Zamani kijiji cha Matouchuan cha wilaya ya Longxi mkoani Gansu, China kilikuwa ni kijiji kilicho nyuma kiuchumi. Lakini katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na mfuko wa kusaidiana wa ngazi ya kijiji kwa ajili ya maendeleo, maisha ya wanakijiji wa kijiji hicho yanaboreshwa siku hadi siku, na sura ya kijiji imebadilika kuwa nzuri.
Mwaka 2006 serikali ya China ilichagua mikoa 14 ikiwemo Gansu na Xinjiang ambayo iko nyuma kiuchumi, kufanya majaribio ya kuanzisha mfuko wa kusaidiana wa ngazi ya kijiji kwa ajili ya maendeleo, yaani kutenga kiasi fulani cha fedha na kuanzisha mfuko wa kusaidiana katika vijiji kadhaa mikoani humo, na wanavijiji wanakopa fedha hizo ili kuendeleza uzalishaji. Kijiji cha Matouchuan kilichaguliwa kuwa ni moja kati ya vijiji vya majaribio ya kuanzisha mfuko huo.
Tukiingia kwenye kijiji cha Matouchuan, tunaweza kuona maneno makubwa yaliyoandikwa kando ya barabara "mfuko wa kusaidiana wa ngazi ya kijiji kwa ajili ya maendeleo ni benki ya watu wenye matatizo ya kiuchumi". Mkuu wa ofisi ya kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi wa wilaya ya Longxi Bw. Zhang Jing alisema, mwanzoni mwa mwaka 2006, wilaya hiyo ilianzisha mfuko huo kwenye vijiji vitano vilivyoko nyuma kiuchumi kikiwemo kijiji cha Matouchuan, yaani serikali ilitenga Yuan laki 1.5 kwa kila kijiji, na iliwahimiza wanavijiji kununua hisa kwa fedha zao. Wakulima waliojiunga na mfuko huo wanaweza kuomba mikopo yenye riba ndogo kuliko mikopo ya benki. Bw. Zhang Jing alisema lengo la kuanzisha mfuko huo ni kutatua upungufu wa fedha kwa wakulima wenye matatizo ya kiuchumi, na kuinua uwezo wa kujiendeleza na kupata maendeleo endelevu ya vijiji vilivyoko nyuma kiuchumi, na familia zenye matatizo ya kiuchumi. Bw. Zhang Jing alisema,
"Tunaendesha mfuko huo kutokana na mawazo ya uaminifu na usimamizi wa kidemokrasia. Kupatikana kwa ufanisi wa mfuko huo kutakuwa ni mchakato wa muda mrefu"
Baada ya serikali kutenga Yuan laki 1.5, wanakijiji wa kijiji cha Matouchuan wengi walinunua hisa za mfuko huo kwa Yuan 400 hadi Yuan elfu 2. Wanakijiji pia walichagua kamati ya usimamizi ili kusimamia na kukagua kazi za mfuko huo. Wanakijiji walionunua hisa wanaweza kuomba mikopo ya Yuan elfu 3 ya muda usiozidi mwaka mmoja ili kushughulikia kazi za upandaji wa mazao na ufugaji. Mwanzoni mwa mwaka 2007, mfuko huo ulikuwa na fedha karibu Yuan laki 3, na wakulima 120 wamejiunga na kwenye mfuko huo.
Katika kijiji cha Matouchun, mwandishi wetu alikutana na wanakijiji wawili walioomba mikopo kutoka kwenye mfuko huo. Bw. Wang Youde na mkewe walikuwa katika kiwanda cha kutengeneza unga wa ngano. Walijiunga na mfuko huo wakati kijiji hicho kilipoanzisha mfuko huo mwaka 2006. Mke wake Bibi Zhang Taohua alisema,
"Riba ya mikopo ya mfuko wa kusaidiana ni ndogo kuliko riba ya mikopo ya benki, na ni rahisi zaidi kuomba mikopo ya mfuko huo."
Wakulima wakitaka kuomba mikopo benkini, wanatakiwa kutafuta dhamana, kujaza fomu mbalimbali, na kulipa riba kubwa. Lakini mfuko wa kusaidiana wa ngazi ya kijiji kwa ajili ya maendeleo umeondoa matatizo hayo. Bw. Wang Youyu alisema wakulima wakinunua hisa za mfuko huo, wataweza kuomba mikopo. Mwanzoni mwa mwaka 2007, alitumia mkopo wa Yuan 3000 na fedha zake Yuan 7000 kununua mashine nzuri zaidi ya kutengeneza unga wa ngano. Ufanisi wa mashine mpya ni mkubwa zaidi, na mapato ya familia yake yameongezeka. Alisema,
"sasa hatuna matatizo makubwa tunapotaka kununua chakula au nguo mpya kwa ajili ya watoto,."
Watoto watatu wa Bw. Wang Youyu wanasoma wilayani, ambao wanatumia fedha nyingi. Bw. Wang alisema mwaka 2007 familia yake ilipata Yuan elfu 20 kwa kutengeneza unga wa ngano na kupanda mitishamba, na hali ya maisha ya familia yake kwa sasa ni nzuri zaidi kuliko ilivyokuwa miaka iliyopita.
Bw. He Junming mwenye umri wa miaka 67 aliomba mkopo wa Yuan 3000 ili kufuga nguruwe. Bw. He Junming alisema licha ya kilimo cha mahindi, sehemu kubwa ya mapato ya familia yake inatokana na ufugaji wa nguruwe. Mwanzoni mwa mwaka jana, bei ya chakula cha nguruwe iliongezeka, na wakati huo hakukuwa na fedha za kutosha kununua chakula cha nguruwe, na alikuwa na wasiwasi kubwa. Alipotaka kuomba mkopo kwenye benki, kiongozi wa kijiji alikuja na kumwambia kuwa kijiji hicho kimeanzisha mfuko wa kusaidiana kwa ajili ya maendeleo, na anaweza kujiunga na mfuko huo. Baada ya kufahamu habari husika, Bw. He alitoa ombi la mkopo wa Yuan 3000 kutoka kwa mfuko huo.
Bw. He alipoona nguruwe walivyokula kwa furaha, tena bei ya nyama ya nguruwe imepanda juu sana, aliushukuru sana mfuko huo. Alisema baada ya miezi miwili hadi mitatu, uzito wa kila nguruwe utakuwa zaidi ya kilo 100, baada ya kuuza nguruwe hao, ataweza kulipa mkopo. Alieleza kuwa mfuko huo unawasaidia sana wakulima, akisema,
"Mfuko huo ni mzuri sana, na umetupatia sisi wakulima manufaa makubwa."
Licha ya kijiji cha Matoucun, wanavijiji wengi wa vijiji vingine vinne vinavyoendeleza mfuko wa kusaidiana kwa ajili ya maendeleo wilayani Longxi wamenunua hisa ya mfuko huo, na fedha za mfuko huo zimekuwa nyingi zaidi. Habari zinasema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2007, katika vijiji hivyo vitano, wakulima wa familia zaidi ya 500 zenye matatizo ya kiuchumi walipata mikopo ya Yuan milioni 1.3, walitumia fedha hizo kwa ajili ya ufugaji, utengenezaji na uchukuzi, na hali ya maisha yao imeboreshwa zaidi.
|