Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-02-29 14:41:28    
Ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya viwanda binafsi vya China na Afrika waendelezwa kwa kasi

cri

Mji wa Yixing uko kusini mwa mkoa wa Jiangsu, kwenye sehemu ya ziwa Taihu ya Delta ya Mto Changjiang. Viwanda binafsi mjini Yixing viliendelezwa tangu miaka ya 90 karne iliyopita, na kiwango cha maendeleo ya viwanda binafsi mjini Yixing kinachukua nafasi ya mbele mkoani Jiangsu. Katika miaka ya hivi karibuni, viwanda vingi vyenye nguvu vilianza kutilia maanani masoko ya nchi za nje yenye fursa nyingi, hasa bara la Afrika lililo na urafiki wa jadi na China. Mwandishi wetu wa habari hivi karibuni alifanya mahojiano na mkurugenzi wa idara ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi za nje ya mji wa Yixing Bw. Jiang Guoqiang.

Bw. Jiang alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, katika kipindi cha mwanzo cha maendeleo ya viwanda binafsi, kufanya biashara na nchi za Afrika kulikuwa ni lengo lisiloweza kutimizwa, kwani bara la Afrika liko mbali sana na China, vilevile viwanda hivyo kwa wakati huo havikuwa na nguvu kubwa. Lakini kutokana na maendeleo ya kasi ya viwanda binafsi katika miaka zaidi ya kumi iliyopita, nguvu ya viwanda binafsi ilizidi kuongezeka siku hadi siku, na mawasiliano na ushirikiano kati yao na nchi za nje pia vilizidi kuongezeka. Katika miaka ya hivi karibuni, ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya viwanda binafsi vya Yixing na nchi za Afrika uliendelezwa kwa kasi. Bw. Jiang Guoqiang alisema, "Katika miaka ya hivi karibuni, maendeleo ya biashara kati ya mji wa Yixing na nchi za Afrika yalidumisha mwelekeo mzuri. Thamani ya bidhaa zilizouzwa na mji wa Yixing barani Afrika katika mwaka 2005, 2006 na 2007 ilifikia dola za kimarekani milioni 27, milioni 30, na milioni 50, na kuongezeka kwa asilimia 21, asilimia 13 na asilimia 66. Hasa katika mwaka 2007 thamani ya bidhaa zilizouzwa barani Afrika iliongezeka kwa kasi, ongezeko hilo lilikuwa kubwa kwa asilimia 27 kuliko thamani ya jumla ya bidhaa zilizouzwa na mji wetu barani Afrika katika miaka ya nyuma. "

Bw. Jiang alijulisha kuwa sekta za kemikali, nguo, bidhaa za ubao na mashine ya za umeme mjini Yixing ni sekta muhimu katika biashara kati yake na bara la Afrika. Bw. Jiang aliona kuwa katika miaka ya hivi karibuni kasi ya ongezeko la biashara kati ya mji wa Yixing na Afrika ilinufaishwa na ongezeko la nguvu za viwanda binafsi kwenye sehemu hiyo. Alisema katika miaka ya hivi karibuni uchumi wa China umekuwa ukiendelezwa kwa kasi, ikiwa nguvu muhimu ya uchumi ya sehemu ya Delta ya Mto Changjiang, viwanda binafsi pia viliendelezwa kwa kasi, na nguvu yake ilizidi kuongezeka siku hadi siku, hivyo vinahitaji soko kubwa zaidi. Na bara la Afrika linaweza kutoa fursa nyingi kwa maendeleo ya viwanda hivyo. Wakati huo huo, maendeleo mapya ya uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika katika karne mpya yanaunga mkono maendeleo ya viwanda hivyo barani Afrika. Bw. Jiang alisema,"Ongezeko la biashara kati ya viwanda binafsi na nchi za Afrika linategemea urafiki wa jadi uliopo kati ya China na Afrika. Kutokana na urafiki huo, mawasiliano ya kibiashara kati ya viwanda vya China na nchi za Afrika yaliendelezwa bila matatizo. Vilevile mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika ulitoa fursa nyingi, na viwanda vya China vilihimizwa kufanya ushirikiano na nchi za Afrika."

