Mwezi Juni mwaka 2007, idara ya sheria za kimataifa kilianzishwa rasmi katika chuo kikuu cha Beijing. Mkuu wa awamu ya kwanza wa idara hiyo ni mtaalamu mashuhuri wa sheria wa Marekani profesa Jeffrey Lehman. Kabla ya hapo, profesa Lehman alikuwa mkuu wa chuo kikuu cha Cornell cha Marekani.
Suti nadhifu, nywele za dhahabu, miwani isiyo na fremu na tabasamu usoni, hii ndiyo picha ya kwanza utakayoiona ukimwona Bw. Lehman kwa mara ya kwanza. Profesa Lehman aliwahi kuwa mkuu wa kitivo cha sheria katika chuo kikuu cha Michigan cha Marekani na mwenyekiti wa shirikisho la vitivo vya sheria vya Marekani, mwaka 2003 aliteuliwa kuwa mkuu wa chuo kikuu cha Cornell, katika muda huo, profesa Lehman alifanya mageuzi katika pande mbalimbali za chuo kikuu hicho na kusukuma mbele zaidi mchakato wa kukifanya chuo hicho kiwe cha kimataifa.
Profesa Lehman aliwahi kuja China mwaka 1998. Mwaka 2004 aliongoza ujumbe wa chuo kikuu cha Cornell na kufanya ziara nchini China, na kuhudhuria siku ya chuo kikuu cha Beijing na chuo kikuu cha Cornell, shughuli hizo zilijenga urafiki mkubwa kati yake na chuo kikuu cha Beijing. Profesa Lehman alisema, ikilinganishwa na safari yake ya kwanza nchini China miaka 10 iliyopita, kila safari alipoitembelea China alikuwa na hisia tofauti. Profesa Lehman alisema:
"kila safari nilipokuja China, nilishuhudia mabadiliko makubwa yaliyotokea. Beijing ya leo ni mji wa kisasa wenye ustawi sana. Mjini huu una majengo mengi mapya na mazuri, kama vile jumba la maonesho la taifa, jengo jipya la makao makuu ya CCTV na jumba la michezo ya Olimpiki "kiota", mabadiliko hayo yote yamenivutia sana. Lakini hayo ni upande wa nje, wanaonivutia zaidi ni watu wa China. Nilipokuja China mwaka 1998, niliona busara na mtazamo wazi wa watu wa China. Wachina wa sasa wamekuwa na mtazamo wa wazi zaidi, wamekuwa na urafiki na wakarimu zaidi, na wamenisaidia zaidi kuifahamu China vizuri."
Kutokana na upendo wake kwa utamaduni wa China, profesa Lehman alifanya juhudi kusukuma mbele mawasiliano na ushirikiano kati ya vyuo vikuu vya China na Marekani kuhusu utafiti wa sheria na elimu ya juu. Mwaka 2005, kituo cha utafiti wa sera na sheria za China na Marekani kilichoandaliwa kwa pamoja na chuo kikuu cha Beijing na Chuo kikuu cha Lugha za kigeni cha China kilianzishwa rasmi. Profesa Lehman akiwa ni mmoja waanzilishi wa shughuli hiyo, alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa kituo hicho na kutoa mchango muhimu kwa maendeleo ya kituo hicho. Bi. Rong Liya aliyefanya kazi pamoja na profesa Lehman kwa miaka mingi alisema:
"yeye ni mtu hodari sana, anapenda kutoa mchango wake kwa kila jambo analofanya, hasa kwa shughuli zinazohusu elimu ya juu ya China na Marekani. Kwa mfano, tulipoanza kuandaa kituo hicho, hatukuwa na pesa hata kidogo, tulitakiwa kukusanya fedha. Lakini kwa nyakati nyingi tulishindwa kupata fedha, baadhi ya nyakati tulikuwa tunapaswa kutoa fedha zetu wenyewe."
Profesa Lehman akiwa ni mkuu wa zamani wa chuo kikuu cha Cornell, alikuwa na machaguo mengi mazuri baada ya kuondoka kutoka kwenye chuo kikuu hicho. Lakini alikubali kwa furaha mwaliko wa kuwa mkuu wa kwanza wa kitivo cha sheria ya kimataifa katika chuo kikuu cha Beijing. Bw. Lehman alisema:
"mpaka sasa bado naona furaha na fahari kuchukua wadhifa huo. Elimu ya sheria inaendelea kwa kasi sana nchini China, mwanzoni nilikuwa napanga kufanya kazi nchini Marekani au Ufaransa kabla ya kustaafu, kwa kuwa elimu ya sheria katika nchi hizo mbili imeendelea kwa muda mrefu. Sheria zina mabadiliko madogo katika mifumo ya sheria ya nchi hizo mbili. Lakini nchini China elimu ya sheria imeendelea kwa kasi, hivi sasa China inaendelea kuelekea kiwango cha kimataifa, naona China itakuwa mtangulizi katika mageuzi ya elimu ya sheria, ninafurahi kuweza kushuhudia mchakato huo."
Profesa Lehman alisema, hivi sasa elimu ya sheria katika nchi nyingi bado inafuatilia mambo ya ndani ya nchi hizo tu, ingawa vyuo vikuu vingi vimeweka masomo ya sheria ya kimataifa, lakini bado yanatilia maanani hali ilivyokuwa katika mazingira ya ndani ya nchi hizo. Profesa Lehman anaona kuwa, mfumo wa elimu ya sheria wa namna hiyo umekuwa unashindwa kukidhi mahitaji ya utandawazi duniani, na unapaswa kufanyiwa mageuzi. Ni matumaini yake kuwa kitivo cha sheria ya kimataifa kinachoongozwa naye kitaweza kupata mafanikio kadhaa katika eneo hilo. Profesa Lehman alisema:
"hivi sasa kama mmarekani akitaka kuwa mwanasheria wa kimataifa, basi itakuwa haitoshi kwake kujifunza sheria za Marekani tu, bali anapaswa kujifunza mambo mengi zaidi, nadhani hii pia ni mahitaji ya kuwa mwanasheria nchini China. Hivi sasa vyuo vingi vya sheria vya China si kama tu vinafundisha sheria za China, bali pia vinafundisha sheria za kimataifa, hali hiyo imekuwa nzuri zaidi kuliko hali ilivyokuwa nilipokuwa nasomea sheria katika chuo kikuu cha Michigan miaka 70 ya karne iliyopita. Lakini naona kuwa, watu bado wanapaswa kufanya kazi nyingi zaidi, vyuo vingi vya sheria pia vinapaswa kuongeza mambo mengi zaidi."
|