Katika kipindi hiki tunawaletea maelezo kuhusu Bw. Guy Rufus Chambers kutoka Uingereza, anayeishi mjini Xi an.
"Hii ni Redio China Kimataifa, mimi ni Qin Bokai, ninakusalimu kutoka mjini Xi'an"
Wasikilizaji wapendwa, mnaonaje Kichina chake? Bw. Chambers alijifunza Kichina kwenye chuo kikuu. Yeye anasimamia kampuni yenye wafanyakazi wachina karibu elfu 1 mjini Xi'an bila kuwa na mkalimani.
"Nilianza kujifunza lugha ya Kichina katika chuo kikuu cha Cambridge mwaka 1989. Nilijifunza Kichina nchini Uingereza kwa miaka minne, na pia nilijifunza katika Chuo Kikuu cha Umma cha China."
Bw. Chambers mwenye umri wa miaka 37 ni msimamizi mwandamizi wa kampuni ya John Swire & Sons ya Uingereza ya Coca Cola, hivi sasa yeye ni mjumbe wa bodi ya wakurugenzi na meneja mkuu wa kampuni ya Coca Cola ya Zhongcui ya kampuni ya John Swire & Sons mjini Xi'an.
Bw. Chambers alisema yeye anapenda kujifunza lugha mbalimbali, alijifunza Kifaransa na Kilatin alipokuwa shule ya sekondari. Kutokana na kupenda utamaduni wa China, alijifunza Kichina katika kitivo cha Emmanuel cha Chuo Kikuu cha Cambridge, na alijipatia jina la Kichina la Qin Bokai.
Bw. Chambers alisema aliamua kujifunza Kichina kutokana na athari ya mwalimu wake na vitabu kuhusu China, ambavyo vinamfanya kutambua kuwa China ni nchi kubwa yenye historia ndefu na utamaduni mkubwa, tena wakati huo China ilikuwa imetekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango kwa miaka 10, na uchumi wake ulikuwa unapata maendeleo ya kasi. Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu mwaka 1993, Bw. Chambers alijiunga na kampuni ya John Swire & Sons ambayo ni kampuni kubwa ya kimataifa. Kutokana na ujuzi wake wa lugha na uwezo wake, alishughulikia usimamizi katika kampuni za Coca Cola za huko Taiwan na Hongkong. Mwaka 2005 alianza kufanya kazi ya usimamizi katika kampuni ya Coca Cola ya Zhongcui mjini Xi'an.
Bw. Chambers anayefahamu Kichina hana tatizo lolote kuwasiliana na wafanyakazi wachina, anaweza kufanya kazi kwa urahisi zaidi. Alisema ingawa anatoka Uingereza, utamaduni wake ni tofauti na utamaduni wa wafanyakazi wachina, lakini siku zote anasisitiza kupata mafanikio kwa mshikamano na ushirikiano. Wao wameanzisha utamaduni unaofaa kampuni yao, ambao unaundwa na asilimia 90 ya mtizamo wa kichina na uzoefu wa makampuni ya kisasa duniani, Bw. Chambers alisema,
"Katika kampuni yetu mjini Xi'an kuna wafanyakazi wapatao 994, na miongoni mwao mgeni ni mmoja tu."
Mwaka 2005 Bw. Chambers na familia yake walihamia mjini Xi'an na alianza kufanya kazi huko. Wakati wa mapumziko baada ya kazi, anaendelea na desturi yake ya kusoma vitabu kuhusu China, na alianza kuupenda mji wa Xi'an. Anaona kuwa miji mingi mikubwa ya China ikiwemo Beijing na Shanghai ni ya kisasa, na watu wengi wanahamia katika miji hiyo kutoka sehemu nyingine, hivyo umaalumu wa utamaduni wa miji hiyo umepungua, lakini utamaduni wa kipekee umehifadhiwa vizuri mjini Xi'an, mambo mengi yakiwemo ukuta wa mji wa kale na mto unaolinda mji, sehemu mpya na sehemu ya zamani za mji zinazotofautiana, mtaa wanakoishi watu wa kabila la Wahui na majengo ya kale, yote hayo yamemfanya Bw. Chambers aone hali halisi zaidi ya China, alisema,
"Xi'an ni mji mzuri sana. Inafahamika kuwa mji huo uliwahi kuwa mji mkuu katika enzi 13 kwenye historia ya China. Aidha, kuna mambo mengi ya kuvutia mjini humo."
Bw. Chambers anapenda kutembelea sehemu mbalimbali kwenye mji huo maarufu wa kihistoria na kiutamaduni. Alisema anafanya kazi na kuishi mjini Xi'an, ni lazima ajue mambo mengi zaidi kuhusu mji huo. Miongoni mwa vivutio vingi vya kihistoria, Bw. Chambers anavutiwa zaidi na makaburi ya Hanyang, alisema,
"Ninavutiwa zaidi na makaburi ya Hanyang. Watalii wengi wanapokuja Xi'an wanapenda kutazama sanamu za askari na farasi. Kweli sanamu za askari na farasi ni nzuri, lakini nafikiri wakipata fursa, ni vizuri zaidi kutembelea makaburi ya Hanyang. Mimi nimewahi kutembelea makaburi hayo kwa mara tano hadi sita."
Bw. Chambers alisema makaburi la Hanyang yako kitongojini, ni makaburi ya Mfalme Jin na mama yake malkia wa Enzi ya Han. Bw. Chambers anavutiwa zaidi na jumba la makumbusho la makaburi hayo. Katika jumba hilo watalii wanaweza kwenda chini ya ardhi, na kutazama mabaki ya utamaduni yaliyofukuliwa au yanayofukuliwa, wakisimama kwenye daraja la kioo. Bw. Chambers pia anavutiwa na vyakula vya Xi'an, anaweza kutaja majina mengi ya vyakula, alisema,
"Napenda zaidi tambi, hiki ni chakula kinachoweza kupikwa kwa urahisi ni chakula kitamu sana, tena unaweza kununua bakuli moja ya tambi kwa Yuan nne hadi tano."
Kutokana na kufanya kazi na kuishi mjini Xi'an kwa muda mrefu, Bw. Chambers anajua mambo mengi kuhusu wakazi wa Xi'an, alisema,
"Wakazi wa Xi'an ni watulivu, wanaaminika, wenye unyofu na ni rahisi kufanya urafiki nao, wageni wanaweza kutalii na kuishi vizuri mjini Xi'an."
Bw. Chambers anaona kuwa Wakazi wa Xi'an wamerithi vizuri utamaduni wao, mila na desturi nyingi ambazo hazionekani katika sehemu nyingine nyingi za China, bado zinaweza kuonekana mara kwa mara mjini humo. Kwenye mitaa ya mji huo, mara kwa mara Bw. Chambers anaona wakazi wanaimba nyimbo za kipekee za mkoa wa Shaanxi na kupiga ala za muziki. Ingawa Bw. Chambers anapenda mji wa Xi'an, lakini ataondoka hivi karibuni, kwa sababu kampuni ya John Swire & Sons imeamua kumhamishia kwenye kampuni ya Hongkong. Alisema,
"Nimeishi kwa furaha mjini Xi' an kwa miaka miwili, na nimekupata marafiki wengi hapa. Katika siku zijazo nitapata fursa ya kurudi hapa kufanya kazi tena, na kama sitapata fursa ya kikazi, basi mimi na familia yangu tutarudi kutembelea mara kwa mara, kwa sababu Xi'an ni mji wa kipekee wenye utamaduni unaong'ara, historia ndefu na vyakula vitamu."
|