanzia zamani za kale hadi sasa dragon ni alama ya China, nataka kukaribia dragon mkubwa wa China. Wanaofundishwa hapa ni watoto, sasa wao ni kama dragon wadogo, na katika siku za baadaye watakuwa dragon wakubwa. Wao ni mustakabali wa nchi. Ni matumaini yangu kuwa baada ya watoto hao kukua, wataweza kutoa mchango kwa maendeleo ya nchi na jamii."
Bw. Yang Yong kyu ameishi mjini Qingdao kwa miaka minne, na ana marafiki wengi wa China. Mtoto wake wa kwanza alizaliwa mjini Qingdao, na amekuwa na umri wa mwaka mmoja na nusu. Alimpa jina la "Yingmin" la Kichina. Ana matumaini kuwa mtoto huyo atakua vizuri na kuwa na ushujaa na akili kama watu wa nchi hizo mbili. Bibi Kwon Young jin ni mke wa Bw. Yang Yong kyu. Licha ya kufanya kazi na mume wake shuleni, pia anamtunza mtoto na kufanya kazi za nyumbani. Alisema kabla ya kuja hapa China alikuwa na wasiwasi kuhusu maisha hapa, kama mazingira ni mazuri au la, na kama anaweza kuzoea hali ya hewa hapa China, vyakula na hali ya usalama. Alikuwa na wasiwasi sana kuhusu kwenda mjini Qingdao pamoja na mume wake. Lakini baada ya kuishi kwa miaka minne, sasa wasiwasi tena wake umetoweka. Alisema,
"Kabla ya kuja hapa China, marafiki wengi waliniambia kuwa ni taabu kuishi nchini China. Lakini baada ya kuishi kwa muda mfupi, naona urahisi mwingi wa kuishi hapa. Hivi sasa maisha yetu hapa Qingdao ni starehe, kila nikirudi Korea Kusini, siwezi kukaa kwa zaidi ya wiki moja, huwa natamani kurudi hapa China."
Bw. Yang Yong kyu na mke wake wanaridhika na maisha yao mjini Qingdao, na mara kwa mara wanawachukua wazazi wa pande mbili za mume na mke kukaa nao kwa muda nyumbani kwao nchini China. Bw. Yang Yong kyu ana matumaini kuwa atanunua nyumba mjini Qingdao, na kuishi hapa kwa muda mrefu. Pia anataka kuanzisha shule nyingi katika miji mingine nchini China. Alisema asili yake iko nchini Korea ya Kusini, lakini hisia zake ziko nchini China.
Mjini Qingdao kuna familia nyingi kama ya Bw. Yang Yong kyu. Kwa mujibu wa takwimu, hivi sasa mkoani Shandong, China kuna makampuni ya Korea Kusini zaidi ya elfu 10, na mjini Qingdao kuna makampuni hayo zaidi ya elfu 6. Uwekezaji wa makampuni hayo mkoani Shandong umezidi dola za kimarekani bilioni 20, ambao ulichukua asilimia 57 ya uwekezaji wa makampuni ya Korea Kusini nchini China. Mkoa wa Shandong umekuwa mwenzi mkubwa kabisa wa biashara kwa Korea ya Kusini.
Bw. Kim Sun heung ni balozi mdogo wa Korea Kusini mjini Qingdao. Kabla ya hapo alikuwa balozi mdogo wa Korea Kusini mjini Shanghai. Watoto wake wawili kati ya watatu walizaliwa nchini China, hivyo wana hisia maalum kwa China. Bw. Kim Sun heung alisema,
"Utamaduni wa Korea ya Kusini unafanana na utamaduni wa mkoa wa Shandong. Kwa muda mrefu, utamaduni wa Korea Kusini unaathiriwa na mkoa wa Shandong. Hali ya hewa, desturi na vyakula vya mkoa wa Shandong vinafanana na Korea Kusini, na jiografia yake pia ni nzuri. Watu wa Shandong ni wakarimu, Wakorea Kusini wanaweza kuishi vizuri mkoani Shandong."
Bw. Kim Sun heung alisema, kutokana na kufanana kwa utamaduni wa Korea Kusini na China, hivyo watu wa Korea Kusini wanaweza kujiunga na jamii ya China kwa haraka. Maendeleo na mabadiliko ya China pia yana athari kwao, na watu wa Korea Kusini wanataka kutoa mchango katika mawasiliano ya uchumi na utamaduni wa nchi hizi mbili.
|