Mjini Taiyuan mkoani Shanxi kuna duka moja la zawadi lililoanzishwa na mgeni, duka hilo linaitwa nyumba dogo la Qiaoqiao. Zawadi zinazouzwa kwenye duka hilo ni pamoja na vitu vilivyochongwa kwa mizizi, mbao na jade kutoka Ulaya, Asia na Afrika. Habari zinasema hilo ni duka la kwanza lililoanzishwa na mgeni mkoani Shanxi. Waandishi wetu wa habari walitembelea duka hilo na kukutana na meneja wa duka hilo.
Waandishi wetu wa habari walipokuwa karibu na nyumba dogo la Qiaoqiao, walisikia muziki kutoka kwenye duka hilo. Baada ya kuingia waligundua kuwa muziki huo ulipigwa kwa marimba kutoka Afrika. Meneja wa duka hilo Bw. Mugodo Joseph aliwakaribisha waandishi wetu wa habari kwa kichina, alisema,
"Karibuni kwenye nyumba dogo la Qiaoqiao!"
Baba wa Bw. Joseph ni mhandisi wa ndege wa Zimbabwe, mama yake ni Mwingereza ambaye ni mwalimu. Duka lake lilianza kufanya kazi mwezi Septemba mwaka 2007. Kwenye duka hilo lenye eneo la mita 10 hivi za mraba, kuna zawadi za jade, kauri, na vitu vilivyochongwa kutokana na mizizi na mbao. Jina la duka hilo liliandikwa kwa rangi ya kibuluu kwenye ukuta. Bw. Joseph mwenyewe anapenda kutalii. Miaka mitano iliyopita alikuja China, aliishi mijini Shaoguan na Zhuhai mkoani Guangdong kwa miaka miwili, baadaye alitaka kutembelea sehemu za ndani ya China, hivyo alikwenda mkoa wa Shanxi. Mwanzoni alipanga kuishi mkoani humo kwa mwaka mmoja na halafu kwenda sehemu nyingine, lakini hivi sasa ameishi mkoani humo kwa miaka mitatu. Alisema,
"Mwanzoni nilipanga kuishi mkoani Shanxi kwa mwaka mmoja tu, lakini ninapoishi hapa kwa muda mrefu zaidi, napenda kuendelea kuishi hapa zaidi. Nilipofika hapa Taiyuan, watu walinikaribisha kwa ukarimu sana, na hii imenipa picha nzuri, hivyo niliishi hapa kwa mwaka mwingine mmoja, hivi sasa imetimia miaka mitatu, na sitaki kuondoka mkoa wa Shanxi, nauchukulia mkoa huu kuwa ni maskani yangu ya pili."
Kabla ya kuja China, Bw. Joseph aliwahi kutalii katika nchi nyingi. Kila alipotembelea sehemu fulani alinunua zawadi zenye sifa za kipekee. Baada ya kununua zawadi nyingi, alikuwa na wazo la kuanzisha duka lake. Siku zote anaamini kuwa penye nia pana njia, hivyo baada ya kuwa na wazo hilo, alianza kujaribu kutimiza matumani yake, alisema,
"Kabla ya kuanzisha duka langu, kwanza nilisoma habari husika, na nilitafuta mkalimani wa kunisadia, baadaye nilifanya juhudi kushughulikia mpango wangu na mwishowe nilifaulu."
Baada ya kumaliza maandalizi ya kuanzisha duka lake, Bw. Joseph aliwaalika marafiki zake, na kuwaambia mpango wake. Marafiki zake wote walishangaa sana. Bi. Li Yufeng ni rafiki mkubwa wa Bw. Joseph, lakini aliposikia mpango huo, pia alishangaa sana, alisema,
"Aliniambia kuwa alianzisha duka la zawadi, sisi sote tulishangaa sana, ingawa tulijua kuwa ana zawadi nyingi nzuri zilizonunuliwa kutoka sehemu mbalimbali, lakini hatukutarajia kuwa anaweza kuanzisha duka nchini China. Tuliona kuwa mpango wake ni mzuri sana, na tulimwunga mkono. Alipofungua duka lake, tulikwenda kumpongeza."