Bw. Jiang alisema msingi wa viwanda mjini Yixing ni mzuri, na bidhaa za viwanda za mjini Yixing zina sifa nzuri na bei nafuu. Bara la Afrika ni soko jipya linaloendelea, kiwango cha biashara kati yake na nchi za nje kinainuka siku hadi siku, na mahitaji ya bidhaa pia yanaongezeka. Bw. Jiang alisema, kutumia raslimali na nguvu kazi za huko, kuanzisha viwanda barani Afrika, si kama tu kunaweza kukidhi mahitaji ya huko kwa bidhaa na teknolojia, bali pia kunaweza kusaidia utatuzi wa suala la ajira, hii inazinufaisha pande hizo mbili, hivyo kuwekeza barani Afrika kumekuwa ni maoni ya pamoja ya viwanda vya China. Bw. Jiang alisema,"Viwanda husika vinapaswa kutumia fursa hiyo, vinaweza kutumia mkopo wa kuhimiza uuzaji ili kuongeza idadi ya bidhaa zinazosafarishwa nje, pia vinaweza kutumia sera nafuu za China kwa Afrika kufanya biashara."

Hivi sasa viwanda kadhaa mjini Yixing vimechukua bara la Afrika kuwa sehemu muhimu ya uwekezaji. Katika mwaka 2006 na mwaka 2007, viwanda vinne vya mjini Yixing viliwekeza barani Afrika. Kiwanda cha kebo cha Jiangnan kilianzisha kiwanda cha kebo cha Jiangnan cha Afrika ya Kusini, kiwanda cha Cableway cha Yixing kilianzisha kiwanda nchini Misri, kampuni ya utalii ya Fantai ilianzisha kampuni nchini Nigeria, na kiwanda cha kauri cha Mingyue cha Yixing kilianzisha kiwanda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Viwanda hivyo vilianzisha shughuli zao barani Afrika, na viliweka mfano mzuri kwa viwanda vingine nchini China, na kuongeza imani kwa viwanda vingine vya China kupata maendeleo barani Afrika.

Katika mchakato wa kufanya biashara na nchi za nje kwa viwanda hivyo vya China, ikiwa shirika la usimamizi wa mambo ya biashara kwa nje, idara ya ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi za nje imeunga mkono na kuvisadia viwanda hivyo. Bw. Jiang alisema, "Tuliunga mkono viwanda hivyo kufanya ushirikiano na nchi za Afrika, na tulivipatia fedha maalumu kwa ajili ya kuvisaidia viwanda hivyo kushughulikia biashara kwenye soko jipya, kwa mfano tulitoa ruzuku kwa mabanda kwenye maonesho, na kutoa tuzo kwa uandikishaji wa nembo za bidhaa kwenye nchi za nje. Vilevile tulivihimiza viwanda kuwekeza barani Afrika, tulitangaza sera za serikali kuhusu kuwekeza barani Afrika, na kutoa huduma za habari kwa viwanda vitakavyotaka kuwekeza barani Afrika. "

Bw. Jiang ana imani na mustakabali wa maendeleo ya viwanda binafsi vya China barani Afrika. Alisema biashara kati ya viwanda binafsi na nchi za Afrika itahimiza viwanda hivyo kuanzisha viwanda barani Afrika, hii itakuwa ni njia muhimu ya maendeleo ya viwanda hivyo barani Afrika. Alisema,"Nafikiri mustakabali wa njia hiyo ni mzuri sana. Hivi sasa kwenye nchi mbalimbali za Afrika hasa kusini mwa Afrika, ujenzi wa miundo mbinu unaendelea kwa utaratibu, hivyo mahitaji ya vifaa vya ujenzi na miundo mbinu ya umeme ni makubwa. Kiwanda cha kebo cha Jiangnan kina bidhaa zenye sifa nzuri, na bidhaa zake zimechukua sehemu kubwa ya soko la kusini mwa Afrika. Hakika kitaanzisha kiwanda kingine nchini Afrika ya Kusini mwaka 2008."

Bw. Jiang alisema nchi nyingi barani Afrika ni nchi zinazoendelea, ambazo zinataka kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara na nchi za nje, na ukweli wa mambo unaonesha kuwa ushirikiano kati ya China na Afrika ni wa kunufaishana. Kutokana na maendeleo ya uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika, mawasiliano na ushirikiano wa kibiashara kati yao utaimarishwa, bila shaka viwanda vya sehemu ya Delta ya Mto Changjiang vitaimarisha biashara na uwekezaji barani Afrika, na mustakabali wa ushirikiano kati yao na nchi za Afrika utakuwa mzuri zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2008-02-29