Michezo ya 29 ya Olimpiki itafanyika hapa Beijing katika majira ya joto ya mwaka huu. Mji mkuu wa Beijing wenye historia ya miaka 3,000 unavutia watalii wengi zaidi kuutembelea mji huu kwa uzuri na vivutio vyake. Katika kipindi hiki cha leo, tunawatembeza kwenye Hutong mjini Beijing, ambavyo ni vichochoro vyembamba kwenye maeneo ya nyumba za wakazi, ili tuwawezeshe kufahamu mazingira ya jadi ya mji wa kale wa Beijing.
Kwenye mji mdogo wa Wanping, ambao uko karibu sana na daraja la Lugou lililoko kwenye sehemu ya magharibi ya Beijing, kuna jumba moja la makumbusho ya mila na jadi ya wakazi wenyeji wa Beijing. Jumba hilo la makumbusho ni jumba binafsi lililoanzishwa na mkazi mwenyeji wa Beijing ambaye ni shabiki wa utamaduni wa jadi wa kibeijing. "Hutong" ni uwakilishi wa utamaduni wa jadi wa kibeijing, na "Zhang" ni jina la ukoo la mwenye jumba hilo la makumbusho. Eneo la maonesho ya jumba hilo la makumbusho ni mita za mraba zaidi ya 700, ambalo limekusanya vitu vya kazi za sanaa za mikono na vitu zaidi ya elfu moja vya jadi vya kuchezea watoto, pamoja na picha zaidi ya 100 kuhusu historia.
Mara tu baada ya kuingia kwenye jumba la makumbusho la "Hutong Zhang", utaweza kusikia sauti ya uimbaji wa Jinyundagu, ambayo ni aina ya opera, mwimbaji huku anaimba huku akipiga ngoma, na pia utaweza kuona vitu vingi vya jadi vya zamani, ambavyo hivi sasa viko tu vichwani mwao. Wafanyakazi wa jumba la makumbusho wanapoeleza kuhusu vitu hivyo wanavyohifadhi, kama wanaeleza vitu vyao vyenye thamani kubwa, hususan kile kinachoitwa "Umaalumu wa Beijing", ambacho ni kielelezo cha mtaa wa zamani wa Beijing, ambacho kimepangwa kwenye urefu wa mita 100 hivi, kikieleza utamaduni wa mila ya wakazi wa miaka ya 20 na 30 wa Beijing, na kuonesha maisha halisi ya wakazi wenyeji wa Beijing. Kielelezo hicho ni pamoja na maduka maarufu ya zamani zaidi ya 140 yakiwemo ya kuuza mafuta na chumvi, nyuzi za sufu, nguo...... ambayo yanafanana na maduka maarufu ya zamani yaliyopo hivi sasa. Kwenye mtaa huo, vinaoneshwa zaidi ya aina kumi za vyombo vya usafiri vya zamani, sanamu mbalimbali za watu za udongo wa mfinyanzi zinazoonekana kama watu hai waliovaa nguo za aina mbalimbali tofauti. Watu wakisikiliza maelezo ya mfanyakazi wa jumba la makumbusho yaliyotolewa kwa matamshi halisi ya kibeijing, watazamaji hujisikia kama wako kwenye mtaa wa zamani wa Beijing ya kale.
"Kiko Kikubwa kinamaanisha duka la Tianhecheng linalouza nyuzi za sufu, kwanini duka hilo linaitwa Kiko Kikubwa? Sababu yake ni kuwa hapo zamani wanawake hawakujua kusoma, hivyo walipokwenda kwenye mtaa wa Huashi kutafuta duka la Tianhecheng, mara kwa mara walikosea na kwenda kwenye maduka mengine, mwenye duka alikuwa na wasiwasi wa kukosa biashara, hivyo alitundika kiko kikubwa mlangoni mwa duka lake, baada ya hapo watu waliotaka kwenda kwenye duka hilo walijua kuwa duka hilo ndilo wanalotaka kwenda"
Kielelezo cha mtaa huo kinachofanana na mtaa halisi wa zamani wa Beijing ya kale, kilitengenezwa na mkuu wa jumba hilo la makumbusho, Bw. Zhang Yujun kwa muda wa zaidi ya miaka kumi. Bw. Zhang Yujun mwenye umri wa miaka 47 mwaka ule, alikuwa mfanyakazi wa uchoraji michoro katika posta. Kutokana na kupenda mno utamaduni wa jadi wa kibeijing, aliacha kazi yake hiyo, na alitumia fedha zake zote kujenga jumba la sanaa. Sanamu za udongo wa ufinyanzi zilizooneshwa kwenye kielelezo cha mtaa wa zamani, pia zilifinywngwa na yeye mwenyewe, alijitahidi sana na kupatwa na taabu nyingi katika kutafuta vitu vya kizamani vilivyotumiwa na wakazi wenyeji wa zamani. Alipoeleza kuhusu kielelezo chake hicho, Bw. Zhang Yujun alisema,
"Hata kielelezo kilipokuwa katika hali ya mwanzo, niliona vigumu kuondoka pale. Ninajisikia niko katika enzi ile kabisa. Nilitembea mara nyingi kwenye mtaa huo wa kielelezo, na kila mara nilijisikia hali tofauti. Ninaona kielelezo hicho ni kizuri na cha kuvutia sana, ninajisikia niko kabisa katika enzi ile."
