Msikilizaji wetu Mbaruk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za kiarabu ametuandikia barua pepe hivi karibuni akisema, Historia inatukumbusha kwamba katika enzi za "vita baridi" hatua za kususia tamasha kubwa kabisa la Michezo mbalimbali duniani yaani Olimpiki ilitumiwa kama ni njia moja wapo ya kisiasa, kwani kwa mara ya kwanza kabisa kususiwa kwa michezo hiyo kulitokea pale Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya nchi huru za Afrika ilipotishia kususia michezo hiyo kama timu kutoka utawala wa Kibaguzi nchini Afrika Kusini itaruhusiwa kushiriki, wakati Rais Jimmy Carter wa Marekani alitangaza nchi yake kususia michezo ya Olimpiki ya mwaka 1980 mjini Moscow kwenye Urusi ya zamani kwa sababu nchi hiyo iliivamia kijeshi Afghanistan mwaka 1979, wakati kambi ya Mashariki ililipiza kisasi pia kwa kususia michezo ya Olimpiki ya mwaka 1984 mjini Los Angeles Marekani. Hatua hizo za kisiasa zilimalizika pale tu Korea ya Kaskazini iliposhindwa kuzishawishi nchi kubwa za Kikomunisti za Jamhuri ya watu wa China, Urusi na Ujerumani Mashariki kususia michezo ya Olimpiki ya mwaka 1988 mjini huko Seoul Korea ya Kusini.
Hata hivyo Bw Mbaruk anasema kwa yeye msikilizaji wa muda mrefu wa Redio China Kimataifa na rafiki Mkubwa wa Watu wa China, ameingiwa na hofu sana, kwa vile tayari watu walipata tuzo ya Nobel, wanamichezo mashuhuri pamoja na wanasiasa mbalimbali wameanza kuendesha kampeni kubwa ya kutaka Michezo ya mwaka huu ya Olimpiki mjini Beijing China isusiwe, kwa kuwa Jamhuri ya Watu wa China imeshindwa kutumia ushawishi wake kwa Serikali ya Sudan kukomesha mgogoro wa Darfur.
Ni matumaini yake makubwa kwamba viongozi wa Jamhuri ya Watu wa China pamoja na Kamati ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing wataweza kushughulikia ipasavyo swala hili, ili kuepusha michezo ya Olimpiki kutumiwa kisiasa na kuitia dosari michezo hiyo, kwa vile dunia nzima inasubiri kwa hamu kubwa kuona tamasha hilo linafanyika katika hali ya mafanikio makubwa chini ya Mwito wa kauli mbiu ya "Dunia moja na ndoto moja " .
Tunakushukuru sana msikilizaji wetu Bw Mbarouk Msabaha, kwa maelezo yako mazuri kuhusu changamoto inayoikabili China katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing. Kama ulivyosema, hii si mara ya kwanza kwa baadhi ya watu kujaribu kuitumia michezo ya Olimpiki kwa sababu za kisiasa, lakini hata hivyo ni jambo la faraja kusikia kuwa watu wengi hawawaungi mkono watu hao wachache wanaojaribu kufanya hivyo.
Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa P.O. Box 504 Lindi, Tanzania ametuandikia barua akisema, anapenda kutuma salamu za pongezi kwa China kutokana na mafanikio yake ya kurusha kwa mara ya kwanza chombo cha kufanya utafiti kwenye sayari ya mwezi, na kujiandaa kurusha chombo kitakachoweza kwenda kutua kwenye sayari ya mwezi.. Kwa maoni yake anaona kuwa, si nchi nyingi zenye uwezo wa kufanikiwa kufanya utafiti kama huo, kwani ili kufanikisha kazi hiyo uchunguzi mkubwa unatakiwa kufanywa kwa makini, na kufanya kwa makini ili kufaulu bila haraka. Kwa upande wa pili anasema yeye bado hajastaafu kusukiliza matangazo yetu, bado yuko na Radio China Kimataifa, na anasikiliza Radio kama kawaida ila muda wa kukaa na kuandika barua unakuwa mfupi, lakini huwa anasikia wana salamu wenzake wakimsalimu, na anapenda kutumia njia hii kuwaomba radhi wote aliochelewa kuwajibu salamu zao, na anapenda kuwasalimu wote kwa pamoja.
Bwana Karim pia anasema ni kawaida yake kushiriki kwenye shindano la chemsha bongo kila mwaka, isipokuwa katika miaka miwili iliyopita hakuweza kushiriki kwenye chemsha bongo hiyo kutokana na sababu ambazo hazikuweza kuzuilika, lakini pia anasema kuwa safari hii amejizatiti vya kutosha na ana matarajio ya kupata nafasi ya mshindi maalum au mshindi wa kwanza.
Bwana Karim anasema Jumapili ya tarehe 11 mwezi Novemba mwaka jana ulisikiliza makala ya kwanza, na tayari amerekodi maswali mawili, wakati anaandika barua hii alikuwa akisubiri kusikia makala nyingine na maswali mengine. Anaomba tumtumie fomu ya kushiriki, na vipeperushi vya michezo ya Olimpiki ya 2008 ambayo yataanza mwezi Agosti 2008 hapa Beijing. Kwa kuwa yeye ni msikilizaji mkongwe anatarajia kupata nafasi fulani ya upendeleo. Na mwisho anasema alijitahidi sana kufuatilia maendeleo ya maonesho ya mrembo wa dunia yaliyofanyika mjini Sanya, mkoani Hainan kusini mwa China lakini bahati haikuwa kwa Tanzania.
Tunakushukuru sana Bw Gulam Haji Karim kwa barua yake, Tumefurahishwa sana na barua yake, japokuwa imechelewa kutufikia. Kweli tunaelewa pilikapilika alizokuwa nazo mwaka jana, lakini hata hivyo alivyopata nafasi alijitahidi kuwasiliana nasi. Na kuhusu ushiriki wako wa shindano la chemsha bongo, tunakutakia kila la heri, lakini tunaomba wewe na wasikilizaji wetu wengine mkumbuke kuwa kamati ya uchaguzi ndiyo inayohusika na kuchagua washindi, na kamati hiyo kwa kweli haina upendeleo, kwa hiyo nafasi ya ushindi iko sawa kwa kila msikilizaji.
Msikilizaji wetu wa Kenya Bw. Jonathan Ngari ambaye hakuandika anuani yake ametuletea barua pepe hivi karibuni akisema huko Narok Kenya anaendelea kusikia matangazo yetu vizuri na kupata salamau kutoka kwa wasikilizaji wenzake. Akiwa Narok anapenda kuwasalimu wasikilizaji wenzake na ndugu zake wa kule Kasigau, Taita Kenya, wanafunzi wa chuo cha ualimu Narok, watu wa familia yake wakiwa huko Nyeri Kenya, na ujumbe anasema anawataka wote wasikilize Radio China Kimataifa.
Na kwenye barua pepe nyingine tuliyoipata hivi karibuni, msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai Falme za Kiarabu anaomba tumpeperushie salamu zake kwa.Mzee Gulam Haji Karim wa Lindi Tanzania, Brown Girl" Rukiya Mohammed wa Riyadh Saudi Arabia, Yahya Hassan Shebe wa Mombasa Kenya, Mogire Machuki, Kepher Gichana na Philip Machuki hawa wako Kisii Kenya, Yakub Saidi Idambira na Mbaraka Mohammed Abucheri wote wakiwa Kakamega Kenya
Idhaa ya kiswahili 2008-02-26
|