Mkoa wa Xinjiang ni sehemu wanakoishi watu wa kabila la Waurgur wa China, na Kashi iliyoko kusini mwa mkoa huo ni sehemu yenye mila na desturi zaidi za kikabila na umaalum wa kiislam mkoani Xinjiang, na wakazi wa huko wengi zaidi ni wa kabila la Waurgur. Hivyo watu husema, "kama ukitembelea mkoa wa Xinjiang bila kufika mji wa Kashi ni sawa na bure".
Kashi iko kusini mwa mkoa wa Xinjiang, na zaidi ya asilimia 90 ya wakazi wa huko ni wa kabila la Waurgur. Waurgur wengi ni waumini wa dini ya Kiislam, hivyo mjini Kashi kuna misikiti karibu 10,000, miongoni mwa misikiti hiyo, msikiti wa Hetgah ni maarufu kabisa.
Msikiti wa Hetgah ulioko katikati ya mji wa Kashi ni alama ya mji huo mkongwe. Msikiti huo ulijengwa mwaka 1442, hadi sasa una historia ya zaidi ya miaka 500, ambayo ni moja ya misikiti mikubwa kabisa nchini China.
Siku moja ya mwezi Agosti, mwandishi wetu wa habari alikwenda kwenye Msikiti wa Hetgah kukusanya habari, wakati muda wa swala ukikaribia. Imam alikuwa anatoa adhana, ambayo ilikuwa inasikika kote mjini. Halafu Waislam waliovaa balaghashia za ki-uyrgur walikuwa wanamiminikia msikitini kutoka sehemu mbalimbali mjini. Kijana wa kabila la Waurgur, Kamil, ni mfanyakazi wa Msikiti wa Hetgah, anaona fahari kwa kazi yake hiyo, akisema,
"Kila mara kwa wastani kuna watu elfu moja hadi elfu mbili wanaokuja kuswali hapa. Siku ya Ijumaa wakati huu, idadi ya watu wanaokuja kuswali huwa inakaribia elfu 20. Sherehe kubwa kabisa ni sikukuu za Iddi Al Haji na Iddi Al Fitri, kila mwaka kufikia wakati huo idadi ya watu wanaofanya ibada hapa haipungui watu elfu 70 au 80, watu wanakuwa wengi sana."
Bw. Cuma mowlanna alifahamisha kuwa, baada ya kuanzishwa kwa Jamhuri ya watu wa China, serikali kuu ya China na serikali ya mkoa wa Xinjiang zilifanya ukarabati wa msikiti huo mara 11, na kupanua eneo la uwanja mbele ya msikiti huo, ili kutoa urahisi mwingi zaidi kwa waislamu kufanya shughuli za kawaida za kidini.
Kashi iko kwenye sehemu ya magharibi mwa China, hivyo uchumi wake bado haujaendelezwa sana. Kwa hiyo kuwasaidia watu wenye uwezo mdogo na kuwasaidia Waislam kuondokana na umaskini, ni jambo kubwa la kwanza kwa chama na serikali ya China.
Bw. Haji Sabir ni mkazi wa kawaida, ana watoto watano, na maisha yao yalikuwa na taabu. Lakini kila mwezi serikali inatoa Yuan za RMB zaidi ya 500 kwa familia ya Bw. Sabir, ili kuhakikisha maisha yao.
Kuanzia mwaka 1999 mtaa anakoishi Bw. Sabir ulianza kutekeleza utaratibu wa kuhakikisha wa maisha ya kimsingi kwa wakazi, na familia zenye mapato ya chini ya Yuan za RMB 130 kwa mwezi zinaweza kupata ruzuku ya uhakikisho wa maisha ya kimsingi. Aidha wakazi wa mtaa huo wanashiriki kwenye bima ya matibabu, kila mwezi wanalipa Yuan za RMB 2 hadi 4 tu, na wakati wanapotibiwa wanapewa ruzuku ya matibabu ya asilimia 20 hadi asilimia 50 kutoka kwa serikali.
Katika mtaa huo, mwandishi wetu wa habari aliona kituo cha utoaji mafunzo ya ufumaji, na wasichana zaidi ya 10 walikuwa wanajifunza kufuma nguo. Kituo hicho kimekuwepo kwa zaidi ya miaka mitano, hadi sasa kimetoa mafunzo kwa watu zaidi ya 1,000, na vijana wa kike wa kabila la Waurgur wengi wamepata ajira baada ya kupewa mafunzo kwenye kituo hicho.
Msichana Patime mwenye umri wa miaka 16 alipata mafunzo kwenye kituo hicho kwa miezi mitatu, na alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, mafunzo yanatolewa hapo bila malipo.
Mwandishi wetu wa habari pia alifanya mahojiano na wasanii wa Mukamu. Mukamu ni aina moja ya muziki, ambayo inaoneshwa kwa mchanganyiko wa muziki, ngoma na nyimbo. Mwaka 2005 aina hiyo ya muziki ya Xinjiang iliorodheshwa kuwa "urithi wa utamaduni simulizi usioonekana" na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa. Wilaya ya Shache mjini Kashi ni maskani ya Mukamu, na mafanikio ya "kuomba kuwekwa kwenye orodha ya urithi" yameinua jina la Shache, na wasanii wa huko mara kwa mara wanaalikwa kufanya maonesho nje ya nchi.
Bw. Yusup Tohti alijifunza sanaa ya Mukamu kutoka kwa baba yake kuanzia utotoni. Hivi sasa yeye ni msanii pekee wilayani Shache anayeweza kupiga muziki wa seti zote 12 za usanii wa Mukamu. Katika miaka ya hivi karibuni, Bw. Yusup Tohti alifanya maonesho katika miji ya ndani ya China ikiwemo Suzhou na Beijing, pia alifanya maonesho nchini Japan, Uingereza na Pakistan. Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,
"Sasa usanii wa Mukamu umeelekea kwenye sehemu nyingine duniani, watu wanaweza kuona maonesho ya michezo ya sanaa ya Mukamu nchini Uingereza, Ujerumani, Japan na Ufaransa, na michezo ya sanaa ya Mukamu inayohifadhiwa vizuri kabisa iko kwenye wilaya yetu ya Shache."
Wilayani Shache kuna bustani ya kiutamaduni iliyojengwa ili kumkumbuka Bw. Amannisahan, ambaye ni mkusanyaji mkubwa na mpangaji wa michezo ya sanaa ya Mukamu. Kila asubuhi ya Ijumaa na Jumapili wasanii wa huko na wakazi wa huko wanakwenda kwenye bustani hiyo, kuonesha na kuburudishwa kwa michezo ya sanaa ya Mukamu. Sasa wilaya ya Shache imechagua wasanii 13 kuwa waalimu wa kufundisha wanafunzi watakaorithi michezo hiyo ya sanaa, tena imetenga fedha maalumu kwa ajili ya kujenga kituo cha mafunzo ya michezo hiyo ya sanaa.
Wasanii wanafurahia hatua zilizochukuliwa na serikali kwa ajili ya kuunga mkono urithi na maendeleo ya "Mukamu". Bw. Memet Tursun anafanya maonesho katika bustani kila wiki, yeye ni msanii wa kizazi cha 3 wa Mukamu. Alisema,
"Serikali inatoa uhakikisho wa kurithisha michezo ya sanaa ya Mukamu, tunafurahi sana. Sisi tunazeeka, na siku moja tutafariki dunia, lakini tunaamini kuwa michezo ya sanaa ya Mukamu hakika itaenziwa kizazi baada ya kizazi."
Idhaa ya kiswahili 2008-02-21
|