Katika kipindi hiki tunawaelezea sera mbalimbali mpya za uhakikisho wa huduma za matibabu zinazotekelezwa huko Hangzhou, mji wa pwani wa mashariki mwa China.
Bw. Liu Jianxing kutoka mkoa wa Jiangxi ni mfanyakazi wa kampuni moja binafsi mjini Hangzhou. Mwaka 2006 aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa uremia, na alikuwa anapaswa kupewa matibabu ya hemodialysis mara mbili kila wiki ili kudumisha maisha yake. Matibabu hayo yanagharamu Yuan elfu 6 kila mwezi, ambayo ni mzigo mkubwa kwa familia ya Bw. Liu Jianxing yenye pato la jumla la Yuan elfu 3 kila mwezi. Lakini la kufurahisha ni kwamba kutokana na sera moja mpya inayoanza kutekelezwa mwaka huu, Bw. Liu Jianxing anaweza kupata bima ya matibabu ya magonjwa makubwa kama wakazi wa kawaida wa mji huo kwa kulipa Yuan mia moja hivi kila mwezi. Bw. Liu Jianxing alisema:
"hata sijui ningefanya nini bila bima hiyo. Kama sikushiriki kwenye bima hiyo, ugonjwa wangu usingetibiwa."
Ingawa hivi sasa Bw. Liu Jianxing bado anakabiliana na shinikizo la kiuchumi, lakini bima hiyo ya matibabu imempa ushupavu kupambana na ugonjwa huo na kupigania maisha yake. Hivi sasa mama yake ameamua kuhamishiwa figo yake moja kwa Bw. Liu Jiangxing. Gharama za matibabu na upasuaji huo pia zitalipiwa kutokana na bima hiyo ya matibabu.
Mwaka 2001 mji wa Hangzhou ulianza kutekeleza utaratibu wa bima ya matibabu kwa wafanyakazi wa mijini. Lakini hadi kufikia kabla ya mwaka 2007, wafanyakazi na watoto wao wanaotoka sehemu nyingine na baadhi ya wazee bado hawakunufaika na utaratibu huo, na mara kwa mara watakuwa na wasiwasi wa maisha kutokana na gharama za matibabu.
Bi. Zhao Caiyun mwenye umri wa miaka 71 alikwenda Hangzhou na mume wake baada ya kustaafu kutoka kwenye kampuni moja ya mkoa wa Liaoning miaka 20 iliyopita. Mume wake ananufaika na utaratibu wa bima ya matibabu kwa wafanyakazi wa Hangzhou, lakini kutokana na kampuni aliyofanya kazi Bi. Zhao Caiyun iko mbali na imefungwa, katika miaka zaidi ya 20 iliyopita, Bi. Zhao Caiyun hakulipiwa hata senti moja ya gharama zake za matibabu. Ingawa ana ugonjwa wa kuwa mawe ndani ya nyongo kwa muda mrefu, lakini kwa kawaida hakwenda hospitali kupewa matibabu. Bi. Zhao Caiyun alisema:
"niligunduliwa kuwa na ugonjwa huo zaidi ya miaka 10 iliyopita, nimeendelea kutumia dawa ili kudhibiti hali ya ugonjwa huo. Lakini mara hii imezidi kuwa mbaya, hata nilishindwa kuvumilia maumivu. Kwa hivyo nililazwa hospitalini, na ni wakati huo ndipo nilipata fursa ya kushiriki kwenye bima ya matibabu ya magonjwa makubwa."
Bima hiyo aliyotaja Bi. Zhao Caiyun ni bima ya matibabu ya magonjwa makubwa kwa wakazi wazee iliyoanza kutekelezwa tarehe 1 Aprili mwaka 2007. Kwa mujibu wa utaratibu huo mpya, wakazi wazee ambao hawakushiriki kwenye bima ya matibabu ya kimsingi, wote wanaweza kushiriki kwenye bima hiyo.
Kwa mujibu wa bima hiyo, wakati Bi. Zhao Caiyun alipoondoka hospitalini matibabu yake yaligharimu zaidi ya Yuan elfu 24, na Yuan elfu 9 kati ya gharama hizo zililipwa na bima. Utaratibu huo kweli umeleta manufaa halisi kwa wakazi wa mji huo.
Kuanzia mwaka 2001, utaratibu wa uhakikisho wa huduma za matibabu wa mji wa Hangzhou umeendelea kukamilika hatua kwa hatua. Mwaka 2007 sera nyingi husika zilitolewa. Kuanzia tarehe 1 Septemba mwaka huu mji huo pia utaanzisha utaratibu wa bima ya matibabu ya magonjwa makubwa kwa watoto, watoto zaidi ya laki tatu ambao hawashiriki kwenye bima ya kawaida ya matibabu watashiriki kwenye utaratibu huo. Mkurugenzi wa uhakikisho wa huduma za matibabu wa Hangzhou Bw. Chen Zhengxiang alisema:
"baada ya kutolewa kwa utaratibu huo, sera za matibabu zinawafikia wakazi wote wanaoishi na kufanya kazi mjini Hangzhou, kila mtu ataweza kushiriki kwenye bima ya huduma ya matibabu."
Mtafiti wa taasisi ya sayansi ya jamii ya mkoa wa Zhejiang profesa Yang Jianxin anaona kuwa, sera hizo ni hatua moja iliyopangwa kuwanufaisha wananchi kwa mafanikio yaliyopatikana katika maendeleo ya nchi yetu. Profesa Yang Jianxin.
Ingawa hali ya hivi sasa ya mjini Hangzhou imeboreka kidhahiri, lakini bado kuna matatizo mengi yanayohitaji kutatuliwa ili kutimiza lengo la kunufaisha kila mkazi kwa uhakikisho wa matibabu. Kwa kuwa uhakikisho unaotolewa hivi sasa bado haujahusisha gharama zote za matibabu, na bima ya matibabu bado inaweza tu kuwanufaisha wakazi wa mjini. Lakini mkurugenzi wa kituo cha uhakikisho wa matibabu cha mji wa Hangzhou Bw. Chen Zhengxiang alisema, idara za serikali zimepanga kuunganisha utaratibu wa uhakikisho wa huduma za jamii mijini na vijijini.
Tunaamini kuwa sera hiyo itaendelea kukamilika, tanufaisha watu wengi zaidi kwenye sehemu kubwa zaidi, na kiwango cha uhakikisho wake pia kitainuka hatua kwa hatua ili kutimiza lengo la kunufaisha kila mtu kwa bima ya matibabu.
|