Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-19 15:39:23    
Utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano vijijini wawanufaisha wakulima wa mji wa Xinzhou mkoani Shanxi

cri

Katika miaka ya hivi karibuni China imeweka mkazo katika kutekeleza utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano vijijini. Baada ya juhudi za miaka kadhaa, mji wa Xinzhou wa mkoa wa Shanxi ulioko katikati nchini China umefanya zaidi ya asilimia 80 ya wakulima wa mji huo waweza kunufaika na utaratibu huo.

Utaratibu mpya ya matibabu ya ushirikiano vijijini ni utaratibu wa kusaidiana katika shughuli za matibabu ambao wakulima wanajiunga kwa hiari. Utaratibu huo unakusanya fedha kwa njia ya malipo ya wanachama binafsi na misaada ya serikali, na utatoa ruzuku kwa wakulima wanachama waliolazwa hospitalini na kuhitaji gharama kubwa za matibabu.

Wilaya ya Xinfu ni wilaya yenye wakulima wengi zaidi mjini humo. Wilaya hiyo ilianza kutekeleza utaratibu huo mpya mwezi Februari mwaka 2007, kila mkulima anaweza kujiunga na utaratibu kwa kulipa Yuan 15 tu. Wakulima wote wanaupongeza sana utaratibu huo. Mkurugenzi wa idara ya huduma za afya ya wilaya hiyo Bw. Li Wentian alisema:

"kwa mujibu wa wakulima, kutumia Yuan 15 tu kuna faida kubwa zaidi kuliko kuwa na mtoto. Wakati wakipatwa na magonjwa, kama mtoto wao hana uwezo wa kulipia gharama za matibabu, itakuwa vigumu kabisa kwao kulipa gharama hizo. Lakini sera hiyo nzuri imeondoa wasiwasi wetu, wakulima wote wanashukuru kwa dhati chama na sera za serikali yetu."

Bi. Huang Chaoxiu mwenye umri wa miaka 67 ni mkulima wa kijiji cha Gao Jiazhuang mjini humo. Mwezi Aprili mwaka 2007 alijeruhiwa vibaya kutokana na kuanguka ndani ya mfereji alipokuwa anakwenda shambani kwa Baiskeli. Baada ya kupelekwa hospitali Bi. Huang Chaoxiu alifanyiwa upasuaji uliodumu kwa saa 11, hatimaye maisha yake yalinusurika. Lakini baada ya kupata fahamu, Bi. Huang Chaojiu mara moja aliingiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu gharama kubwa za matibabu. Familia ya Bi. Huang Chaoxiu haina pato kubwa, na pia inapaswa kumtunza mzee mwenye umri wa miaka 98. Hali hiyo ilimtia wasiwasi Bi. Huang Chaoxiu. Ili kuondoa wasiwasi wake, daktari aliuliza hali mbalimbali za familia yake, alipojua kuwa Bi. Huang Chaoxiu ni mwanachama wa utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano, daktari alimwambia asiwe na wasiwasi kabisa. Bi. Huang Chaoxiu alisema:

"daktari aliniuliza kama nilijiunga na utaratibu wa matibabu ya ushirikiano, nilijibu kuwa ilijiunga, basi daktari aliniambia nisiwe na wasiwasi na niendelee na matibabu. Kama gharama ni Yuan elfu 10, ninapaswa kulipa Yuan elfu 5 tu."

Lakini Bi. Huang Chaoxiu bado alikuwa haamini, baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi miwili, aling'ang'ania kurudi nyumbani. Bi. Huang Chaoxiu alisema:

"halafu nilitaka kurudi nyumbani, bila kuhesabu gharama za chakula, ilikuwa inagharimu Yuan 50 hadi 60 kila siku kwenye hospitali. Baada ya kurudi nyumbani bado sikuamini maneno ya daktari, nilitumia pesa nyingi mno, ningelipa mpaka lini?"

Baada ya siku 10 tu, Bi. Huang Chaoxiu alipokea simu kutoka ofisi ya utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano ya wilaya ya Xinfu, aliambiwa kuwa gharama za matibabu zimehesabiwa tayari na aliweza kwenda kwenye ofisi hiyo kuchukua pesa. Bi. Huang Chaoxiu alisema:

"mwanangu mkubwa alienda kuchukua Yuan elfu 12, gharama zote za matibabu zilikuwa ni Yuan elfu 24, serikali ilinilipia Yuan elfu 12. Nilipofahamu hivyo nilifurahi sana, na ugonjwa wangu uliendelea kupona siku hadi siku"

Bi. Huang Chaoxiu alipokumbuka wakati mtoto wake akirudi na pesa, aliendelea kuwa na furaha. Alisema:

"naona kuwa sera ya chama kwa kweli ni nzuri sana, kweli imetunufaisha sisi wakulima tuliojiunga na utaratibu wa matibabu ya ushirikiano."

Mjini Xinzhou wakulima wengi walikuwa na uzoefu kama ilivyokuwa kwa Bi. Huang Chaoxiu. Naibu mkurugenzi wa idara ya afya ya mji huo Bw. Gao Fanghua alisema, tangu utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano uanze kutekelezwa kuanzia mwaka 2003, hivi sasa wakulima milioni 1.61 kutoka wilaya 10 wamejiunga na utaratibu huo. Katika hali hiyo, idara ya afya ya mji huo itaweka mkazo katika kazi za usimamizi na kusikiliza maoni na mapendekezo ya wakulima kuhusu utaratibu huo. Bw. Gao Fanghua alisema:

"tunatembelea wilaya 14 zenye tarafa 185, tunakwenda vijijini na kutembelea kila familia ili kusikiliza maoni ya wakazi wa huko. Tunataka kufanya juhudi kadri iwezekanavyo kuwapa huduma nzuri na teknolojia bora, ili kuridhisha na kunufaisha kihalisi wakulima hao."

Hivi karibuni rais Hu Jintao wa China alipofanya ukaguzi mkoani Anhui alisisitiza kuinua zaidi kiwango cha ruzuku ya matibabu kwa wakulima mwaka huu, rais Hu jintao alisema:

"serikali kuu imeamua kuongeza ruzuku ya bima ya matibabu kutoka Yuan 40 ya mwaka huu hadi kufikia Yuan 80 baada ya miaka miwili, na kiwango cha matibabu ya ushirikiano pia kitaendelea kuinuka. Si watu wanaona vigumu kupata matibabu au hawawezi kumudu kulipia matibabu? Sasa serikali itatatua tatizo hilo kwa wakulima hatua kwa hatua."

Utaratibu mpya wa matibabu ya ushirikiano vijijini ulianza kutekelezwa mwaka 2003 na unaendelea vizuri. Wataalamu wanakadiria kuwa ifikapo mwaka 2010 sera hiyo itatekelezwa kwenye vijiji vyote na kuwanufaisha wakulima wote kote nchini China.