Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-20 16:46:34    
Familia ya Montpellier yaimarisha urafiki kati ya China na Ufaransa

cri

Mjini Chengdu, kusini magharibi mwa China, kuna familia ya Montpellier, ambayo ilianzishwa mwaka 2006 na mji wa Chengdu uliopo China na mji wa Montpellier wa nchini Ufaransa. Familia ya Montpellier inachukuliwa kuwa ni "balozi" wa kupashana habari za uchumi, utamaduni na historia kati ya miji ya Chengdu na Montpellier, inahimiza mawasiliano na ushirikiano wa sekta mbalimbali kati ya miji hiyo miwili na nchi hizo mbili. Sasa watu wengi kutoka mji wa Montpellier wanafanya kazi, kujifunza na kuishi mjini Chengdu, na mara kwa mara wanajifunza lugha ya Kichina na michezo ya sanaa katika familia ya Montpellier. Katika muda mfupi uliopita, mwandishi wetu wa habari alikwenda kwenye familia ya Montpellier, na kukutana na marafiki kadhaa kutoka Ufaransa.

"Nilipokuwa nchini Ufaransa nilikuwa nakumbuka vyakula vya kichina, lakini nikiwa nchini China sikumbuki vyakula vya kifaransa."

"Mji wa Chengdu ni wa kisasa, watu wa hapa wanajua kujistarehesha katika maisha, mji huo una mvuto wake mkubwa wa kimaisha."

"Nimejifunza vitu vingi hapa, kama vile kucheza ngoma, Wushu na Beijing opera, na maisha ya hapa ni ya kufurahisha."

Mwaka 1981 miji ya Montpellier na Chengdu ilijenga uhusiano wa miji rafiki. Familia ya Montpellier iko katikati ya mji wa Chengdu, mkurugenzi wa familia ya Montpellier Bibi Liu Jinghong alisema, Chengdu na Montpellier ni miji ya kwanza kati ya China na Ufaransa iliyoanzisha ushirikiano. Alisema,

"Ingawa inaitwa 'familia ya Montpellier mjini Chengdu', ambayo ni dirisha la kuitangaza Montpellier mjini Chengdu, lakini kwa kweli kwa mji wa Montpellier, sisi ni dirisha la kutangaza Chengdu. Wafaransa wengi wakiwemo watu wa Montpellier wanafahamu zaidi mji wa Chengdu kwa kupitia dirisha letu hilo."

Bibi Stephanie Valette aliyetoka mjini Montpellier, Ufaransa. Anaupenda sana mji wa Chengdu, na ameishi mjini Chengdu kwa miaka miwili, hadi sasa bado anajifunza lugha ya Kichina katika familia ya Montpellier. Akizungumzia tofauti kati ya Paris na Chengdu, alisema, ingawa watu wengi wanaona kuwa Paris ni mji wenye hali ya starehe zaidi, lakini naona kuwa, sasa maisha huko hayana mvuto, lakini maisha ya hapa Chengdu ni ya raha starehe, na watu wa hapa wana adabu sana.

Familia ya Montpellier imekuwa daraja la kufahamishana kati ya miji ya Chengdu na Montpellier na nchi za China na Ufaransa. Bibi Liu Jinghong ni balozi wa kiutamaduni. Yeye ni mwenyeji halisi wa Chengdu, baada ya kuhitimu kutoka Chuo cha lugha za kigeni cha Sichuan, mwaka 2002 alishiriki kwenye mradi wa mawasiliano wa utoaji mafunzo uliofanywa na China na Ufaransa, na kwenda kusoma mjini Montpellier. Alisomea kozi ya usimamizi na mazungumzo ya miradi ya kimataifa, na alipata shahada ya pili. Wakati familia ya Montpellier ilipoanzishwa, alichaguliwa na serikali za miji ya Montpellier na Chengdu kuwa mkurugenzi wa familia ya Montpellier. Alisema,

"Kwa kuwa ninafahamu hali za miji hiyo miwili, hivyo serikali za miji hiyo miwili ziliona kuwa ni jambo mwafaka kwa mimi kufanya kazi katika familia ya Montpellier."

