Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2008-03-25 20:26:15    
Barua 0323

cri

Msikilizaji wetu wa sanduku la posta 209 Songea Ruvuma Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, ana tumaini kuwa hatujambo na tunaendelea na kazi zetu kama kawaida, yeye hajambo ana hofu na sisi tu tulio mbali naye japo matangazo ya Radio China Kimataifa yanamfanya awe karibu nasi kwa saa chache kila siku. Msikiliza huyu anataka kutuambia kuwa yeye ni mtoto wa kiume wa Bw. Kaziro Dutwa, na amekuwa akimuona baba yake akirejea mapema kila siku jioni na kukaa katika kusikiliza radio, awali hakujua kuwa alikuwa anasikiliza radio au idhaa gani? Hadi mwaka jana alipomuona akisikiliza radio kwa makini sana jambo lililomvuta kukaa karibu naye ndipo aliposikiliza habari zinazohusu ujenzi wa viwanja mbalimbali kwa ajili ya Michezo ya Olimpiki ya Beijing mwaka 2008.

Anasema kuwa alivutiwa sana na maelezo ya kiwanja kimoja ambacho sherehe za ufunguzi na ufungaji wa Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya mwaka 2008 zitafanyika hapo , kiwanja hicho kilikuwa na maelezo mengi juu ya ujenzi wake, na kwa mujibu wa mhandisi wake, iliwabidi kukibadilisha kutokana na utata uliokuwepo juu ya ujenzi wake! Uwanja huo umepewa jina la "Kiota", yeye alishangaa sana kusikia jina hilo kwani kila akitazama kiota cha ndege anajiuliza inayumkinika vipi uwanja wa michezo wa taifa wa China ukafanana na kiota cha ndege?

Tangu hapo amekuwa akitaka kujua mengi juu ya China na uhandisi wa Kichina vilevile amekuwa akitamani sana kuona kiota kilichojengwa na binadamu, amejaribu kumdadisi baba yake ampe picha kamili juu ya "kiota" hicho cha ndege hakika amejaribu sana kumfafanulia lakini bado hajasema wazi ni kiota cha ndege gani ambacho uwanja wa michezo unamithilishwa nacho? Ni hua, kitwitwi, kizamia dagaa, mnandi, furukombe, mraruasanda au Yangeyange? Hajaelewa vizuri hivyo anaomba ufafanuzi zaidi kwani akili yake ni changa ndio kwanza yupo darasa la sita mwaka huu. Angepata vielelezo kama picha ya uwanja huo angalisaidiwa sana; kwenye magazeti na majarida, kadi na barua mbalimbali zilizosheheni kwenye maktaba ya baba yake ni za toka miaka ya 80, ni jarida moja tu linaloonesha uwanja huu kwa picha ndogo ya pembeni. Anaomba kama kuna uwezekano tumtumie kielelezo chochote kinachoonesha taswira ya uwanja huo wa michezo wa taifa, atafurahi sana kutuliza hisia na ndoto zake juu ya uwanja huo ulio wa ajabu kwani picha nyingi sana za uwanja huo zimepita kichwani mwake, lakini hafahamu wazi uwanja huo utakuwa na picha gani. Hapa anapenda kushiriki mara ya kwanza katika mashindano ya chemsha Bongo, na anaomba tumpokee kama mwanachama wetu mpya, atafurahi sana kama tutampokea.

Tunamshukuru sana mtoto wa Bw. Kaziro Dutwa kwa kututumia barua na kueleza ombi lake kuhusu kufahamishwa zaidi uwanja wa michezo wa taifa ambao unaitwa pia kuwa ni Kiota, kwani umbo lake la nje ni kama lile la kiota cha ndege, lakini hatuwezi kusema ni ndege gani. Maelezo ya barua yake hiyo yametufurahisha sana, na tunamkaribisha kwa mikono miwili ajiunge nasi, ni matumaini yetu kuwa atasikiliza matangazo yetu kila mara, ili kupata habari nyingi zaidi kuhusu China na mambo mbalimbali ya China. Kama tutapata picha ya uwanja huo wa michezo tutakutumia.

Msikilizaji wetu Mchana J. Mchana wa Morogoro Tanzania ametuletea barua pepe juzi juzi anasema, anapenda kutoa pole kwa wakazi wa Lhasa Mkoani Tibet kwa machafuko yaliyotokea hivi karibuni, anaungana nao kwa majonzi kwani kupoteza mali na vifo ni tatizo kwa binaadamu. Yeye analaani moja kwa moja vyombo vya habari vya magharibi ambavyo vimekua ni wachochezi wakubwa, hii inaonesha kuwa kuna vyombo mahususi kwa ajili ya uchochezi tu. Anasema kundi la wafarakanishaji la Dalai ambalo lipo nje ya China, ambalo yeye anaona kuwa linafanya njama, popote pale ukitumiwa kwa kusaidiwa pesa au chochote, basi ujue kuwa hiyo ni njama inayokufanya umsaliti hata mzazi wako. Anaomba viongozi wa China washikamane na wawe kitu kimoja waidhibiti hali iliyotokea huko Lahsa, kwani baadhi ya watu hawapendi kuona China inavunja rekodi ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki kwa utulivu wa hali ya juu.

Bw Mchana anaitaka China isikubali kuvunjika moyo, na iendelee na mandalizi ya michezo ya Olimpiki ili adui wetu abaki na aibu. Anasema watanzania wanaungana na wachina na kuzidi kumuomba mungu awaepushe na wabaya wote wasiopenda maendeleo. Mungu ibariki China wabariki waandaaji wa michezo ya Olimpiki uwajaze roho ya kugundua njama zozote zile.

Msikilizaji wetu Fadhili Sibili ametuletea barua pepe pia anasema, anaamini vurugu zinazotokea huko Tibet ni kazi ya nchi fulani, yeye anasema aligundua tokea mwezi Januari mwaka jana pale alipopata gazeti kutoka Marekani ambalo lilikuwa linatoa maelezo kuhusu nchi fulani inavyowasaidia watu wa Tibet dhidi ya serikali ya China, ni gazeti ambalo lilijaa maelezo mengi kuhusu Tibet tu, kwa maana hiyo yeye anaona kuwa ni mpango wa muda mrefu sana, na hiyo ilikuwa dhidi ya Michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwezi Agosti mwaka huu mjini Beijing, China, madhumuni hasa makuu ni kuzorotesha nguvu za kisiasa za China ulimwenguni pamoja na ukuaji wa kiuchumi wa China. Nchi fulani ina malengo kadha kwa kadha kwa namna fulani, kuifanya China iwaache waandamanaji waendelee kufanya uharibifu au vinginevyo vyovyote vile, hata hivyo anaamini kuwa juhudi zao haziwezi kufanikiwa. Anasema angeweza kuandika mengi zaidi lakini kwa leo ameamua kuishia hapa.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu waliotuletea barua kueleza maoni yao kuhusu tukio lililotokea huko Lahsa mkoani Tibet, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China siku hizi amesema, ghasia zilizotokea huko Lahsa, Tibet zilipangwa na kuzushwa na Kundi la Dailai kwa kusudi la kufarakanisha taifa. Lakini toka vurugu hizo zitoke siku chache zilizopita, sasa hali ya utaratibu wa jamii ya Lahsa iko shwari kimsingi, na watu wameanza kuendelea na shughuli za kila siku kama kawaida. Sasa tunapenda kuwaletea maelezo kuhusu hali ya Tibet.