Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita China ilipoanza kufanya mageuzi ya kiuchumi mwimbaji Bi. Zheng Xulan aliishangaza China nzima kutokana na mtindo wake tofauti wa uimbaji wa nyimbo kwa sauti yake nyororo. Ingawa maisha yake yaliwahi kuwa ya taabu nyingi, lakini siku zote alikuwa anakabiliana nazo kwa nia imara. Alisema alizaliwa kwa ajili ya muziki na ataimba nyimbo katika maisha yake yote.
Siku chache zilizopita kwenye likizo ya sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China alifanya maonesho binafsi ya nyimbo yanayoitwa "kukumbuka miaka iliyopita" na kuadhimisha miaka 30 ya ushiriki wake kwenye usanii.
Bw. Zhang Hanzhong aliyewahi kusikiliza nyimbo zake miongo kadhaa iliyopitaalisisimka sana aliposikia tena nyimbo zake. Alisema nyimbo za Bi. Zheng Xulan ziliwahi kuwa na athari kwa watu ambao sasa wamekuwa na umri wa zaidi ya miaka hamsini, na kutokana na kupenda nyimbo zake amekuwa rafiki yake. Alisema,
"Tunaposikiliza tu nyimbo zake, mara tunavutiwa na sauti yake nyororo, hasa wimbo wake wa 'Mchunga Kondoo' na 'Kwenye Kisiwa cha Jua'. Kutokana na wimbo huo watu wengi walikwenda kwenye kisiwa hicho."
Mwaka 1977 Bi. Zheng Xulan aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari alijiunga na Kundi la Nyimbo na Dansi la Dongfang. Hili ni kundi la wasanii linaloshughulika na maingiliano ya kiraia ya sanaa kati ya China na nchi za nje. Katika miaka mingi baadaye alikuwa mmoja kati ya wasanii wakubwa katika kundi hilo. Bi. Zheng Xulan alisema mwaka 1979 alipoanza kuimba jukwaani alibahatika kupata nafasi ya kuimba wimbo unaoitwa "Kwenye Kisiwa cha Jua". Huu ni wimbo unaosifu mandhari nzuri ya Kisiwa cha Jua kilichopo karibu na mji wa Harbin, kaskazini mashariki mwa China. Wakati huo ambapo kutokana na sababu fulani hali ya michezo ya sanaa nchini China ilikuwa michache, Wachina waliposikia wimbo kama huo walishtuka na kuvutiwa sana, baadaye wimbo huo ulichaguliwa kuwa moja ya "nyimbo 15 zinazopendwa sana" nchini China. Tokea hapo Bi. Zheng Xulan alianza kupata mafanikio mengi mfululizo. Alisema mafanikio yake yalipatikana kutokana na kuwa na bahati. Alisema,
"Sikutegemea kama ningepata bahati ya kurekodi wimbo wa 'Kwenye Kisiwa cha Jua' katika kituo cha redio, na baada ya wimbo huo kutangazwa, mara wasikilizaji wote nchini China waliupenda sana, nilijipongeza kwa kuwa na bahati na nathamini sana sifa niliyopata."
Baada ya kuwa maarufu Bi. Zheng Xulan alirekodi nyimbo nyingi na amekuwa na mtindo pekee wa uimbaji. Aliwahi kwenda Thailand, Philippines na Malaysia kujifunza uimbaji wa huko. Alipokuwa katika nchi hizo, mwanzoni hakuweza kuwasiliana na watu wengine kutokana na tatizo la lugha, lakini baadaye aliweza kuimba nyimbo za nchi hizo hata watazamaji walifikiri yeye ni mwimbaji wa nchi yao. Hivyo alikuwa akijifunza, kuimba, kurekodi na kufanya maonesho katika nchi za nje kwa miaka mingi.
Mwaka 1989 Bi. Zheng Xulan alikwenda Marekani na kuishi huko kwa miaka sita. Katika miaka hiyo kazi yake ilikuwa ni kulea mtoto, aliachana na muziki siku hadi siku. Katika miaka hiyo aliwahi kulazwa hospitali na kufanyiwa upasuaji mara mbili. Baada ya upasuaji wa mara ya pili alipokuwa bado hospitalini mchumba wake alipata saratani na kulazwa kwenye hospitali aliyolazwa. Kila siku aliamka kwa shida na kwenda kwenye kitanda mchumba wake kumfariji na kukaa naye mpaka alipofariki. Bi. Zheng Xulan alihuzunika sana kutokana na magonjwa na kifo cha rafiki yake, lakini pia aligundua kwamba hakuwa mtu mnyonge. Alisema,
"Naona taabu na balaa haziniangukia peke yangu, bali zipo kwa kila mtu kwa viwango tofauti. Ninapokuwa na shida navumilia na kuzuia machozi yasitoke nikipiga hatua siku hadi siku."
Maisha kama hayo wengine walifikiri pengine angeshindwa kuvumilia lakini Zheng Xulan alipita, anaona bahati yake si mbaya na amejaliwa kuweza tena kuendelea kuimba jukwaani. Anapofikiri hayo anaona amezaliwa kwa ajili ya muziki.
Yeye ni mtu kama anavyoimba kwenye wimbo wake unaoitwa "Ruka Njiwa": "Dhoruba inajaribu nia yako. Mvua inaimarisha mabawa yako. Ruka njiwa wangu, utakuwa shupavu kwenye dhoruba na mvua." Baada ya kupita dhoruba na mvua Bi. Zheng Xulan amejitokeza tena mbele ya watazamaji na nyimbo zake zinazovutia zaidi. Mwaka 1999 mwanamuziki wa Singapore mwenye asili ya China alikusanya muziki na nyimbo zote kwenye filamu ya "Ndoto kwenye Jumba Jekundu" na kuoneshwa jukwaani. Maonesho yalipooneshwa yalisifiwa sana. Bi. Zheng Xulan alisema,
"Mwanamuziki huyo anapenda sana muziki na nyimbo za filamu ya 'Ndoto kwenye Jumba Jekundu', alitaka kuonesha yote kwa pamoja kwenye maonesho. Maonesho yalipooneshwa yalitingisha Singapore, tokea hapo mpaka sasa tumeonesha mara zaidi ya 80 katika miji mingi."
Si barani Ulaya au Amerika ya Kaskazini bali popote penye watu wenye asili ya China nyimbo za Zheng Xulan zinapendwa sana. Ingawa siku hizi waimbaji vijana wanachipukia kwa wingi, lakini wasikilizaji wake wa zamani wanaendelea kumshabikia.
Idhaa ya kiswahili 2008-03-10
|