Bw. Joseph aliona kuwa wakati alipofanya maandalizi ya kufungua duka lake, wafanyakazi wa serikali ya huko walimpa msaada mkubwa, alisema,
"Nilipokuwa nafanya maandalizi, nilikwenda kwenye ofisi za idara mbalimbali za serikali, wafanyakazi wa idara hizo walinipa msaada mkubwa, na walirahisishia utaratibu wa kusajili duka langu."
Kuendesha duka hilo la zawadi ni jambo analopenda kufanya Bw. Joseph, kazi yake rasmi ni mwalimu wa Kiingereza wa chuo kikuu cha viwanda na biashara cha Shanxi, pia anafundisha Kiingereza katika vyuo vingine kikiwemo chuo cha mafunzo ya ufundi wa kazi cha Shanxi, na wakati fulani anafanya kazi ya muda ya kuwaanda watu wanaotaka kwenda kusoma katika nchi za nje. Kuhusu sababu ya kuendesha duka hilo, Bw. Joseph alisema,
"Lengo la kuendesha duka hili ni kuwawezesha watu wa Shanxi waweze kupata zawadi zilizotengenezwa katika sehemu mbalimbali duniani. Nataka marafiki zangu wa Uingereza na Zimbabwe wajue kazi zinazofanya hapa, pia naweza kuwaelezea habari kuhusu China. Tena naweza kupata marafiki wengi zaidi kwenye duka langu, Watu wanapotembelea duka langu, hunipatia kadi ambazo zimeandikwa maneno kama "Joseph, naweza kukutana na wewe?" au "tunaweza kucheza pamoja?" Hii ni njia nzuri ya kupata marafiki. Na wachina wanaweza kujua jinsi wageni walivyo. Tunaweza kumchukulia kila mtu kwa usawa, tuna moyo wa urafiki kwa kila mtu, kama kauli mbiu ya michezo ya Olimpiki ya Beijing ilivyosema, dunia moja, na ndoto moja!"
Bw. Joseph ana hamu kubwa kuhusu michezo ya Olimpiki ya Beijing. Tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2007, kampuni ya Lenovo ilianzisha uchaguzi wa wageni watakaoshika mwenge wa michezo ya Olimpiki kati ya wageni wanaoishi nchini China. Uchaguzi huo ulifanyika kwa vipindi viwili. Kwenye kipindi cha kwanza watu walipiga kura kwenye mtandao wa internet, ili kuwachagua wagombea 100. Bw. Joseph alipata habari kuhusu uchaguzi huo kwenye gazeti la China Daily, alijiandikisha haraka. Wageni zaidi ya mia 5 walishiriki kwenye uchaguzi huo. Bw. Josefu anaona kuwa ana bahati kuwa mmoja kati ya wagombea 100 waliochaguliwa, alisema,
"Nina bahati kuwa mmoja kati ya wagombea 100 waliochaguliwa. Baadaye walichagua wageni wanane waliopata kura nyingi zaidi, sikuwa na bahati kuwa mmoja kati ya watu hao wanane, lakini kuchaguliwa kuwa mmoja kati ya wagombea 100 ni jambo zuri, kwa sababu nilijiandikisha wiki moja tu kabla ya muda wa mwisho wa kujiandikisha."
Ingawa Bw. Joseph hakupata fursa ya kushiriki kwenye kipindi cha mwisho cha uchaguzi huo, lakini alipata zawadi ya kampuni ya Lenovo. Alisema atahifadhi zawadi hiyo katika maisha yake, kwani zawadi hiyo inaonesha kuwa ameshiriki kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing, pia inaonesha upendo wake kuhusu China.
Bw. Joseph ni mtu mwenye furaha na ndoto, ambaye anafanya juhudi kutimiza ndoto zake. Alisema ana matumaini kuwa atachaguliwa kuwa mtu anayejitolea kwenye michezo ya Olimpiki ya Beijing, ataanzisha maduka mengine ya zawadi katika miji mingine ya China, na ataoa na msichana mmoja wa mkoa wa Shanxi.
|