Ikilinganishwa na nchi za Ulaya na Marekani, mchezo wa mashua zenye matanga nchini China ulichelewa kuanza. Hivi sasa Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 inakaribia, ukiwa mji utakaoaandaa mashindano ya mashua zenye matanga wakati wa Michezo ya Olimpiki, Qingdao imeanza kuwahimiza watu wengi zaidi washiriki kwenye mchezo huo.
Katikati ya mwezi Februari mwaka 2008, kwenye kituo cha mashua zenye matanga cha Michezo ya Olimpiki kilichoko huko Qingdao, mamia ya wakazi wa huko walikusanyika kwenye kituo hicho kukaribisha mashua 10 zilizoshiriki kwenye Mashindano ya kupiga makasia kwa Mashua zenye Matanga, hususan zile makubwa zaidi zilizopewa jina la "Qingdao" zilizokuwa zinarudi bandarini.
Mashindano ya kupiga makasia ya mashua zenye matanga yalianzishwa na mwingereza Bw. Robin Knox-Johnston, na umbali wa mashindano hayo unafikia maili elfu 35. Tangu mashindano hayo yaanzishwe mwaka 1996, yamekuwa mashindano maarufu zaidi ya mashua zenye matanga duniani. Mwaka 2006, Qingdao ilishiriki kwenye mashindano hayo kwa mara ya kwanza kikiwa kituo kimoja cha mashindano hayo. Mwaka huu jambo linalowafurahisha wachina zaidi ni kuwa wachina watatu walishiriki kwenye mashindano hayo, nao ni Gao Jun na Dufei kutoka Qingdao, na Yan Xinmin kutoka Beijing. Akizungumzia kuhusu hisia zake za kushiriki kwenye mashindano hayo Bw. Yan Xinmin alisema:
"Naamini kuwa kushiriki kwenye mashindano hayo ni uzoefu muhimu kwa kila mtu, na watu wanaweza kunufaika na uzoefu wao na jamaa na marafiki zao, na kujiburudisha kutokana na uzoefu huo katika siku za baadaye. Kwa mimi binafsi, kutokana na kufanya ushirikiano na watu wenye utamaduni tofauti, nimeona tofauti kuhusu mitizamo katika kusafiri baharini, na kuwa na uwezo wa kufanya ushirikiano na watu wenye tamaduni mbalimbali, wanaozungumza lugha mbalimbali na kuwa na desturi tofauti."
Je, kwa Qingdao inayosifiwa kama ni "mji wa mashua zenye matanga wa China", mashindano hayo yana umuhimu gani kwake? Akizungumzia suala hilo naibu meya wa mji wa Qingdao ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa Kamati ya Mashua zenye Matanga ya Michezo ya Olimpiki Bibi Zang Aimin alisema:
"Mashindano ya kupiga makasia ya mashua zenye matanga yameleta nuru kwa Qingdao wakati inapofanya maandalizi kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki, pia yamepima uwezo wetu wa maandalizi na uendeshaji wa mashindano makubwa. Aidha yametoa mchango kwa ajili ya hatua ya Qingdao ya kuutangaza "mji wa mashua zenye matanga", kwani ukiwa "mji wa mashua zenye matanga" unapaswa kuandaa mashindano hayo ya kiwango cha juu duniani."
Tangu Qingdao iliposhiriki kwenye shughuli za Mashindano ya kupiga makasia kwa Mashua zenye Matanga, mji huo umezidi kuinua kiwango cha zana mbalimbali za uendeshaji wa mashua zenye matanga wakati wa kufanya maandalizi kwa ajili ya mashindano ya mashua zenye matanga ya Michezo ya Olimpiki, pia unajitangaza kwa dunia nzima kwa kupitia mashindano ya kupiga makasia ya mashua zenye matanga.
Lakini ukweli wa mambo unaonesha kuwa, mchezo wa mashua zenye matanga hauna mvuto mkubwa kama inavyoonekana, na unahitaji juhudi kubwa. Lakini kwa watu wengi, huu ndio mvuto wa mchezo huo. Mchezo wa mashua zenye matanga si kama tu unawasaidia watu kujenga mwili, kuongeza imani, na kuwasaidia washiriki kuongeza uwezo wa kukabiliana na hali mbalimbali za dharura.
Kwenye mashindano hayo, mwanamaji kutoka mji wa Qingdao Bibi Du Fei alikumbwa na tatizo baya la kupungukiwa na maji mwilini wakati wa safari ya kuelekea Singapore kutoka Qingdao, na hali ya ugonjwa huo ilihatarisha maisha yake, lakini imani imara ilimhimiza ashikilie mpaka mashindano kumalizika. Ingawa wanamaji watatu wa China walikabiliwa na matatizo mbalimbali wakati wa mashindano hayo, lakini walipata ufahamu wa kina zaidi kuhusu mchezo huo kwa kupitia mashindano hayo. Bw. Yan Xinmin alimkariri Bw. Robin Knox-Johnston akisema, kama kuna uwezekano, kila mtu anatakiwa kusafiri baharini, kwani uzoefu kama huu unaweza kubadilisha maisha yake.
Bw. Robin Knox-Johnston alianza safari yake baharini alipokuwa na umri wa miaka 17. Wakati aliposafiri baharini kwa mara ya kwanza, hali ya uhuru aliyohisi ilimfanya akumbuke safari hiyo daima. Alipoulizwa kuhusu safari iliyomwachia kumbukumbu kubwa zaidi katika miaka 50 iliyopita, mzee huyo alijibu kwa tabasamu: "daima itakuwa safari ijayo". Mwaka 2007 Bw. Robin aliyekuwa na umri wa miaka 68 alijipa changamoto na kushiriki kwenye mashindano ya mashua yenye matanga ya mabara matano duniani kwa mwanamaji mmoja mmoja, na alimaliza mara yake ya pili ya kusafiri yeye peke yake kuzunguka dunia bila kusita, Bw. Robin alisema:
"Safari ya Mara hii ya pili linifurahisha, kwani tulitumia mashua mpya na yenye kasi kubwa. Siku moja nilikumbwa na upepo mkubwa, na mashua ilikuwa ikienda kwa kasi zaidi, hali ya hatari iligusa hisia zangu kweli."
Ingawa mchezo wa mashua zenye matanga upo kwenye hatua ya mwanzo tu nchini China, lakini kadiri Michezo ya Olimpiki ya Beijing inavyokaribia, ndivyo wachina wengi zaidi wanavyojiunga na kushiriki kwenye mchezo huo wenye mvuto pekee.
Idhaa ya kiswahili 2008-03-18
|