Kutokana na mazingira ya kimaumbile, baadhi ya watu wanaoishi kwenye mkoa unaojiendesha wa kabila la Tibet wanakabiliwa na matatizo ya kiuchumi. Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya China imeongeza nguvu ya kuwasaidia watu maskini wa mkoa huo. Mwaka 2006, China ilianzisha mradi wa kuwasaidia wafugaji wa mkoa wa Tibet kujenga nyumba mpya Katika miaka miwili iliyopita, imetenga zaidi ya Yuan bilioni saba na kuzisaidia familia laki 1.2 za wakulima na wafugaji wapatao laki 6 kujenga nyumba, na Bw. Ben Bha ni mmoja kati ya watu waliosaidiwa. Bw. Ben Bha ni mkazi wa tarafa ya Yangda ya mji wa Lahsa, sasa anaishi kwenye nyumba yake mpya aliyoijenga kwa msaada wa serikali ya China. Bw. Ben Bha alisema,
"Nilihamia kwenye nyumba hiyo mwaka 2007. Serikali ya mkoa unaojiendesha wa Tibet ilianzisha mradi wa kuwasaidia watu maskini kujenga nyumba mpya mwaka 2006. Nyumba yangu ilijengwa kutokana na mradi huo. Serikali ilinipa ruzuku ya Yuan elfu 24 ili kunisaidia kujenga nyumba hiyo. Zamani nyumba yangu ilikuwa mbovu, ndogo na chafu, na ndani yake hakukuwa na mwanga wa kutosha. Sasa nyumba yangu ni kubwa na nzuri, baba yangu anaweza kuishi maisha mazuri ya uzeeni."
Bw. Ben Bha alisema mbali na kuwapa ruzuku ya kujenga nyumba, serikali iliwapa wafugaji wa kabila la Watibet misaada katika sekta mbalimbali. Alisema,
"Serikali imetusaidia sana, imetimiza ahadi zake zote, ahadi hizo ni pamoja na kutoa ruzuku ya kujenga nyumba, ruzuku kwa wakulima na wafugaji na ruzuku kwa familia zenye matatizo ya kiuchumi. Licha ya hayo, serikali ilituandalia semina za ajira bila malipo. Kwenye semina hizo, walimu waliwafundisha wakulima na wafugaji teknolojia ya kisasa ya kilimo na ufugaji, na kuwafundisha watu wengine wanaopanga kutafuta kazi nyingine zisizo za kilimo na ufugaji ufundi wa ajira ikiwemo kutengeneza na kuendesha magari."
Kaka mdogo wa Bw. Ben Bha pia alinufanishwa na mpango wa serikali wa kuwasaidia watu wa kabila la Watibet wenye matatizo ya kiuchumi. Alijifunza ufundi wa ajira kutoka kwenye semina zilizoandaliwa na serikali, na sasa anafanya kazi kwenye sehemu ya nje na kupata mapato mazuri. Mwaka mpya wa jadi wa kichina ulipita hivi karibuni. Bw. Ben Bha alisema wanakijiji walisherehekea sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China katika nyumba mpya, furaha ilijaa moyoni mwao, kwa kuwa walihamia kwenye nyumba nzuri, na kupata ruzuku nyingine ya serikali, na walikuwa na pesa za kununua vitu vingi ili kusherehekea sikukuu ya mpaka mpya. Alisema,
"Zamani tuliishi maisha magumu, wakati wa sikukuu ya mwaka mpya wa jadi tuliweza kula vyakula vya kawaida kama vile viazi na figili tu, na hatukuweza kuweka akiba ya chakula kwa kuwa hatukuwa na jokofu. Sasa hali imebadilika, tunanunua vyakula vingi na kuvihifadhi kwenye jokofu mpaka sikukuu inapowadia. Aidha tumenunua vifaa mbalimbali vinavyotumiwa nyumbani. Zamani kwenye kijiji chetu kulikuwa na televisheni moja tu, wanakijiji wakitaka kutazama TV walitakiwa kulipa pesa. Lakini sasa kila familia ina televisheni, na maonesho kwenye televisheni yameboresha maisha yetu ya utamaduni."
Baba mzazi wa Ben Bha Bw. Purpu Tsering mwenye umri mkubwa amethibitisha mabadiliko makubwa ya watu wa kabila la Watibet katika miaka mingi iliyopita. Alipozungumzia maisha ya familia yake, alisema,
"Zamani familia yangu iliishi kwenye nyumba ndogo yenye eneo la mita za mraba 20. Baadaye tulikuwa na nyumba kubwa zaidi, lakini hatukuwa na vifaa vya kutosha vinavyotumiwa nyumbani, na tulikuwa na watoto wengi, nyumba hiyo bado haikutosha. Kutokana na sera nzuri ya serikali, sasa tumehamia kwenye nyumba nzuri. Sasa mimi nina umri wa miaka 67, ninafurahi sana kupata nyumba hiyo nzuri. Nyumba yetu mpya ni kubwa sana, hata mimi sikuweza kuizoea."
Damdren Wongdui mwenye umri wa miaka kumi ni mtoto mdogo zaidi wa Bw. Ben Bha. Baada ya kuhamia nyumba mpya alifurahi sana, alisema,
"Tulikuwa na televisheni mbili baada ya kuhamia kwenye nyumba mpya, pia tulinunua vifaa vingi vipya vya nyumbani, nilifurahi sana."
Maisha mapya ya familia ya Bw. Ben Bha hasa yanatokana na mpango wa serikali ya China wa kuwasaidia wakulima na wafugaji wa kabila la Watibet kujenga nyumba nzuri. Kutokana na msaada wa serikali, katika miaka mitatu ijayo, serikali ya mkoa unaojiendesha wa kabila la Watibet itatenga Yuan milioni 100 kila mwaka, ili kuharakisha mradi wa kuwasaidia wakulima na wafugaji kujenga nyumba, kuboresha nyumba za watu hao na kuwahamishia watu wenye matatizo ya kiuchumi hadi kwenye sehemu nzuri, na kuwawezesha asilimia zaidi ya 80 ya wakulima na wafugaji wa mkoa huo kupata nyumba nzuri. Inakadiriwa kuwa kutokana na utekelezaji mzuri wa mipango ya kuusaidia mkoa wa Tibet, hadi kufikia mwaka 2010, familia karibu elfu 30 za wakulima na wafugaji wa kabila la Watibet zitahamia kwenye nyumba mpya.
Idhaa ya kiswahili 2008-03-12
|