Licha ya kuweko kwa vitu vingi vizuri vya kutazamwa, pia kuna vitu vingi vya kimichezo. Katika jumba la makumbusho la "Hutong Zhang" watazamaji wanaweza kuchezea vitu vya kimichezo vya kizamani, na kujiburudisha kwa maisha ya wakazi wenyeji wa zamani wa Beijing. Watazamaji wanafurahishwa na vitu hivyo, hususan kwa vitu vya kuchezea vilivyotumiwa katika miaka ya 50 na 60 vya mjini Beijing.
Watazamaji wakichoka wanaweza kwenda kwenye ghorofa ya juu kusikiliza opera ya kibeijing na kula chakula chepesi cha jadi cha Beijing. Watu wanaokwenda kutembelea jumba hilo la makumbusho, hupenda kutumia muda wa siku nzima. Bw. Matti Leirimaa kutoka Finland ni mmoja kati ya watazamaji wa aina hiyo, alisema.
"Rafiki yangu alinifahamisha kuhusu matembezi hayo, leo ni mara yangu ya nne kutembelea jumba hilo la makumbusho katika muda wa nusu mwaka uliopita, ninapenda sana kutembelea hapa. Ninaweza kuona majengo ya kizamani.........pia ninaweza kucheza baadhi ya michezo ya kizamani ya Beijing. Katika nchi yangu Finland pia kuna majumba mengi ya makumbusho ya binafsi, ninatarajia wageni wengi zaidi watapajua na kupapenda hapa, hapa ni mahali pazuri sana. Ninapenda sana jumba hili la 'Hutong Zhang'!"
"Hutong Zhang" ni jumba la makumbusho binafsi, ni shida kuliendesha kwa kutegemea nguvu za mtu mmoja, kwa hiyo jumba hilo la makumbusho linapewa misaada mara kwa mara kutoka kwa watu wa sekta mbalimbali za jamii wanaoupenda utamaduni wa jadi wa Beijing, baadhi ya watu walitoa mchango wa vitu vya kizamani walivyohifadhi kwa miaka mingi, baadhi ya wasanii walitoa zawadi za michoro na vitu walivyotengeneza, licha ya hayo, kuna watu kadha wa kadha wanaojitolea kufanya kazi katika jumba la makumbusho, kijana Zhang Jun, ambaye alimfahamisha Bw. Matti Leirimaa kuhusu jumba hilo la makumbusho, alisema,
"Hivi sasa mimi ni mfanyakazi wa hapa ninayejitolea, hapo mwanzoni mimi nilikuwa ni mtazamaji pia, ninapenda utamaduni wa China, tena nimekulia kwenye Hutong hiyo, niliona utamaduni wa Hutong na Siheyuan, ambayo ni nyumba ya jadi yenye ua kwenye sehemu ya kati ya wenyeji kabisa wa Beijing, ulikuwa unafifia mwaka hadi mwaka, hivyo nilihisi ninabeba jukumu la kuzuia hali hiyo isiendelee."
Mkuu wa jumba la makumbusho, Bw. Zhang Yujun pamoja na wafanyakazi wanaojitolea wa huko, wanajitahidi kuimarisha na kuboresha jumba hilo la makumbusho, wanatarajia kuwa kutakuwa na watazamaji wengi zaidi watakaotembelea "Hutong Zhang", na kutakuwa na watu wengi zaidi wanaofuatilia utamaduni wa jadi wa Beijing. Alisema,
"Tufanye wakazi wa Beijing wapende zaidi Beijing; tunatarajia wakazi wa mikoa mingine waifahamu zaidi Beijing; tunatarajia kuwa wachina wanaoishi nchi za nje waje Beijing kutafuta mambo ya kikwao; na tunatarajia kuwa wageni kutoka nchi za nje watakuja kuangalia dunia ya mashariki ya kale na ngeni".
Idhaa ya kiswahili 2008-03-10
|