Familia ya Montpellier mjini Chengdu sio tu inatoa huduma kwa wakazi wa Chengdu, bali pia inatoa huduma kwa kampuni na watu kutoka Montpellier. Bibi Liu Jinghong alisema,

"Baadhi ya wakazi wa Chengdu wana hamu ya kujua utamaduni wa Ufaransa au Montpellier, watakuja hapa kupata ushauri husika kuhusu mambo ya utamaduni, utalii na ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, na sisi tutawahudumia. Wakati huohuo, baadhi ya kampuni na watu wa Montpellier, huenda wanataka kutafuta nafasi kujiendeleza mjini Chengdu, au kutalii au kukaa kwa muda mfupi, watawasiliana nasi kwa kupitia E-mail au kutupigia simu, sisi pia tunawapa habari, mashauri au maoni husika."

Bw. Alexandre Beaudoux kutoka mji wa Montpellier alikuja mjini Chengdu kwa ajili ya kutafuta fursa ya maendeleo. Kabla ya kuja mjini Chengdu, aliwahi kusoma katika chuo kikuu mjini Shanghai. Mwezi Septemba mwaka 2007, alijifunza kozi ya uchumi na biashara katika Chuo Kikuu cha Sichuan mjini Chengdu. Alisema sababu muhimu ya kuja Chengdu ni kuwa hapa kuna viwanda na makampuni mengi, hii inamaanisha kuwa hapa kuna soko kubwa.

Katika familia ya Montpellier, mwandishi wetu wa habari pia alimkuta "mtaalam wa mambo ya China"?Bibi Cyrielle Perilhon, mwenye ufahamu mkubwa kuhusu utamaduni wa China. Alisema anapenda sana lugha ya Kichina na Beijing opera, aliposoma katika sekondari ya juu nchini Ufaransa alijifunza lugha ya Kichina. Baadaye alipata msaada wa masomo, na kuja nchini China kujifunza lugha ya Kichina, Beijing opera na opera nyingine. Alisema,

"Mimi ninaitwa Cyrielle Perilhon, kutoka mjini Montpellier, Ufaransa. Nilipokuwa mwanafunzi wa shahada ya pili huko Montpellier, makala ya taaluma niliyoandika ilihusu maendeleo ya Beijing opera. Sasa nimekuja nchini China kutokana na kupata udhamini wa masomo, naweza kufanya mazoezi katika familia ya Montpellier, huku ninajifunza lugha ya Kichina na kucheza ngoma katika Chuo Kikuu cha Chengdu. Licha ya hayo, nikiwa na wakati, ninatafuta mwalimu wa Beijing opera na mwalimu wa Wushu, na kujifunza Beijing opera na Wushu kutoka kwao."

Akiwa Mfaransa, Bibi Cyrielle Perilhon pia anafurahia maisha yake baada ya kazi mjini Chengdu. Akiwa na wakati, anatembelea mtaa wa vyakula mbalimbali wa Jinli, pia anatembelea mtaa wa kisasa wa Chunxi, ambapo kuna maduka mengi, wakati fulani pia anakwenda kwenye mkahawa wa chai kunywa chai huku akitazama maonesho ya opera ya Chuan. Alisema, ukiingia kwa undani kwenye maisha ya wakazi wa huko, ndipo unaweza kufahamu zaidi utamaduni wa huko. Alisema anapenda sana maisha ya furaha mjini Chengdu.

Mkurugenzi wa familia ya Montpellier Bibi Liu Jinghong alisema, familia ya Montpellier mjini Chengdu inarahisisha mawasiliano ya miji ya Chengdu na Montpellier, pia inahimiza mawasiliano ya miji hiyo miwili. Kwa upande wa kuendeleza utamaduni, jamii, matibabu na uchumi, familia ya Montpellier imekuwa kama daraja la miji hiyo miwili kuwasiliana na kushirikiana, vilevile ni alama ya urafiki kati ya China na Ufaransa.

Idhaa ya kiswahili 2008-03-20